Hamia kwenye habari

NOVEMBA 18, 2016
URUSI

SEHEMU YA 1 Nyongeza

Mahojiano ya Pekee—Wataalamu Waeleza: Urusi Yatumia Vibaya Sheria ya Kudhibiti Vikundi Vyenye Msimamo Mkali Ili Kuwafanya Mashahidi wa Yehova Waonekane Kuwa Wahalifu

Mahojiano ya Pekee—Wataalamu Waeleza: Urusi Yatumia Vibaya Sheria ya Kudhibiti Vikundi Vyenye Msimamo Mkali Ili Kuwafanya Mashahidi wa Yehova Waonekane Kuwa Wahalifu

Hii ni Sehemu ya 1 ya mfuatano wenye sehemu tatu.

Wenye mamlaka nchini Urusi wanataka kufunga shirika la kisheria la Mashahidi wa Yehova kwa madai ya kuwa na shughuli za kidini zenye msimamo mkali na hivyo kupiga marufuku Mashahidi katika nchi hiyo. Mashahidi wamekata rufani mashtaka hayo dhidi yao na pia onyo lililotolewa dhidi ya Kituo chao cha Usimamizi nchini Urusi.

Kuhusu kesi hiyo ya Mashahidi, na mtazamo wa Urusi kuelekea kupambana na kukabiliana “msimamo mkali” mahojiano ya pekee yalifanywa pamoja na wasomi maarufu wa mambo ya dini, siasa, na soshiolojia, na pia wataalamu wanaofahamu ule uliokuwa Muungano wa Sovieti na hali baada ya kuvunjika kwa Muungano wa Sovieti.

Je, mnafikiri kwamba kikundi cha kidini kisichofanya jeuri kama Mashahidi wa Yehova, kinapaswa kutangazwa kuwa chenye “msimamo mkali” na kupigwa marufuku nchi nzima?

  • Prof. William S. B. Bowring

    “Hapana. Kwa maoni yangu, ni jambo la kipumbavu na lisiloeleweka kuwarejelea Mashahidi wa Yehova kuwa ‘watu wenye msimamo mkali.’”—Profesa William S. B. Bowring, profesa wa sheria, mkurugenzi wa masomo ya Haki za Kibinadamu kwenye LLM/MA, Shule ya Sheria ya Birkbeck, Chuo Kikuu cha London; wakili wa Middle Temple na Gray’s Inn, Uingereza

  • Dakt. Ekaterina Elbakyan

    Ikitegemea mambo ambayo nimejionea mwenyewe nikichunguza maisha ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi, nina uhakika kwamba hili ni shirika la kidini lenye amani kabisa na ambalo limekuwepo nchini Urusi kwa muda mrefu (zaidi ya miaka 100). Waumini hao si wenye msimamo mkali hata kidogo. Hata hivyo , kwa sababu zisizoeleweka, mahakama imewatangaza waumini hao kuwa watu wenye msimamo mkali, sawa na wahalifu wa ugaidi walioshikwa, eti kwa sababu wanakutana pamoja na kufanya ibada ya kidini, kuzungumzia Biblia, na kuimba nyimbo za kumtukuza Mungu.”—Dakt. Ekaterina Elbakyan, profesa wa soshiolojia na usimamizi wa mawasiliano, Chuo cha Mahusiano ya Kazi na ya Jamii jijini Moscow; mshiriki wa shirika la Ulaya la Masomo ya Dini; mhariri mkuu wa makala ya Kirusi ya Westminster Dictionary of Theological Terms, Study of Religion, na Encyclopedia of Religions, Urusi

  • Dakt. Roman Lunkin

    “Kesi hizi dhidi ya Mashahidi zimefunua sifa mbili za msingi za sera mpya ya kidini wakati huu: kwanza, sera hiyo ni yenye kuonyesha chuki na inategemea kupinga uvutano wa nchi za Magharibi; pili, mashtaka hayo dhidi ya Mashahidi yanategemea mawazo na mitazamo yanayotokana na sera za Muungano wa Sovieti ambao haupo tena. Makosa hayo yote na njia hizi za kushughulika na “jamii ambazo si maarufu” ndiyo sababu kesi hizi zinafanywa dhidi ya Mashahidi wa Yehova.”—Dakt. Roman Lunkin, mkuu wa Kituo cha Dini na Jamii katika Taasisi ya Ulaya, (Center for Religion and Society at the Institute of Europe), Chuo cha Sayansi cha Urusi jijini Moscow; rais wa Muungano wa Wataalamu wa Dini na Sheria, Urusi

  • Dakt. Dmitry Uzlaner

    “Jambo linalotatiza zaidi kuhusu sera za kidini za Urusi ni kutungwa kwa mfumo unaokandamiza wa kupinga mambo ya kidini uliokusudiwa kuelekeza na kudhibiti utendaji wa waumini. Yaani, si kwamba tu wanafanyiza sheria mpya kuhusu msimamo mkali au suala la kuhubiri, bali pia wanatumia mamlaka yao vibaya katika cheo cha juu na cha chini. Mfumo huu hutumiwa dhidi ya vikundi vyenye amani na vinavyofuata sheria.”—Dakt. Dmitry Uzlaner, mtafiti katika Chuo cha Moscow cha Sayansi za Kijamii na Kiuchumi; mhariri mkuu wa State, Religion and Church, Urusi

  • Dakt. Liudmyla Fylypovych

    “Kwa kuwa Mashahidi wa Yehova wanatambua Mungu ana mamlaka ya juu kabisa, wenye mamlaka hawawapendi na—hivyo wanawapiga marufuku. Uamuzi kuhusu Mashahidi wa Yehova tayari umefanywa: Hawapaswi kuwepo nchini Urusi. Mahakama inataka tu kufanya uamuzi huo uonekane kuwa wa kisheria.”—Dakt. Liudmyla Fylypovych, profesa, mkuu, Idara ya Historia ya Dini na Masomo ya Mambo ya Kidini, Chuo cha Kitaifa cha Sayansi na Falsafa, makamu wa rais, Shirika la Ukrainia la Watafiti wa Dini (UARR), Ukrainia

  • Dakt. Ringo Ringvee

    “Kutumia mwelekeo na mbinu zilezile zinazotumiwa dhidi ya vikundi vinavyochochea jeuri na chuki ya kidini vikiwa na nia ya kufanya ugaidi kwa kikundi cha kidini chenye amani ambacho hakijawahi kufanya jeuri na kinachoshikamana na kanuni za kutojiunga na vita ni tendo lililopita kiasi na lisilozingatia haki. Kila serikali ulimwenguni ina changamoto nyingi na zilizo muhimu za kukabiliana nazo kuliko kukabiliana na Mashahidi wa Yehova, kikundi kisichofuatia mambo ya kisiasa na amabacho kinasubiri kwa amani Ufalme wa Mungu uje.”—Dakt. Ringo Ringvee, mshauri, Masuala ya Kidini, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Estonia; profesa wa dini ya ulinganisho, Taasisi ya Kitheolojia ya Kanisa la Kievanjeli la Lutheran, Estonia

  • Bw Andrew Wood

    “Urusi si ndiyo nchi pekee iliyo na sheria dhidi ya msimamo mkali. Mtajo huo hauko wazi na unaegemea upande mmoja. Mimi si wakili, lakini ningependa ikiwa sheria hizo zingeonyesha wazi uhusiano kati ya msimamo mkali na kile ambacho sheria ya Uingereza imerejelea kuwa uhalifu wa kuchochea watu wafanye jeuri. Sheria za Urusi ziko karibu kuwa kama sheria zinazowekwa dhidi ya maoni yaliyo tofauti na yale ya serikali inayotawala. Kutumia sheria hiyo dhidi ya Mashahidi wa Yehova ni sawa na kufanya hivyo. Sijawahi kusikia kwamba Mashahidi wa Yehova wamewachochea watu wafanye jeuri. Hilo ni kinyume cha jinsi serikali inavyodai.”—Sir Andrew Wood, mshiriki wa programu ya Urusi na mabara ya Ulaya na Asia, Chatham House, Taasisi ya Masuala ya Kimataifa ya Royal; aliyekuwa balozi wa Uingereza nchini Urusi (1995-2000), Uingereza

  • Dakt. James Christie

    “Mimi sijui lolote na kulingana na ninavyowafahamu Mashahidi fulani hususa, sioni jambo lolote ambalo linaweza kunifanya niamini kuwa dini hii inaonyesha msimamo mkali katika njia yoyote ile.”—Dakt. James Christie, profesa wa theolojia ya mazungumzo, mkurugenzi, Taasisi ya Ridd ya Sera za Dini na Ulimwengu, mwenyekiti, Masomo ya Programu ya Mambo ya Miungu, Kituo cha United cha Masomo ya Kitheolojia, Chuo Kikuu cha Winnipeg; mwenyekiti, Project Ploughshares, Conrad Grebel Chuo Kikuu cha Conrad Grebel, Chuo Kikuu cha Waterloo, Kanada

  • Dakt. George D. Chryssides

    “Sheria inayowaathiri Mashahidi wa Yehova ina kasoro kadhaa. Inanyimana sana uhuru wa kidini, na hivyo kukiuka hati ya Umoja wa Mataifa ya Azimio la Watu Wote la Haki za Kibinadamu, hasa Kifungu cha 18, ambacho kinaonyesha kwamba mtu ana haki ya kufuata dini anayotaka, iwe ni kwa matendo, faraghani, au pamoja na wengine. Maneno ‘msimamo mkali wa kidini’ hayako wazi. Hapo awali ilihusisha mashirika ambayo yalitekeleza matendo ya kigaidi na jeuri. Maneno hayo hayafai hata kidogo kutumiwa kuwarejelea Mashahidi wa Yehova, ambao wanapinga kwa uthabiti vita na jeuri ya aina yoyote. Ninaelewa kwamba maneno hayo yanatumiwa kwa kadiri fulani katika sheria ya Urusi kama ‘kuchochea mizozo inayotokana na ubaguzi wa rangi, wa kitabaka, au wa kidini ambayo tena hauhusiani na Mashahidi wa Yehova kwa njia yoyote ile. Wao ni shirika la kimataifa, lenye watu wa rangi tofauti ambalo limeazimia kuendelea kutia ndani watu wa rangi na lugha zote.”—Dakt. George D. Chryssides, aliyekuwa msimamizi wa masomo ya kidini, Chuo Kikuu cha Wolverhampton; mtafiti wa cheo cha juu katika masuala ya dini, Chuo Kikuu cha York St. John na Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza

  • Dakt. Silvio Ferrari

    “Kwa maoni yangu, sheria ya Urusi ya kukabiliana na msimamo mkali wa kidini na jinsi sheria hiyo ilivyotekelezwa kuelekea Mashahidi wa Yehova na vikundi vingine vya kidini ni mfano mbaya zaidi wa hatua ya kukazia fikira dini na uhuru wa kidini kupita kiasi, jambo ambalo kwa kiwango kidogo linatekelezwa na nchi nyingine za Ulaya. Sheria hiyo inatokeza mambo haya mawili yasiyofaa—inajiingiza sana katika mafundisho na utendaji wa jamii za kidini na hivyo kusababisha ubaguzi kati ya jamii za kidini.”—Dakt. Silvio Ferrari, rais wa Shirika la Kimataifa la Masomo ya Sheria na Dini; mhariri mkuu Oxford Journal of Law and Religion, mwanzilishi wa Shirika la Ulaya la Dini na Serikali, profesa wa sheria na dini na orodha ya kanuni za kanisa, Chuo Kikuu cha Milan, Italia

  • Prof. Elizabeth Clark

    “Kutumia sheria dhidi ya msimamo mkali ili kupiga marufuku vikundi visivyofanya jeuri kama Mashahidi wa Yehova ni matumizi mabaya ya sheria hiyo isiyo wazi. Ikitegemea jinsi ambavyo waendesha mashtaka na mahakama wamefafanua ‘msimamo mkali’ dini yoyote ile inaweza kufunguliwa mashtaka. Isipokuwa dini iwe inataka kusababisha madhara, jambo ambalo hakuna aliyedai kwamba Mashahidi wa Yehova wanafanya, kuwapiga marufuku kunakiuka Katiba ya Urusi na sheria ya kimataifa.”—Profesa Elizabeth A. Clark, msimamizi-mshirika, mshauri wa Ulaya Kati na Ulaya Mashariki, Kituo cha Kimataifa cha Sheria na Masomo ya Kidini, Chuo Kikuu cha Brigham Young, Marekani

  • Dakt. Zoe Knox

    “Ikiwa maneno ‘msimamo mkali’ yanafafanuliwa kama isiyo maarufu au isiyo ya kawaida, basi wenye mamlaka wanayatumia isivyofaa ili kutimiza malengo yao. Kwa hiyo, wenye mamlaka wanawataja Mashahidi wa Yehova kuwa watu wenye msimamo mkali kwa sababu imani yao si maarufu ila si kwa sababu wanasababisha tisho lolote. Kwa kiwango kikubwa Mashahidi wa Yehova wanaendelea kutendewa jinsi walivyokuwa wakitendewa wakati wa ule uliokuwa Muungano wa Sovieti, iwe ni kupitia vyombo vya habari au mitazamo ya kisiasa.”—Dakt. Zoe Knox, profesa mshirika wa historia ya kisasa ya Urusi, Chuo Kikuu cha Leicester, Uingereza

  • Dakt. Eric D. Patterson

    “Tatizo la sheria hii dhidi ya msimamo mkali ni kwamba imebuniwa kwa lengo la kukandamiza dini ndogondogo, wala si kukabili magaidi.”—Dakt. Eric D. Patterson, profesa wa cheo cha juu, Shule ya Serikali ya Robertson, Chuo Kikuu cha Regent, Marekani

  • Prof. Frank Ravitch

    “Isipokuwa mtu afafanue neno ‘msimamo mkali’ kwa njia isiyo ya kawaida, haipatani na akili kuwaita Mashahidi wa Yehova watu wenye msimamo mkali. Jambo hilo halipatani kabisa na mambo yote ninayoelewa kuhusu theolojia na mafundisho ya Mashahidi.”—Profesa Frank Ravitch, profesa wa sheria, Walter H. Stowers Kitengo cha Sheria na Dini, Chuo Kikuu cha Michigan State, Marekani

  • Dakt. Alar Kilp

    “Misukosuko na mizozo ya kisiasa imeingizwa hadi katika masuala ya dini. Sababu za kuenea kwa vita vikali zaidi dhidi ya msimamo mkali wa kidini nchini Urusi ni za kisiasa, wala hazihusiani na mambo ya kidini. Kwa sasa, Mashahidi wa Yehova nchini Urusi wananyanyaswa ingawa hawajafanya kosa lolote.”—Dakt. Alar Kilp, mhadhiri wa siasa za ulinganisho, Taasisi ya Serikali na Siasa, Chuo Kikuu cha Tartu; msimamizi mshiriki wa “Dini na Siasa nchini Urusi na Ulaya Mashariki,” Kituo cha Masomo ya EU-Urusi, Estonia

  • Dakt. Emily B. Baran

    “Upinzani wa serikali kuelekea Mashahidi wa Yehova una historia ndefu nchini Urusi, tangu wakati wa utawala wa Sovieti. Mashahidi wa Yehova walioishi chini ya utawala wa Sovieti walikataa kupiga kura, kujiunga na jeshi, kununua hisa za kutegemeza serikali, kujiunga na Chama cha Kikomunisti, au kuendeleza sera za serikali. Hata waliposhinikizwa vikali kukana imani yao, waliendelea kukutana katika nyumba za watu binafsi na kuwahubiria wengine kuhusu imani yao. Kwa kuwa walikataa kupendelea utawala wa Sovieti, waliteswa vikali kwa miaka mingi, na hata wengi wao walipelekwa uhamishoni katika maeneo ya mbali ya Siberia. Serikali ya Sovieti iliwakamata na kuwatia Mashahidi wengi gerezani kwa makumi ya miaka, hata iliwatenganisha watoto na familia zao. Zaidi ya hilo, ilichapisha propaganda zilizotiwa chumvi ambazo zilionyesha kwamba Mashahidi ni wahalifu, wasaliti, na waliopotoka. Haishangazi kwamba, ingawa Muungano wa Sovieti ulivunjika miaka zaidi ya ishirini iliyopita, bado matokeo ya uadui na mateso yaliyokuwa katika utawala huo yanaendelezwa leo.”—Dakt. Emily B. Baran, profesa msaidizi wa historia ya Urusi na Ulaya Mashariki, Chuo Kikuu cha Middle Tennessee State, Marekani

  • Dakt. Giampiero Leo

    “Kwa maoni yangu, hatua ambazo Urusi imechukua zimepita kiasi, hasa wakati huu ambao kumekuwa na matukio yenye kushangaza, inapaswa kuwa wazi ‘msimamo mkali’ ni nini na ni nani wenye ‘msimamo mkali’ hasa. Mashahidi wa Yehova ni kikundi kinacholeta amani; fikira na utu wao si wa jeuri hata kidogo.”—Dakt. Giampiero Leo, makamu wa rais, Kamati ya Haki za Kibinadamu, Eneo la Piedmont, Italia

  • Bi. Melissa Hooper

    “Kwa kweli, sheria hiyo imepita mipaka. Sheria hiyo imeandikwa kwa njia ambayo inaweza kutumiwa na watekelezaji sheria ili kuwakamata au kuwatisha wale walio na maoni ya kidini ambayo hayapendwi na wengi au wale ambao serikali haiwapendi. Mifano ya jinsi sheria hiyo ilivyotekelezwa ni kukamatwa kwa Mashahidi wa Yehova, watu katika vikundi vingine vidogo, na hata wale wanaoamini hakuna Mungu. Sheria hiyo imekuwa ikitumiwa kulinda maoni ya kanisa Othodoksi yanayoungwa mkono na serikali, na kuadhibu wenye maoni yanayoonekana kuwa tofauti au tisho kwa mafundisho ya kanisa la Othodoksi.”—Bi. Melissa Hooper, wakili, mkurugenzi, shirika la kimataifa la sheria (International Law Scholarship Project/Pillar Project), Haki za Kibinadamu Kwanza; aliyekuwa mkurugenzi wa mkoa wa shirika linaloitwa American Bar Association Rule of Law Initiative in Moscow, Marekani

  • Dakt. Basilius J. Groen

    “Ingawa Mashahidi wa Yehova ni dini ya Kikristo na imani yao inategemea Biblia, Warusi wengi huwaona kuwa dini ‘isiyo ya Kikristo,’ ‘wasio wazalendo,’ (kwa sababu Mashahidi hukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi), kuwa ‘tisho’ na mambo mengine kama hayo. Ninafikiri kuwaita dini ‘yenye msimamo mkali’ si sahihi.—Dakt. Basilius J. Groen, UNESCO (Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni) Mwenyekiti wa Mazungumzo ya Kijamii na Kidini ya Kusini Mashariki mwa Ulaya, Chuo Kikuu cha Karl-Franzens; profesa wa theolojia ya liturujia na utakatifu, mkuu wa Taasisi ya Liturujia, Sanaa na Nyimbo za Kikristo, Chuo Kikuu cha Graz, Austria

  • Bw. Eric Rassbach

    “Mashahidi wa Yehova wanapaswa kuishi kulingana na imani yao nchini Urusi kama wanavyofanya katika nchi nyingine. Haki ya msingi ya wanadamu ya kuamini katika dini na kuionyesha hadharani imelindwa na mikataba ya haki za kibinadamu na sheria za kitaifa, kutia ndani Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na za Kisiasa, Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu, na Katiba ya Urusi. Mashahidi wa Yehova wanapaswa kupewa haki hiyo kikamili.”—Bw. Eric Rassbach, naibu wakili mkuu, Hazina ya Becket ya Uhuru wa Kidini, Marekani

  • Dakt. Shawn F. Peters

    “Ninashangaa na kuhuzunika sana kuona Mashahidi wa Yehova wakitajwa kuwa wenye ‘msimamo mkali,’ jambo lililopangwa ili kupotosha malengo manyoofu ya kidini ya washiriki wa dini hiyo. Azimio thabiti la Mashahidi la kufuata na kueneza dini yao halionyeshi kuwa wao ni tisho kwa serikali ya Urusi, na kuwapiga marufuku, jambo ambalo halichangii kwa vyovyote usalama na utaratibu katika jamii nchini Urusi, kutakuwa kukandamiza kabisa uhuru wa kidini na haki za kibinadamu.”—Dakt. Shawn F. Peters, mhadhiri mkuu wa dini na sheria, Chuo Kikuu cha Wisconsin, Marekani

  • Prof. Robert C. Blitt

    “Jibu fupi hapa ni hapana. Kwanza, kufikia mkataa huo kunatokana na ufafanuzi uliopita kiasi wa maneno msimamo mkali ambao hauonyeshi mambo kama vile jeuri au njia nyingine za kuonyesha chuki kama mambo yanayofanyiza kosa hilo, na badala yake unatia ndani maelezo ya aina zote. Pili, kupiga marufuku mashirika kungeonyesha kwamba serikali imeshindwa kugundua hatua nyingine ambazo zingeweza kutumiwa kwa mafanikio kukomesha matendo ya watu wenye msimamo mkali. Kwa sababu ya hatua za kiadhabu ambazo serikali imechukua kuelekea Mashahidi, tume ya kisheria iliyo huru inahitaji kubuniwa ili ichunguze ikiwa hatua ya serikali dhidi ya Mashahidi inalingana na mashtaka yao na ikiwa inastahili ili kuyashughulikia. Ingawa vikundi vya kidini kama Mashahidi wa Yehova hawastahili kuitwa watu wenye msimamo mkali au kupigwa marufuku, sheria yenye makosa ambayo nimeeleza inaweza kuruhusu jambo hilo lifanyike.”—Profesa Robert C. Blitt, profesa wa sheria, Chuo Kikuu cha Tennessee, aliyekuwa mtaalamu wa sheria ya kimataifa wa Tume ya Marekani Inayoshughulikia Uhuru wa Kidini wa Kimataifa (USCIRF), Marekani

  • “La hasha. Ninafikiri ni kosa, na hilo halipatani na sera ya kutetea uhuru wa dini.”—Profesa Pasquale Ferrara, profesa msaidizi, Mwenyekiti wa diplomasia, Idara ya Sayansi ya Siasa, Libera Università internazionale degli Studi Sociali Guido Carli (LUISS); Mwenyekiti wa Uhusiano na Utangamano wa Kimataifa, Taasisi ya Chuo Kikuu cha “Sophia,” Figline e Incisa Valdarno, Italia

  • Dakt. Javier Martínez-Torrón

    “Sikubaliani na baadhi ya mafundisho yao, lakini ninafikiri si sahihi na imepita kiasi kuwaita Mashahidi wa Yehova ‘watu wenye msimamo mkali’ kulingana na ufafanuzi wa wenye mamlaka nchini Urusi.”—Dakt. Javier Martínez-Torrón, profesa wa sheria, mkurugenzi, Idara ya Sheria na Dini, Chuo Kikuu cha Complutense Kitengo cha Sheria, Hispania

  • Dakt. Jim Beckford

    “Watu fulani katika Kanisa Othodoksi la Urusi wanapanga njama na wenye mamlaka ili kuendeleza masilahi yao wenyewe na kukandamiza jambo lolote wanaloona kuwa ushindani.”—Dakt. Jim Beckford, mshiriki wa Chuo cha Uingereza; profesa mstaafu anayeheshimika wa sosholojia, Chuo Kikuu cha Warwick; aliyekuwa rais wa Shirika la Masomo ya Kisayansi ya Dini (USA), Uingereza

  • Dakt. Gerhard Besier

    “Mrusi halisi, iwapo ni Mkristo, ni mshiriki wa Kanisa Othodoksi la Urusi. Warusi walio katika mashirika ya kidini ‘yasiyofaa’ wanatengwa na kukataliwa katika jamii. Kwa hiyo, haki za kiraia za Mashahidi wa Yehova zinakiukwa kabisa.”—Dakt. Gerhard Besier, profesa mstaafu anayeheshimika wa masomo ya Ulaya, Technische Universität Dresden; mhadhiri, Chuo Kikuu cha Stanford; mkurugenzi, Taasisi ya Sigmund Neumann ya Utafiti wa Uhuru na Demokrasia, Ujerumani

  • Dakt. Mark R. Elliott

    “Ninahisi kwamba Mashahidi wa Yehova wanatendewa kikatili sana si kwa sababu ya mafundisho yao na maandiko bali kwa sababu ya mafanikio ya kazi yao ya kuhubiri. Inashangaza kwamba hesabu yao imeongezeka kwa sehemu kwa sababu ‘wananawiri wanaponyanyaswa.’ Isitoshe, uhamisho uliofanywa wakati wa utawala wa Muungano wa Sovieti, ulienda kinyume cha matarajio. Katika mwaka wa 1951-52 Mashahidi 7,000 hivi walipelekwa uhamishoni huko Asia ya Kati na Siberia, jambo hilo lilifanya waeneze ujumbe wao zaidi. Kwa hiyo, kuenea kwao kotekote nchini humo kumechangiwa na wenye mamlaka bila kupenda na pia kazi ya Mashahidi ya kuhubiri. Kama walivyoendelea na utendaji wao waliponyanyaswa na Wasovieti, inaweza kutarajiwa kwamba Mashahidi wa Yehova watafaulu licha ya marufuku ya sasa.”—Dakt. Mark R. Elliott, mhariri mkuu, East-West Church and Ministry Report, Chuo Kikuu cha Asbury, Kentucky, Marekani

  • Dakt. Régis Dericquebourg

    “Kulingana na ujuzi nilio nao, sosholojia haiwezi kutumiwa kufafanua msimamo mkali. Msimamo mkali ni wazo la kisiasa linalotumiwa na nchi za kidemokrasia kurejelea maoni ya kisiasa yanayotofautiana na yao. Lakini ni vigumu kulitumia kufafanua dini. Kuna vikundi vya kidini vilivyo na desturi zinazowaathiri kuliko vikundi vingine (kama vile, desturi zinazowatia moyo wafuasi wao wasali zaidi kuliko wengine au wafuate matakwa fulani kuhusu chakula au kuwa na mfungo) au ambazo zinataka wafuasi wake wawe na viwango vya maadili vinavyowabana kuliko wengine. Mashahidi wa Yehova wana desturi kadhaa; wanakutana mara nyingi kuliko washiriki wa dini kuu, lakini Wayahudi waliojitoa sana pia wanakutana mara nyingi. Mashahidi wanahisi ni lazima waeneze mafundisho yao kwa kuhubiri barabarani au nyumba kwa nyumba. Wana viwango vya juu sana wakilinganishwa na mshiriki wa kawaida wa dini kubwa, na wanahisi wana wajibu wa kuwa wanyoofu wanapofanya kazi, katika uhusiano na majirani, wanakuwa washikamanifu katika ndoa zao, wanawatendea wengine kwa fadhili, na hawawaumizi wengine. Wanakata kujiunga na jeshi ili wasimwue mwanadamu mwingine vitani. Mambo yote hayo yanatofautiana na dini kubwa, lakini hawahatarishi jamii kwa njia yoyote kupitia mambo hayo. Mashahidi wa Yehova hawataki kunyakua mamlaka ili waanzishe serikali ya kidini (kwa maoni yao, mapenzi ya Mungu ndiyo yataleta serikali inayotawaliwa na Mungu). Hawataki kuanzisha jamii inayoongozwa na kanuni zao, kama Waislamu wenye imani kali. Mashahidi ni Wanabiblia tu, kwa kuwa wanaishi kulingana na jinsi wanavyoielewa Biblia. Huo ni uamuzi wao. Jambo ambalo jamii ingependa kujua tu ni ikiwa wao ni hatari au la. Ninajibu hivi, ‘La.’ Mashahidi hawaungi mkono upande wowote, na hawajihusishi na siasa za nchi. Jambo muhimu hata zaidi, hawashiriki katika mashambulizi yoyote.”—Dakt. Régis Dericquebourg, sociologist, associate professor of new religious movements, Antwerp FVG, Ubelgiji

  • Dakt. Thomas Bremer

    “Hapana, sidhani. Mimi si Shahidi wa Yehova na siwaungi mkono, hata sikubaliani na baadhi ya mafundisho yao, lakini sidhani wao wana msimamo mkali (bila shaka, inategemea ufafanuzi wa mtu wa maneno ‘msimamo mkali’), na hata zaidi nafikiri wanapaswa, kama watu wengine wote, kuwa na haki ya kuzungumzia mambo wanayoamini.”—Dakt. Thomas Bremer, former research fellow, Jordan Center for the Advanced Study of Urusi, New York University; professor of ecumenical theology, eastern churches studies and peace studies, Chuo Kikuu cha Münster, Ujerumani

  • Dakt. Marco Ventura

    “Kutumia sheria ya Kirusi dhidi ya Mashahidi wa Yehova kumefanya wapoteze uhuru wao wa msingi bila haki, na hivyo kupingana na haki za kibinadamu za kimataifa zinazolinda uhuru wa mtu au kikundi cha watu kushiriki ibada au kuwa na imani fulani, na zinazokataza ubaguzi kwa msingi wa dini. Ufafanuzi huo unategemea mbinu inayotumiwa katika haki za kisheria za kimataifa, kulingana na mbinu hiyo kuingiliwa kwa haki ya kidini au imani kunapaswa kuchunguzwa kulingana na: 1) ikiwa kweli uhuru wa kutangaza au kuishi kulingana na dini au imani uliingiliwa, na 2) ikiwa kuingiliwa kwa haki hiyo kulikuwa kwa kiwango kilekile na kuthibitishwa na sheria.”—Dakt. Marco Ventura, professor of law and religion, University of Siena; director, Center for Religious Studies at the Bruno Kessler Foundation; associate researcher, Centre for Droit, Religion, Entreprise et Société (DRES), Chuo Kikuu cha Strasbourg (Ufaransa), Italia

  • Dakt. Mark Juergensmeyer

    “Kuingilia uhuru wa ibada eti kwa sababu ya msimamo mkali ni mbinu inayosikitisha. Inashtua kwamba mbinu hizo za kudhibiti mawazo bado zinatumiwa katika karne ya 21. Sisi sote tunastahili kutendewa kwa njia bora zaidi.”—Dakt. Mark Juergensmeyer, director, Orfalea Center for Global and International Studies, professor of sociology, affiliate professor of religious studies, Chuo Kikuu cha California, Santa Barbara, Marekani

Ungefafanuaje njia ya Urusi ya kukabiliana na “msimamo mkali”?

  • “Katika kupambana na msimamo mkali, nchi ya Urusi yenyewe inatumia mbinu zenye msimamo mkali. Imetenda kwa njia mbaya, ya kulazimisha, na ya kibaguzi ili kuweka marufuku hiyo. Matendo ya ubaguzi ya wenye mamlaka hayawezi kutetewa au kueleweka. Mtu anaweza tu kuogopa maamuzi hayo.”—Dakt. Fylypovych, Ukrainia

  • “Hakuna mtu anayepigana dhidi ya ugaidi wa aina yoyote na anayethamini umuhimu wa kuandaa ulinzi kuliko mimi. Hata hivyo, kutumia sheria ya msimamo mkali dhidi ya Mashahidi wa Yehova, yaani, dhidi ya jamii ya kidini ambayo imekataa kushiriki jeuri, ni kufanya suala la usalama kuwa haki kuu inayoshinda haki nyingine, kutia ndani uhuru wa ibada. Hiyo ndiyo sababu ninafikiri kwamba ni jukumu la kila mtu, kutia ndani wasomi, kushutumu waziwazi sheria hiyo na jinsi inavyotumiwa bila aibu kutishia uhuru na usawa wa kidini.”—Dakt. Ferrari, Italia

  • Dakt. Derek H. Davis

    “Matendo ya msimamo mkali yanayopaswa kupingwa ni yale yanayohatarisha maisha ya watu. Kupingana na kitu kingine chochote ni aina fulani ya msimamo mkali; hivyo jinsi nchi ya Urusi inavyowanyanyasa kwa bidii kikundi chenye amani kama Mashahidi wa Yehova ni kuwa na ‘msimamo mkali.’”—Dakt. Derek H. Davis, mwanasheria, msimamizi wa zamani wa Taasisi ya J.M. Dawson ya Masomo ya Kanisa na Dini, Chuo Kikuu cha Baylor University, Marekani

  • “Kama nilivyotaja awali, maneno kuwa na ‘msimamo mkali’ hayaeleweki waziwazi na yanaweza kutumiwa kwa njia mbalimbali. Ningefafanua hatua ambayo nchi ya Urusi imechukua kuwa imepita kiasi na haifai, na wenye mamlaka wamehukumiwa na ECtHR [Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu] kuwa wamekiuka uhuru wa kidini. Vikundi vyenye msimamo mkali kama ISIS bila shaka ni hatari sana na hatua zinapaswa kuchukuliwa kudhibiti utendaji wao. Hata hivyo, Mashahidi wa Yehova hawawezi kulinganishwa na vikundi vinavyotisha kama hivyo, na haifai kutumia mbinu hiyo ya kudhibiti mashirika ya kigaidi ili kuzuia kazi yao.”—Dakt. Chryssides, Uingereza

  • “Marekebisho yaliyofanywa katika sheria za Urusi kuhusu msimamo mkali zinaashiria mwisho wa uhuru wa mtu kuchagua ibada nchini Urusi, na kama mfano wa hivi karibuni wa Mashahidi wa Yehova unavyoonyesha, marekebisho hayo yanalenga kukomesha utendaji wa vikundi vidogo vya kidini. Ukiangalia historia, vizuizi kuhusu kazi ya umishonari wa kidini vinafanana na vile vilivyowekwa katika utawala wa Sovieti.”—Dakt. Ringvee, Estonia

  • Dakt. William Schmidt

    “Mwelekeo wa kuwa na msimamo mkali unaweza kuonekana, kama tujuavyo, si kwa vikundi vya watu tu, bali pia kwa mtu mmoja-mmoja; msimamo mkali ni aina fulani ya utendaji wa kisiasa, si utendaji wa kidini. Katika nchi ya Urusi, kuna vizuizi vya kisheria dhidi ya utendaji kama huo ukifanywa na mashirika ya kidini. Na ikiwa kuna visa fulani (vya utendaji wenye msimamo mkali), basi, mkosaji anapaswa kuadhibiwa—hiyo ni njia ya kawaida ya kushughulikia sheria. Je, kuna hatari ya kufanya utendaji wa kidini kuwa uhalifu kwa msingi wa msimamo mkali? Ndiyo, hasa kwa sababu ya ufafanuzi na matumizi yasiyofaa ya sheria, na vilevile matumizi ya watu wasio wataalamu katika uchunguzi wao.”—Dakt. William Schmidt, mhariri mkuu, Eurasia: the spiritual traditions of the peoples; profesa, National and Federative Relations, The Urusin Presidential Academy of National Economy and Public Administration (RANEPA), Urusi

  • “Kutumia sheria dhidi ya msimamo mkali—ili kulinda watu wasioweza kujitetea—inakubalika inapotumiwa kwa usawaziko. Kwa upande mwingine, kutumia sheria hizo kuingilia uhuru wa dini ndogo zisizo na jeuri, kama Mashahidi wa Yehova, si jambo linalokubalika hata kidogo.”—Dakt. Leo, Italia

  • “Kuna mabadiliko makubwa katika sera za serikali ya Urusi tangu angalau mwaka wa 2012. Sheria zinakuwa kali zaidi, zinadhibiti haki za kisiasa na hata haki za kiraia. Sheria ya sasa nchini Urusi dhidi ya msimamo mkali inaweza kumhusisha mtu yeyote; si lazima upange shambulizi la kigaidi ili ushutumiwe kwa kuwa na msimamo mkali, kuchambua mkuu fulani kwenye mtandao wa kijamii au kushiriki mkutano wa kisiasa kunaweza kufanya ushutumiwe kuwa na msimamo mkali. Sheria kuhusu dini ni mfano mmoja tu wa aina hiyo ya sheria.”—Dakt. Uzlaner, Urusi

  • “Matendo ya Urusi (pamoja na Azerbaijan) ya kudhibiti dini yamepita kiasi, kwa sababu si nchi nyingi barani Ulaya zilizo na orodha ya vitabu vya kidini vilivyopigwa marufuku, au kushughulika machapisho yenye msimamo mkali kisheria au kisiasa.”—Dakt. Kilp, Estonia

