Hamia kwenye habari

OKTOBA 14, 2015
URUSI

Wataalamu Wapinga Uamuzi wa Urusi wa Kupiga Marufuku JW.ORG

Wataalamu Wapinga Uamuzi wa Urusi wa Kupiga Marufuku JW.ORG

ST. PETERSBURG, Urusi—Julai 21, 2015, Shirikisho la Urusi lilipiga marufuku jw.org, tovuti rasmi ya Mashahidi wa Yehova, na kutangaza kwamba ni kosa la jinai kuhamasisha watu watembelee tovuti hiyo ndani ya shirikisho hilo. Urusi ni nchi pekee ulimwenguni iliyopiga marufuku jw.org.

Yekaterina Elbakyan, mtaalamu wa masomo ya dini na profesa wa Chuo cha Mahusiano ya Kazi na Jamii kilichopo jijini Moscow, anasema hivi kuhusu jw.org: “Nafikiri tovuti hiyo ni muhimu sana kwa sababu ina habari zisizo na upendeleo kutoka kwa Mashahidi wa Yehova kuhusu tengenezo lao na si kutoka chanzo kingine. . . . Tovuti hiyo inapendwa na washiriki wa dini hiyo na pia watu wengine wanaopenda habari za dini. Watu hao wanatia ndani wasomi wa dini kama mimi na pia waandishi wa habari wanaoandika habari za dini.”

“Nafikiri Tovuti hiyo ni muhimu sana kwa sababu ina habari zisizo na upendeleo zinazotoka moja kwa moja kwa Mashahidi wa Yehova”— Yekaterina Elbakyan, Profesa, Chuo cha Mahusiano ya Kazi na Jamii, Moscow

Lev Levinson, mtaalamu wa sheria katika Taasisi ya Haki za Binadamu jijini Moscow, anazungumzia jambo hilo akifikiria historia ya nchi hiyo: “Urusi ya karne ya ishirini na moja ina katiba ambayo inahakikisha kutakuwa na uhuru wa ibada na usawa wa mashirika ya dini. Hata hivyo, kama ilivyokuwa katika karne ya 19, kwa mara nyingine Urusi inazuia uhuru wa watu kuwaeleza wengine maoni ya dini zao kwa kunyang’anya machapisho na kupiga marufuku tovuti. Na mambo hayo yanafanywa na majaji na wataalamu ambao hutumia sheria zisizo halali wakisingizia wanapambana na watu wenye msimamo mkali.”

Marufuku hiyo ndiyo tukio la karibuni katika mapambano ya kisheria yaliyoanza mwaka 2013. Agosti 7 mwaka huo, mahakama ya wilaya nchini humo iliendesha kesi kwa siri na kutangaza Tovuti hiyo kuwa “ina habari zenye msimamo mkali wa dini”, lakini uamuzi huo ulibadilishwa na mahakama ya mkoa Januari 22, 2014. Hata hivyo, Makamu Wakili Mkuu wa Shirikisho la Urusi alikata rufaa kwenye Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi akipinga uamuzi wa mahakama ya mkoa. Desemba 2, 2014, Mahakama Kuu ilisikiliza rufaa hiyo bila Mashahidi kuwepo ili wajitetee, kwa kuwa hawakuwapa taarifa kamili. Mahakama Kuu ilirudisha tena uamuzi wa mahakama ya wilaya. Hata ingawa mahakama hiyo ilikiri kwamba Tovuti hiyo haikuwa tena na habari za dini zilizopigwa marufuku na wenye mamlaka nchini Urusi ilitangaza kuwa habari zote kwenye Tovuti hiyo “zinachochea watu kuwa na msimamo mkali.” Mashahidi walipinga uamuzi huo na kukata rufaa kwa mwenyekiti wa Mahakama Kuu hata hivyo hawakufanikiwa. Kutokana na uamuzi huo, Julai 21, 2015, Wizara ya Haki ya Shirikisho la Urusi iliingiza tovuti hiyo kwenye Orodha ya Serikali ya Habari Zinazowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali na hivyo kupiga marufuku tovuti kotekote nchini Urusi.

Yaroslav Sivulskiy, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi, anazungumzia athari za marufuku hiyo: “Tunasikitika kwamba wenye mamlaka nchini Urusi wamechukua hatua hii isiyo na msingi. Marufuku hiyo inazuia ibada ya watu zaidi ya 170,000 ambao ni Mashahidi wa Yehova. Lakini pia watu 285,000 nchini Urusi wanatembelea tovuti hiyo kila siku, ni wazi kwamba hata wale ambao si washiriki wa imani yetu wamenyimwa chanzo bora cha habari za kujifunza Biblia.”

Akizungumza kutoka kwenye makao makuu ya Mashahidi huko Brooklyn, New York, J. R. Brown, msemaji wa kimataifa wa Mashahidi wa Yehova, anasema: “Tovuti yetu rasmi, jw.org, ina video zilizoshinda tuzo, machapisho ya kujifunzia Biblia katika mamia ya lugha, na magazeti mawili yanayosambazwa kwa wingi zaidi duniani, Mnara wa Mlinzi na Amkeni! Imetumiwa katika maonyesho makubwa ya kimataifa ya vitabu na katika shule mbalimbali. Imewanufaisha watu wengi duniani na ilitumiwa sehemu nyingi nchini Urusi. Kwa kweli, hii ni tovuti inayopaswa kutangazwa.”

Vyombo vya Habari Vinaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Urusi: Yaroslav Sivulskiy, simu +7 812 702 2691