Hamia kwenye habari

JUNI 8, 2017
URUSI

Rais Putin Awapa Mashahidi wa Yehova Tuzo ya Mzazi Bora

Rais Putin Awapa Mashahidi wa Yehova Tuzo ya Mzazi Bora

NEW YORK—Mei 31, 2017, Rais wa Urusi Vladimir Putin aliwapa Valeriy na Tatiana Novik tuzo ya “Mzazi Bora” katika sherehe jijini Moscow kwenye makao ya rais huyo. Wao ni Mashahidi wa Yehova wanaoishi Karelia, na wamelea watoto wanane.

Sherehe hiyo ilifanywa Kremlin siku moja kabla ya Siku ya Kimataifa ya Watoto.

Tuzo ya “Mzazi Bora” ilianzishwa na rais mnamo Mei 2008. Urusi huwapa tuzo hiyo wazazi ambao wamelea angalau watoto saba. Wazazi hao wanapaswa kuwa wametunza wote katika familia kwa njia ya pekee wakiwa na afya, elimu, na ukuzi unaofaa wa kimwili, kiakili, na kimaadili. Familia zinazopewa tuzo hiyo huonwa kuwa mfano mzuri wa kuigwa na familia nyinginezo ambazo zingependa kuwa imara pia.

Valeriy Novik, baba mwenye watoto wanane, akipokea tuzo ya “Mzazi Bora” kutoka kwa Rais Putin.

David A. Semonian, msemaji wa Mashahidi wa Yehova katika makao yao makuu, anasema hivi: “Tunaona tuzo hiyo kuwa uthibitisho kwamba elimu ya Biblia inayotolewa ulimwenguni pote na Mashahidi wa Yehova bila malipo inasaidia wazazi na watoto wao kuwa raia bora si nchini Urusi tu bali ulimwenguni pote. Tunatumaini kwamba tuzo hii iliyotolewa na Rais Putin itazingatiwa Julai 17, 2017, Mahakama Kuu ya Urusi inapochunguza upya uamuzi wa kupiga marufuku Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova nchini Urusi.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu, +1-845-524-3000