  • “Pambano lisilofaa dhidi ya msimamo mkali ikitegemea dini lilianza hatua kwa hatua baada ya Sheria ya Kupambana na Utendaji Wenye Msimamo Mkali iliyopitishwa mwaka wa 2002. Sera dhidi ya msimamo mkali imekuwa silaha ya kupigana na dini ‘ndogo.’ Kwa kuwa mtajo ‘msimamo mkali’ ni mpana unawapa mahakimu nafasi ya kufanya maamuzi ya kutangaza machapisho ya kidini kuwa na msimamo mkali bila sababu zinazopatana na akili. Tangu miaka ya katikati ya 2000, Sheria ya Kupambana na Msimamo Mkali imetumiwa kwa njia isiyofaa kwa watu ambao si Waothodoksi au Waislamu nchini Urusi.”—Dakt. Lunkin, Urusi

  • “Nchi ya Urusi inataka kuzuia kuenea kwa vikundi vya kidini au mawazo tofauti na dini rasmi nne. Vikundi kama Mashahidi wa Yehova na waevangeli au Waprotestanti wanaohubiri wananyanyaswa.”—Prof. Bowring, Uingereza

  • “Jinsi Urusi inavyopigana na vikundi vyenye washiriki wachache kama Mashahidi wa Yehova, ni kuonyesha ubaguzi. Unapatana na zoea la kuonyesha vikundi vidogo chuki ya jamii, kisiasa na ya kidini, vikundi hivyo vinalaumiwa kwa matatizo yoyote yanayotokea. Nchi ya Ufaransa pia inaongoza katika ‘kuyawinda madhehebu.’ Ufaransa ilitaka kuwakandamiza Mashahidi wa Yehova kwa kuwatoza kodi lakini Mashahidi walipeleka kesi hiyo kwenye ECtHR [Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu] huko Strasbourg na mwishowe wakashinda kesi. Mahakama ya ECtHR ilitoa hukumu kwamba Ufaransa walipe ofisi ya tawi ya Mashahidi pamoja na riba kwa sababu serikali ilikuwa imewabagua kwa kutowatambua kisheria, na hivyo kutotoza kodi michango inayotolewa na washiriki wake.”—Dakt. Dericquebourg, Ubelgiji

  • “Urusi inapaswa kupambana dhidi ya msimamo mkali kikweli, ambao unawasukuma watu wawe wajeuri, lakini vikundi vingi vya kidini vinatendewa ukatili kwa sababu ya sheria hizo. Ukatili unaonekana kwa sababu huwezi kulinganisha adhabu na kosa. Pia, ni ukatili unapofikiria zinalenga nini au nani. Mfano mmoja ni faini ya dola 15,000 za Marekani ambayo inaweza kuwa na madhara makubwa kwa kikundi kidogo cha kidini au kisichopata faida. Sheria moja inasema kwamba lazima uwe umesajiliwa nchini kwa miaka 15 kabla ya kumkaribisha nchini mtu kama vile kiongozi wa kidini au mmishonari nchini Urusi.”—Dakt. Patterson, Marekani

  • “Changamoto za kupambana na uhalifu, kutia ndani kupambana na ugaidi na msimamo mkali kwa kutumia matendo yasiyo ya kawaida au ya udhalilishaji zinaonekana kila siku. Hata hivyo, kupambana na uhalifu ni jambo moja, nalo ni tofauti kabisa na kutumia Sheria ya Uhalifu kubagua haki za watu za uhuru wa dhamiri, kutia ndani uhuru wa ibada. Wataalamu wengi nchini Urusi, wasomi na wanasheria, wanaona matumizi ya mtajo ‘msimamo mkali’ dhidi ya vikundi vyenye washiriki wachache kuwa kinyume cha sheria. Hata hivyo, wakati ambapo, kwa sababu mbalimbali, kanuni za sheria zinaathiriwa na ufisadi, basi, kama tujuavyo, haki, kutia ndani haki na uhuru wa kibinadamu, inapuuzwa.”—Dakt. Elbakyan, Urusi

  • Dakt. Hocine Sadok

    “Jambo linaloleta ubishi mkubwa zaidi katika sheria ya Urusi dhidi ya msimamo mkali ni dhana ya msimamo mkali wenyewe. Si dhana ya kisheria bali ya kisiasa. Kwa mfano, kwa maoni ya ECHR [Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu], Serikali zinaweza kuzuia uhuru kulingana na Mkataba huo, kama vile uhuru wa ibada au uhuru wa usemi wakati ambapo, ni lazima kufanya hivyo ili kulinda ‘usalama wa taifa, usalama wa umma, hali nzuri ya nchi, kuhakikisha sheria inafuatwa na kuzuia uhalifu, kulinda afya au maadili, au kulinda haki na uhuru wa wengine, kudumisha utaratibu,’ na kadhalika. Hivyo, serikali zimepewa mamlaka na sheria za kimataifa kuzuia uhuru ikiwa kuna hatari halali. Hivyo, si lazima kutunga sheria hususa dhidi ya msimamo mkali ili kufikia malengo yanayoonwa kuwa ya kisheria kulingana na ECHR. Jambo linalotatiza hata zaidi ni kwamba sheria ya Urusi haijafafanuliwa kikamili. Inamaanisha nini kuwa na ‘msimamo mkali’ chini ya sheria ya Kirusi? Tena, hiyo ni dhana ya kisiasa, ambayo iliwaruhusu wenye mamlaka wazuie uhuru wa wale wasiowataka. Kwa maoni hayo, ni wazi kwamba sheria ya Kirusi inapingana na mtazamo na sheria ya ECHR.”—Dakt. Hocine Sadok, mhadhiri wa sheria, msimamizi, Idara ya Masuala ya Kijamii na Kisheria, Université de Haute Alsace, Ufaransa

  • “Kazi ya kupambana na msimamo mkali inahusisha kusawazisha masilahi ya serikali na uhuru wa mtu mmoja-mmoja na si kuzuia uhuru wa watu. Katika kusawazisha huko, jitihada za Urusi za kupambana na msimamo mkali hazijafaulu. Isitoshe, njia ya serikali ya kufafanua msimamo mkali na kuwakamata wahusika kunaendeleza masilahi yao tu. Ingawa sheria hiyo inaweza kuwalinda raia wa Urusi dhidi ya hatari fulani halisi, pia inaipa serikali njia rahisi ya kuzuia au kunyamazisha watu na vikundi ambavyo kwa sababu moja au nyingine hawavitakiwi au vinavyoonekana kuwa hatari kwa viwango vya dini zinazokubalika. Sababu moja inayofanya Urusi idumishe na kupanua sheria hiyo ni kwa sababu misingi ya kidemokrasia haifanyi kazi vizuri pamoja na mapungufu mengine—kutia ndani mataifa na mashirika ya kimataifa—kutambua na kushughulikia tatizo hilo.”—Prof. Blitt, Marekani

  • “Inasikitisha kwamba Urusi inaelekea kufanya kosa lilelile ambalo Marekani ilifanya dhidi ya Mashahidi katika miaka ya 1940. Katika kipindi hicho Mashahidi wa Yehova walionekana kimakosa na Wamarekani kuwa ‘wenye msimamo mkali’ kwa sababu dhamiri zao za kidini hazikuwaruhusu washiriki sherehe ya Kiapo cha Uaminifu. Mwanzoni maofisa wa serikali—kutia ndani Mahakama Kuu ya Marekani—iliwaadhibu Mashahidi wa Yehova kwa mwenendo wao wa kutoshiriki. Hilo lilifanya Mashahidi wa Yehova watendewe kikatili, lakini baadaye walifikiria upya suala la dhamiri. Mwishowe, mahakama za Marekani na Wamarekani wengi, walikuja kugundua kwamba unamna-namna wa kidini, ni jambo zuri kwa jamii. Unamna-namna huo unatia ndani Mashahidi wa Yehova.”—Bw. Rassbach, Marekani

  • “Mfumo wa Urusi wa kisheria unapenda kutumia maneno yenye maana pana kama vile ‘msimamo mkali’ na ‘utendaji wenye msimamo mkali,’ ‘kusambaza imani,’ na ‘utendaji wa kimishonari,’ na madai ya ‘ukweli’ au ‘ubora’ wa dini au mfumo wa mtu wa ibada. Kwa kuwa hati haziandai ufafanuzi wa aina mbili, mpana na usio mpana, na sheria kuhusu kuandaa na kuchunguza uthibitisho zina uwanja mkubwa—hivi kwamba msimamo mkali katika muktadha wa kidini hauhusishi vitisho au kutenda kwa jeuri—maofisa wa usalama, wasimamizi, mahakimu na wataalamu wanaruhusiwa kutoa hukumu. Inasikitisha kwamba wenye mamlaka wamepuuza ombi la Kamati ya Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa (Uchunguzi wa Mwisho uliofanywa Aprili 28, 2015) la kutoa ‘ufafanuzi wa wazi wa “msimamo mkali,” kuhakikisha ufafanuzi unahusisha jeuri au chuki na kusitawisha viwango vilivyo wazi’ ‘jinsi vitu vinavyoweza kuonwa kuwa msimamo hatari’ na kuchukua ‘hatua zote za kuzuia matumizi yasiyofaa ya sheria na kuchunguza upya Orodha ya Serikali ya Vitu Vinavyoonyesha Msimamo Mkali.’”—Dakt. Ventura, Italia

