Hamia kwenye habari

Jumba la Kusanyiko la Kolomyazhskiy lililoko St. Petersburg

DESEMBA 25, 2017
URUSI

Wenye Mamlaka Nchini Urusi Wachukua Jumba la Kusanyiko la Mashahidi wa Yehova

Wenye Mamlaka Nchini Urusi Wachukua Jumba la Kusanyiko la Mashahidi wa Yehova

Desemba 14, 2017, wenye mamlaka walivunja Jumba la Kusanyiko la Mashahidi wa Yehova lililoko Kolomyazhskiy jijini St. Petersburg, wakaweka ishara ya kuzuia watu wasiingie na kuweka ulinzi katika jengo hilo. Hakuna Shahidi wa Yehova yeyote aliyejeruhiwa wakati wa uvamizi huo, na jengo linaonekana halijaharibiwa.

Picha ya kamera ya ulinzi inayoonyesha maofisa wa Urusi wakifanya uvamizi

Jumba la Kusanyiko ndilo jengo kubwa ambalo wenye mamlaka nchini Urusi wamelichukua kutoka kwa Mashahidi wa Yehova tangu kutolewa kwa uamuzi wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Shirikisho la Urusi wa Julai 17, 2017. Uamuzi wa Mahakama Kuu uliagiza kufungwa kwa mashirika yote ya kisheria ya Mashahidi, kupigwa marufuku kwa utendaji wake, na kutaifishwa kwa mali zake.

Maofisa wakiwa ndani ya Jumba la Kusanyiko

Watu 1,500 wanaweza kuketi kwenye Jumba hilo la Kusanyiko na lilikuwa likitumiwa kwa ajili ya mikutano mikubwa ya kidini na pia lilitumiwa na makutaniko ya eneo hilo baada ya kufanyiwa marekebisho mwaka wa 2002. Mawakili wa Mashahidi wamegundua kuwa wenye mamlaka walikuwa wamelisajili upya Jumba hilo la Kusanyiko na sasa linamilikiwa na Shirikisho la Urusi. Jengo hilo tayari limekabidhiwa kwa mmiliki mpya, na limefanywa kuwa kituo cha afya na tayari wameweka bango jipya kwenye mwingilio wa jengo hilo.

Uvamizi huo umetukia juma moja baada ya uamuzi wa mahakama ambao unatishia kuchukuliwa kwa jengo lililotumiwa na Mashahidi wa Yehova kama makao yao makuu ya taifa, lililoko karibu na jiji la St. Petersburg. Uamuzi huo ulibatilisha mkataba uliofanywa miaka 17 iliyopita kati ya makao makuu ya Mashahidi nchini Urusi na shirika la kisheria la Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania. Ikiwa wakati wa rufaa mahakama itaunga mkono uamuzi huu, hilo litafungua njia kwa wenye mamlaka nchini Urusi kupora jengo hilo na mali nyingine nyingi za Mashahidi zilizoko Urusi ambazo zinamilikiwa na mashirika yaliyo nje ya nchi hiyo.

Mashahidi wa Yehova wanaona matendo ya serikali ya Urusi kuwa ubaguzi mkubwa wa kidini, ambao si tuunawanyima uhuru wao wa kuabudu bali pia mali zao zinachukuliwa—ambazo nyingi kati hizo zilinunuliwa na kukarabatiwa na raia wa Urusi wenye kipato cha chini. Mashahidi wanatumia kila fursa ya kukata rufaa kupinga matendo ya serikali, kutia ndani kupeleka malalamiko kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu na kwenye Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu.