Hamia kwenye habari

Mashahidi wa Yehova wakiimba wakati wa mkutano wa Kikristo Rostov-on-Don, Urusi

SEPTEMBA 22, 2016
URUSI

SEHEMU YA 1

Wataalamu Waeleza: Urusi Yatumia kwa Hila Sheria ya Kudhibiti Vikundi Vyenye Msimamo Mkali ili Kuwafanya Mashahidi wa Yehova waonekane kuwa Wahalifu

Wataalamu Waeleza: Urusi Yatumia kwa Hila Sheria ya Kudhibiti Vikundi Vyenye Msimamo Mkali ili Kuwafanya Mashahidi wa Yehova waonekane kuwa Wahalifu

Hii ni Sehemu ya 1 ya mfuatano wa mahojiano ya pekee yaliyo na sehemu tatu pamoja na wasomi maarufu wa mambo ya dini, siasa, na soshiolojia na pia wataalamu wa masomo yanayohusu Urusi ilipokuwa sehemu ya Muungano wa Sovieti na ilipojitenga na Muungano wa Sovieti.

ST. PETERSBURG, Urusi—Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Shirikisho la Urusi inadai kwamba Mashahidi wa Yehova wana “msimamo mkali wa kidini.” Iwapo mahakama itafanya uamuzi unaopendelea ofisi ya mwendesha-mashtaka, hilo linaweza kufanya shirika la kisheria la Mashahidi nchini Urusi lifungwe, na hivyo kupiga marufuku utendaji wa Mashahidi nchini kote. Mashahidi wamekata rufani mashtaka hayo na kesi hiyo inatazamiwa kuendelea Septemba 23, 2016.

Kesi hiyo dhidi ya Mashahidi inategemea sheria ya kudhibiti vikundi vyenye msimamo mkali ya Urusi ambayo wasomi wanasema “inabagua,” “ina kasoro nyingi,” na “haipatani na akili.”

Dakt. Derek H. Davis

Dakt. Derek H. Davis, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya J.M. Dawson ya Masomo ya Kanisa na Serikali katika Chuo Kikuu cha Baylor anasema hivi “Misimamo mikali ya kidini ambayo inahatarisha maisha ya watu ndiyo inayohitaji kudhibitiwa.” Kisha akaongeza hivi, “kudhibiti mambo ambayo hayahatarishi usalama wa taifa ni kuwa na msimamo mkali.”

Dakt. Mark Juergensmeyer

Dakt  Mark Juergensmeyer, mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Masomo ya Ulimwengu na ya Kimataifa cha Orfalea katika Chuo Kikuu cha California, jijini Santa Barbara anaeleza kwa nini kuchukuliwa kwa hatua kali hivyo dhidi ya kikundi cha kidini kisichofanya jeuri kama Mashahidi ni msimamo mkali, aliposema hivi: “Kuwanyima wengine uhuru wa kidini huku ukidai kwamba unakabiliana na dini zenye msimamo mkali ni hila isiyofaa.” Kwa kuongezea, Dakt. Jim Beckford, wa chuo cha British Academy anaeleza kwamba “baadhi ya watu katika Kanisa Othodoksi la Urusi wanapanga hila na wenye mamlaka ili kuchochea mapendezi yao wenyewe na kuzuia chochote wanachoona kuwa ushindani.”

Dakt. Jim Beckford

Wataalamu wanaeleza kuwa tatizo si kwamba tu sheria hiyo inatumiwa isivyofaa bali pia sheria hiyo imefanyizwa kwa njia ambayo inaruhusu itumike vibaya. Kituo cha SOVA cha kutetea haki za kibinadamu kilicho na makao yake jijini Moscow kinaripoti hivi: “Kama ambavyo tumekuwa tukisema, sheria ya kudhibiti vikundi vyenye msimamo mkali, na kifungu chake cha maneno yasiyoeleweka vizuri, inatumiwa kuhukumu vyama pinzani vya kisiasa au vikundi vinavyoonekana kuwa tofauti.”

Dakt. Emily B. Baran

Dakt. Emily B. Baran, profesa msaidizi wa historia ya Urusi na Ulaya Mashariki katika Chuo Kikuu cha Middle Tennessee anasema hivi: “Raia wa Urusi wanapaswa kuhuzunishwa na uamuzi huu wa serikali wa kuwabagua Mashahidi, kwa sababu hilo linaonyesha kwamba serikali iko tayari kuondoa usawa wa haki kwa vikundi vingine na kufanya hivyo pia kuelekea jamii zenye watu wachache.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, 1-718-560-5000

Russia: Yaroslav Sivulskiy, 7-812-702-2691