  • Bi. Catherine Cosman

    “Sheria ya Urusi dhidi ya msimamo ilipitishwa mara ya kwanza mwaka wa 2002; kufikia mwaka wa 2007, ilipanuliwa kufikia utendaji usio wa jeuri au kuendeleza maoni, kutia ndani dini. Maofisa Warusi wakiamua kuwaadhibu watu bila sababu, wataathiri watu wenye amani wanaotaka tu kufuatilia dini au mawazo yasiyopendwa na Serikali. Kwa mfano, Waislamu wanaoamua kuwa na imani nje ya zilizokubaliwa, mara nyingi wanahukumiwa na mahakama za Kirusi kwa kuvunja sheria pana ya Urusi kuhusu msimamo mkali. Ikiwa maofisa hawatakuwa na ubaguzi na mahakama pia ikirekebisha sheria kuhusu dini na msimamo mkali itasaidia Warusi, ambao wanatoka jamii na dini mbalimbali. Urusi inapaswa kuacha kutumia nguvu kuingilia uhuru wa watu kuwa tofauti na kuwalazimisha wawe na msimamo mmoja.”—Bi. Catherine Cosman, senior policy analyst (Europe and the countries of the former Soviet Union), Tume ya Marekani Inayoshughulikia Uhuru wa Kidini wa Kimataifa (USCIRF), Marekani

  • “Sera za serikali kuhusu msimamo mkali wa kidini zinatokana na utamaduni unaofuatiliwa na Kanisa Othodoksi la Urusi.”—Dakt. Besier, Ujerumani

  • “Ingawa Urusi imekabili jeuri iliyotokana na msimamo mkali wa kidini, inafuatilia sheria dhidi ya msimamo mkali kudhibiti vikundi vya kidini visivyopendwa na wengi na si kutafuta vikundi vinavyohusianishwa na jeuri.”—Prof. Clark, Marekani

  • “Mfumo wa kisheria wa Urusi umepungukiwa katika njia mbili muhimu. Katiba ya Urusi yenye habari nyingi inahakikisha kati ya mambo mengine uhuru wa ibada, ambao unatangazwa kuwa wa juu, ambao Mahakama ya Kikatiba ya nchi ina jukumu la kuamua matendo fulani au maandalizi ya sheria yanalingana na Sheria ya Urusi. Lakini mkataba huo hauheshimiwi. Mahakama za Urusi ziko chini ya mamlaka iwe ya serikali kuu au ya maeneo, ambayo haiwajibiki chini ya Sheria. Pili, sheria za Urusi zinaweza kufafanuliwa kwa njia mbalimbali. Sheria za Urusi kuhusu msimamo mkali hazielezi waziwazi msimamo mkali unamaanisha nini. Kwa hiyo, sheria inaweza kufafanuliwa jinsi wenye Mamlaka wanavyotaka.”—Sir Andrew Wood, Uingereza

  • “Urusi ina haki na wajibu kwa watu wake kushughulikia msimamo mkali, lakini kutangaza vikundi vya kidini visivyopendwa kuwa na msimamo mkali wakati ambapo hawatishii usalama wa wengine ni kuwa na msimamo mkali. Nafikiri serikali ya sasa ya Urusi haihangaishwi na watu walio na msimamo mkali mradi wanaweza kuwadhibiti. Nahisi wanaogopa zaidi kikundi ambacho wanahisi hawawezi kukidhibiti. Kwa kuwa Mashahidi wa Yehova ni washikamanifu kwanza kwa Mungu, nafikiri serikali ya sasa inatumia mtajo ‘wenye msimamo mkali’ kuwaondoa Mashahidi. Pia, ninafikiri Kanisa Othodoksi la Urusi linajaribu kupunguza uvutano wa dini ndogo zinazohubiri.”—Prof. Ravitch, Marekani

  • “Sheria ya Urusi na jinsi wenye mamlaka wanavyoitumia inawanyima watu na mashirika mengi haki za msingi, kama haki ya kutoa maoni yao. Hata ikiwa maoni fulani ni kosa, lazima kuna haki ya kutoa maoni hayo. Mtu anaweza kuzuiwa kihalali mara chache sana ambapo anahatarisha uhai wa wengine au kuvuruga amani ya jamii. Mashahidi wa Yehova hawajafanya hivyo.”—Dakt. Bremer, Ujerumani

Sheria ya Urusi inasema kwamba waumini wanaweza kutangazwa kuwa na “msimamo mkali” kwa kutangaza ukweli na ubora wa dini yao. Je, huo unapaswa kuwa msingi wa kisheria wa kutambua msimamo mkali?

  • “Hapana. Hilo halipatani na akili, halionyeshi usawaziko, na linavunja haki za kibinadamu ambazo nchi ya Urusi imefanya mkataba kushikamana nayo, kutia ndani Kifungu cha 9 cha ECHR [Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu] na Kifungu cha 18 cha ICCPR [Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na za Kisiasa].”—Prof. Bowring, Uingereza

  • Prof. Garrett Epps

    “Hapana, sijui kanuni yoyote ya sheria ya kimataifa inayomruhusu mtu yeyote atangazwe kuwa na msimamo mkali kwa kuamini ukweli wa dini yake.”—Profesa Garrett Epps, profesa wa sheria, Chuo Kikuu cha Shule ya Sheria ya Baltimore; mwandishi wa Mahakama Kuu, The Atlantic, Marekani

  • “Kwanza, wazo hilo ni la ajabu sana. Ikiwa ingetekelezwa kwa haki, ingemaanisha dini zote zingepigwa marufuku kupitia sheria hiyo ya Urusi. Dini zote zinadai kwamba zina ukweli na waumini wote wanaamini kwamba imani yao ni ya kweli. Kama sivyo, dini ina thamani gani? Sheria hii ni mbinu ya kisheria ya kuruhusu nchi ya Urusi iwabague washiriki wa dini ndogo, hasa Mashahidi wa Yehova.”—Dakt. Baran, Marekani

  • “Nilifikiri kila mtu anaamini ubora wa dini yake. Ikiwa hawangefanya hivyo, wangehamia dini nyingine. Ni jambo hakika kwamba Mashahidi wa Yehova wanaamini kwamba wao pekee ndio walio na ‘ukweli,’ lakini dini nyingine za Kikristo na dini nyingine wamedai vivyo hivyo. Kuamini kwamba dini yako ni bora na ya pekee ni jambo linalopaswa kuruhusiwa kukiwa na uhuru wa kidini, kama ufafanuzi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu unavyoonyesha.”—Dakt. Chryssides, Uingereza

  • “Inashtua kwamba wataalamu wanaweza kutangaza utendaji wa kawaida wa kidini kuwa ‘msimamo mkali.’ Huo ndio msingi wa maisha katika jamii yoyote ya waumini wanaoishi wakiamini ukweli wao ulio wa pekee. Waumini wa jamii moja wanafafanua ukweli kwa njia yao na huo unakuwa msingi wa kufafanua maandishi matakatifu. Kwa sababu hiyo basi ufafanuzi wao ‘hautakuwa sawa na vikundi vingine vya kidini.’”—Dakt. Lunkin, Urusi

  • “Bila shaka, maoni hayo yamepita kiasi. Watu wa kidini wanachagua na kuishi kulingana na viwango vya dini walizochagua kwa sababu wanaviamini kuwa bora na kweli kuliko dini nyingine. Msimamo wa Urusi unadhihaki dini zote.”—Dakt. Davis, Marekani

  • “Katika visa vingi, dini zote zinaamini kwamba imani yao kumhusu Mungu ni kweli. Hakuna mtu anayesema, ‘Dini nyingine ni bora na ya kweli kuliko yetu.’”—Dakt. Bremer, Ujerumani

  • Dakt. Aidar Sultanov

    “Nafikiri swali hilo halihitaji jibu. Bila shaka, kila mwamini angependa wengine pia waokolewe badala ya kutangatanga gizani kwa sababu ya mawazo yenye makosa; ni kwa sababu hiyo waumini wanasisitiza usahihi wa dini yao.”—Dakt. Aidar Sultanov, msomi wa sheria wa Urusi na mwanaharakati wa haki za kibinadamu, Urusi

  • “Kama nilivyosema, msimamo mkali si dhana ya sosholojia ya dini. Ili kuchunguza ikiwa kikundi fulani cha kidini ni hatari kwa umma au kwa usalama wa nchi, lazima mtu achunguze matendo yake bali si imani yake. Ikiwa haitendi kinyume cha sheria, haipaswi kushutumiwa. Kikundi cha kidini kina haki ya kusema kwamba kinahisi kipo sehemu bora zaidi. Wanasiasa wote husema kwamba wao ndio bora na hakuna yeyote anayesema wana msimamo mkali. Sijawahi kumwona mwanasiasa anayesema kwamba yeye ni mwongo na kuwa chama chake cha kisiasa ni duni kuliko cha wanasiasa wengine. Kila kikundi kinafikiri kwamba ufafanuzi wao wa Maandiko Matakatifu ndio bora. Serikali zinapaswa kuhangaika ikiwa vikundi vinavunja sheria au vinajihusisha na jeuri.”—Dakt. Dericquebourg, Ubelgiji

  • “Marekebisho yaliyofanywa hivi karibuni yanayodhibiti kutangaza imani yamepita kiasi. Yanadhibiti sana uhuru wa kidini kwa kumzuia muumini kuamini au kutangaza kwa njia ya amani na yenye fadhili kwamba dini yake ni ya kweli.”—Dakt. Ferrari, Italia

