Hamia kwenye habari

NOVEMBA 28, 2014
URUSI

Rufani Yakatwa Kwenye Mahakama ya Wilaya ya Rostov—Je, Mashahidi wa Yehova Wataondolewa Mashtaka au Watafungwa?

Rufani Yakatwa Kwenye Mahakama ya Wilaya ya Rostov—Je, Mashahidi wa Yehova Wataondolewa Mashtaka au Watafungwa?

Desemba 11, 2014, Mahakama ya Wilaya itasikiliza rufani kuhusu kesi ya uhalifu dhidi ya Mashahidi 16 wa Yehova huko Taganrog, Urusi. Walishtakiwa kwa kuhudhuria na kufanya mikutano ya kidini yenye amani.

Matatizo ya Mashahidi yalianza 2011, wenye mamlaka walipofanya upekuzi ndani ya nyumba zao na kurekodi kisiri mikutano yao ya kidini. Hilo lilifanya wafunguliwe mashtaka ya uhalifu. Julai 30, 2014, baada ya kesi iliyochukua miezi 15, Mahakama ya Jiji la Taganrog iliwahukumu Mashahidi saba. Jaji aliwatoza faini kubwa Mashahidi hao saba na kuwahukumu wanne kati yao vifungo virefu gerezani, lakini akaondoa faini hizo na kuahirisha vifungo vyao baada ya muda mfupi. Jaji aliwaondolea mashtaka Mashahidi wale wengine tisa kwa sababu ya kukosa ushahidi, lakini aliunga mkono kwamba walijihusisha na shughuli zenye msimamo mkali. Mashahidi wote 16 wamekata rufani, wakiomba waondolewe mashtaka yote ya uhalifu.

Mwendesha-mashtaka pia amekata rufani. Anaomba Mahakama ya Wilaya ya Rostov iwafunge Mashahidi hao wanne, ambao ni wahudumu wa kidini, na wawekwe korokoroni baada ya kesi kusikilizwa. Pia aliiomba mahakama ibadili uamuzi kuhusu Mashahidi wale wengine tisa na iwahukumu kuwa na hatia ya kujihusisha na shughuli zenye “msimamo mkali.”

Vasiliy Kalin, mwakilishi wa Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova nchini Urusi, alisema hivi: “Natumaini kwamba Mahakama ya Wilaya ya Rostov itaona ukosefu wa haki ambao tayari waathiriwa 16 wa ukandamizaji wa kidini wamevumilia na kuwaondolea hukumu ya uhalifu ambayo wamehukumiwa.”