  • “Kutangaza tu ukweli wa maoni ya mtu ya kidini na ubora wa imani fulani hakutoshi kuonyesha msimamo mkali. Dini nyingi zimeshikilia kwa bidii kweli zao na mara nyingi kweli hizo zinapingana na za dini nyingine na wanazibishania ana kwa ana. Licha ya kutofautiana huko, madai hayo yanatolewa kwa amani, njia ambayo haiingilii haki na uhuru wa wengine au kutishia amani ya umma. Kwa hakika, mradi maoni hayo yanayotofautiana yanatolewa bila vitisho au kuomba watendewe kwa jeuri au kuendeleza chuki iliyopita kiasi, basi ni sehemu ya msingi ya jamii inayoheshimu demokrasia. Ingawa ICCPR [Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na za Kisiasa] unaipa serikali jukumu la kukataza ‘kuendeleza . . . chuki ya kidini kwa kuchochea ubaguzi, chuki, au jeuri,’ chuki ya kidini lazima iwe imepita kiasi kabla ya serikali kuchukua hatua. Isitoshe, uamuzi wa serikali kuchukua hatua kwa msingi huo unapaswa kutimiza matakwa kabla matendo hayo yathibitishwe kwamba yanafaa. Uthibitisho mwingi katika matumizi ya sheria ya msimamo mkali nchini Urusi unaonyesha kwamba haukuzingatia vya kutosha sababu za kuchukua hatua au hata kujaribu kuelewa maoni yanayoonwa kuwa na ‘msimamo mkali.’”—Prof. Blitt, Marekani

  • “Suala si la uhuru wa kidini tu bali uhuru wa kusema. Sheria hiyo inamaanisha kwamba adhabu hiyo inaweza kutumiwa dhidi ya kikundi chochote cha kidini kisichopendwa na serikali au na vikundi vingine vya kidini vyenye uvutano mkubwa wa kufanya maamuzi ya kisiasa ili kuondoa uvutano wa mawazo ya kidini wasiyoyataka.”—Dakt. Ringvee, Estonia

  • “Kusema kwamba kutangaza ukweli na ubora wa dini ya mtu ni uthibitisho wa msimamo mkali ni uthibitisho mmoja wa jinsi sheria ya Urusi dhidi ya msimamo mkali ilivyo na kasoro. Angalau dini moja nchini Urusi imeshikilia misingi kama hiyo.”—Sir Andrew Wood, Uingereza

  • “Sheria ya Urusi inasema kwamba kupendekeza kwamba dini yako ni ya kweli ni maneno ya chuki au jeuri. Mpaka halisi, kulingana na mtazamo wa usalama wa taifa, unapaswa kuwa wakati ambapo mtu au kikundi cha kidini kinapendekeza wengine waumizwe, yaani, watu wanaposema kwamba dini yao inawalazimisha kuua watu wa imani nyingine. Serikali zinazingatia usalama zikidhibiti watu kama hao. Kuchochea jeuri: Ni kama kutangaza kwamba kuna moto ndani ya jumba la sinema au wenye mamlaka wa dini wakiwaelekeza watu waue. Lakini wale wanaolengwa na sheria hii ya Urusi hawafanyi hivyo.”—Dakt. Patterson, Marekani

  • “Sheria ya Urusi inapinga sehemu muhimu ya uhuru wa kidini au ibada kwa kutia ndani kutaja ubora wa dini kuwa sehemu ya msimamo mkali; hiyo ni sababu kubwa inayofanya USCIRF [Tume ya Marekani Inayoshughulikia Uhuru wa Kidini wa Kimataifa] ione sheria hiyo kuwa ‘tisho kubwa kwa uhuru wa kidini.’ Sehemu nyingine ya sheria inayokataza ‘kuchochea mgawanyiko wa kidini’ inatumiwa kupiga marufuku kuhubiri, hasa kuhusu vikundi visivyopendwa na serikali kama Mashahidi wa Yehova.”—Bi. Cosman, Marekani

  • “Kwa sababu sheria hiyo inapinga mtu kudai kwamba ana ukweli wa kidini au dini bora, hilo linamaanisha hana haki ya kuwa na dini (forum internum) na uhuru wa msingi haswa wa kuamini, kwa kweli ukiukwaji huo hauwezi kutetewa kwa njia yoyote ile.”—Dakt. Ventura, Italia

  • Dakt. Brian Grim

    “Vikundi vyote vya kidini wana haki ya kudai kwamba wana kweli na madai hayo si hatari. Kwa kweli, ni kawaida kwa dini nyingi kudai kwamba ndizo dini pekee zilizo na ukweli.”—Dakt. Brian Grim, rais, Uhuru wa Kidini & Msingi wa Kibiashara; profesa aliyezuru, Chuo Kikuu cha St. Mary’s University jijini London; mshauri, Tony Blair Faith Foundation; msomi, Mradi wa Uhuru wa Kidini, Chuo Kikuu cha Georgetown; msomi, Taasisi ya Utamaduni, Dini na Masuala ya Ulimwengu, Chuo Kikuu cha Boston, Marekani

  • “Uhuru wa kidini unahusisha haki ya waumini kutangaza kwamba dini yao ni ya kweli na bora na hakuna ukweli mwingine. Ingawa huenda wengine wasifurahie hilo, mradi hawajitahidi kuwalazimisha wengine wawe na maoni kama yao, basi wana haki ya kutangaza ukweli wa imani yao wenyewe.”—Dakt. Carolyn Evans, dean, Mwenyekiti wa Sheria wa Harrison Moore, Shule ya Sheria ya Melbourne, mhariri msaidizi wa Religion and International Law; mhariri msaidizi wa Law and Religion in Historical and Theoretical Perspectives, Australia

  • Dakt. William Cavanaugh

    “Ikiwa kutangaza ukweli wa dini ya mtu ni kuwa na ‘msimamo mkali’ basi waumini wengi wana hatia hiyo.”—Dakt. William Cavanaugh, profesa wa masomo ya Kikatoliki, msimamizi, Kituo cha Ukatoliki Ulimwenguni Pote na Masomo ya Dini, Chuo Kikuu cha DePaul, Marekani

  • Dakt. John A. Bernbaum

    “Kutangaza kwamba imani yako ni ya kweli si dalili ya ‘msimamo mkali wa kidini,’ badala yake ni kushikamana na viwango vyako vya msingi. Mradi viwango hivyo havisumbui imani au dini nyingine, vinapaswa kuungwa mkono na mamlaka kwa kuwa hiyo ni haki ya msingi.”—Dakt. John A. Bernbaum, rais, Taasisi ya Urusi na Marekani (Moscow), Marekani

Ninyi Wasomi na Wataalamu mnasemaje kuhusu Mashahidi wa Yehova; wanajulikana kuwa raia wa aina gani?

  • “Utafiti wangu kuhusu Mashahidi wa Yehova katika nchi kadhaa umenifanya nikutane na watu wenye amani, wanaofuata sheria na wanaotambua na kuheshimu dini nyinginezo na wakati huohuo wakijitahidi kuhakikisha wanashikamana na haki yao ya kuamini na kutenda kulingana na imani yao ya kidini. Jitihada zao, hasa kupitia mbinu za kisheria, zimeboresha sana uhuru wa dini au imani wa mtu mmoja-mmoja na wa jamii za dini nyingine ndogo na kubwa.”—Dakt. Effie Fokas, msimamizi (2008-2012), Forum on Religion, mtafiti, Hellenic Observatory, Shule ya Uchumi ya London; mwanasheria wa zamani wa Marie Curie, “Pluralism and Religious Freedom in Orthodox Countries in Europe” (PLUREL), Shirika la Ulaya na Sera za Kigeni la Ugiriki, Ugiriki

  • “Ninawajua Mashahidi wa Yehova si tu nikiwa msomi anayechunguza historia, mafundisho, na matendo yao, bali pia nikiwa mtu wa kawaida, yaani, katika maisha ya kila siku. Wao ni majirani, watu ninaofahamu, na watu ninaofanya kazi nao. Katika kazi yangu, wanaheshimiwa sana. Wanatii sheria. Wanaishi kwa amani na watu wengine, haidhuru maoni yao ya kisiasa au mapendezi ya kidini. Hawashughulikii tu masilahi na mahitaji ya jamii yao ya kidini. Mashahidi wa Yehova hawashiriki mambo ya kisiasa ya nchi, ni waangalifu kuhusu mambo wanayosema kuwahusu wenye mamlaka lakini wanaelewa mambo yanayotukia nchini mwao wakiwa raia. Ninaamini kwamba wanatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii, wanazidisha hali njema ya jamii na kuleta usawaziko, kwa sababu wanahubiri viwango vya Kikristo. Wana familia nzuri, waaminifu kwa wake na waume zao; wanawapenda wazazi na wanawajibika wanapowalea watoto wao.”—Dakt. Fylypovych, Ukrainia

  • “Mashahidi wa Yehova ninaowajua nchini Uingereza wanachangia katika jamii kwa kutafuta kazi halali na kulipa kodi bila kukwepa. Wanaona kutii sheria kuwa wajibu wa kidini, isipokuwa katika visa vichache tu ambapo wanaona kuwa sheria inapingana na uelewaji wao wa sheria ya Mungu.”—Dakt. Chryssides, Uingereza

  • “Baada ya kujifunza kuhusu dini mbalimbali nikiwa msomi wa mambo ya dini, ninajua kwamba Mashahidi wa Yehova hawapendi vurugu, bali wanapenda amani, ni shirika la kidini ambalo washiriki wake hawazungumzii au kushiriki siasa na hawaingilii masuala ya Serikali. Hata hivyo, waumini wanachangia katika jamii hii kwa kufanya kazi kwa unyoofu katika biashara na mashirika mbalimbali, kulipa kodi kwa unyoofu ili kutegemeza serikali, na kuwasaidia raia wenzao kukiwa na uhitaji, kama vile baada ya misiba ya asili au ya kijamii.”—Dakt. Elbakyan, Urusi

  • “Nimekutana na Mashahidi wengi wa Yehova maishani, na mwanafunzi wangu bora katika shahada ya Stashahada ya Haki za Kibinadamu alikuwa mwanamke mmoja ambaye ni Shahidi na aliyeandika maelezo marefu kuhusu uhuru wa ibada nchini Urusi. Kwa maoni yangu, Mashahidi wa Yehova wana tabia njema na hawakasiriki kwa sababu sikubaliani na imani yao.”—Prof. Bowring, Uingereza

  • Bw. Bruno Segre

    “Mimi binafsi baada ya kuwa wakili wa Mashahidi wa Yehova kwa miaka 60 iliyopita, ninaweza kusema kwamba—ingawa sikubaliani na maoni yao kuhusu Biblia—sikuzote nimewaona kuwa watu wenye viwango vya juu vya maadili, imani yenye nguvu, na utendaji wenye amani.”—Bw. Bruno Segre, wakili; mwanahabari, mhariri mkuu, L’INCONTRO; rais honorary, Taasisi ya Turin Institutional Laity; honorary president, National Association of Free Thought “Giordano Bruno,” Italia

  • “Kwa miaka kadhaa niliwachunguza Mashahidi wa Yehova ili niandike ripoti kuwahusu, na kisha niandike makala katika magazeti ya kisayansi kuwahusu. Ninaweza kusema kwamba Mashahidi ni raia wazuri na wanyoofu katika nchi wanazoishi. Hawajihusishi na masuala ya kisiasa ya nchi zao, lakini wanalipa kodi; wanashiriki mambo ya kawaida kama kujitolea kuwa wazimamoto; wanawasaidia watu wakati wa misiba ya asili kama mafuriko yaliyotokea Orange na Bollène nchini Ufaransa—bila kuwashawishi waliowasaidia wawe wafuasi wao. Wanafanya hivyo ili tu kuwasaidia watu. Mashahidi wanasaidia katika utafiti wa mbinu badala za kutiwa damu mishipani ambazo zinawasaidia watu wasio Mashahidi.”—Dakt. Dericquebourg, Ubelgiji

  • “Mashahidi wa Yehova wanajulikana kwa kuwa raia wenye bidii wanaotii sheria.”—Dakt. Knox, Uingereza

  • “Ninawaheshimu sana Mashahidi wa Yehova. Ni watu washikamanifu, wenye amani, wanachukulia kwa uzito tamaa ya kumheshimu Mungu, na wanawatumikia wengine kwa uaminifu. Ninajua waajiri wanaowatafuta Mashahidi wa Yehova wawaajiri kwa sababu ya unyoofu wao na bidii kazini.”—Dakt. Davis, Marekani

  • “Ninapoangalia hali ya Mashahidi wa Yehova nchini Estonia, ni wazi kwamba watu kwa ujumla wamebadili maoni yao katika miaka ya karibuni, sasa hawana maoni yasiyofaa kuwaelekea. Katika jamii yenye dini nyingi, Mashahidi wa Yehova ni kikundi kimoja cha kidini kati ya vikundi vingine.”—Dakt. Ringvee, Estonia

  • “Mashahidi wa Yehova wanaishi kwa amani wakiwa sehemu ya jamii.”—Prof. Clark, Marekani

  • “Inasikitisha kwamba Mashahidi wa Yehova wananyanyaswa kwa sababu hawapendwi na kikundi fulani katika jamii ambacho hakijui mafundisho na utendaji wa Mashahidi wa Yehova. Hata hivyo, licha ya kupekuliwa na kunyang’anywa vitabu na magazeti yao na kutangazwa kuwa na msimamo mkali, Mashahidi wa Yehova nchini Urusi bado wanaishi kulingana na sheria.”—Dakt. Lunkin, Urusi

  • “Wale ambao hawajashirikiana sana na Mashahidi wa Yehova huenda wanajua tu kwamba wanahubiri nyumba kwa nyumba, jambo ambalo linawaudhi watu fulani. Hata hivyo, huwa ninapenda kuwakumbusha watu kwamba haki ya Mashahidi kubisha mlango wako ni sehemu ya kuishi katika jamii ya kidemokrasia. Tunapaswa kuwashukuru Mashahidi kwa kutetea kisheria haki zao katika mahakama zetu, jambo ambalo limefanya uhuru wa kusema ulindwe zaidi.”—Dakt. Baran, Marekani

  • “Ninawafahamu Mashahidi wa Yehova hasa nchini Marekani na wamechangia sana katika jamii, wamechangia sana kutusaidia kuelewa maana ya Marekebisho ya Kwanza ya katiba kwa kutetea haki za kibinadamu katika kesi zinazojulikana kama kesi ya Barnette. Cha kushangaza ni kwamba huenda historia hiyo ya kutetea haki za kibinadamu ndiyo inawafanya wenye mamlaka nchini Urusi waogope.”—Prof. Ravitch, Marekani

  • “Kutokana na utafiti wangu wa historia ya Marekani ya kisheria, nimekuja kuthamini mchango mkubwa wa Mashahidi wa Yehova wa kuhakikisha kwamba haki za kibinadamu zinalindwa katika katiba. Azimio lao la kudhihirisha imani yao ya kidini waziwazi limefanya haki za Wamarekani wote zipanuliwe katika Marekebisho ya Kwanza ya katiba. Wamekuwa na mchango muhimu pia katika mataifa mengine, wakijinufaisha na kuwanufaisha washiriki wengi sana wa dini nyingine.”—Dakt. Peters, Marekani

  • Dakt. Ain Riistan

    “Katika nchi yangu ya Estonia, Mashahidi wa Yehova wanajulikana kuwa raia wazuri. Wanachangia katika jamii na kulipa kodi. Wao ni sehemu ya jamii inayotii sheria. Hawashiriki utumishi wa kijeshi, lakini kuna mfumo wa utumishi badala (kazi katika shule, hospitali na kadhalika), wanafanya kazi hizo.”—Dakt. Ain Riistan, mhadhiri wa Agano Jipya, Shule ya Theolojia na Masomo ya Kidini, Chuo Kikuu cha Tartu; profesa wa theolojia ya dini huru na historia ya dini, Seminari ya Theolojia ya Tartu, Estonia

  • “Nina marafiki kadhaa ambao ni Mashahidi Wagiriki. Majirani wa zamani huko Thessalonica (ambako niliishi) ni Mashahidi. Popote nilipo, mimi hupinga kunyanyaswa kusiko kwa haki kwa Mashahidi, kwa sababu ya kanuni na kwa sababu pia kwa ujumla wao ni Wakristo wanyoofu, wenye bidii, na washikamanifu.”—Dakt. Groen, Austria

  • “Kwa muda mfupi niliposhughulika na Mashahidi wa Yehova nchini Hispania nimeona kwamba wao ni watu wazuri, washikamanifu, na wanyoofu, wanashikilia sana mafundisho yao—ambalo si jambo baya, mradi unakuwa na mazungumzo yenye usawaziko pamoja nao.”—Dakt. Martínez-Torrón, Hispania

  • “Watu wenye imani kama Mashahidi wa Yehova ni raia muhimu katika nchi wanazoishi. Hupaswi kuogopa chochote kuhusu kikundi hiki cha kidini. Hawapaswi kubaguliwa.”—Dakt. Bernbaum, Marekani

  • “Kile ninachopenda kuwahusu Mashahidi wa Yehova ni kwamba hawapendi jeuri na wanapinga ibada ya sanamu, yaani, hawaabudu utaifa au bendera.”—Dakt. Cavanaugh, Marekani

  • “Ninaweza kusema kwamba jamii ya Ujerumani sikuzote imewaona kuwa raia wa kawaida, washikamanifu, na wasiojionyesha, kama watu wengine tu.”—Dakt. Bremer, Ujerumani

  • “Kuingilia maisha ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi ni ukosefu wa haki na hakuna msingi mzuri ukifikiria rekodi ya Mashahidi wa Yehova barani Ulaya na ulimwenguni pote ya kuwa jamii yenye amani, inayotafuta faida za kila mtu. Kama inavyothibitishwa na utafiti katika historia na sayansi ya jamii, Mashahidi wa Yehova wanafurahia msimamo mzuri katika jamii wa kufundisha kutii sheria, kutotenda kwa jeuri, na kuchangia kwa njia mbalimbali ukuzi, umoja, na maendeleo ya jamii. Uhuru wao ni chanzo chenye thamani katika pambano dhidi ya msimamo mkali, nchini Urusi na kwingineko.”—Dakt. Ventura, Italia

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu 1-718-560-5000

Urusi: Yaroslav Sivulskiy, simu 7-812-702-2691