Hamia kwenye habari

FEBRUARI 17, 2017
URUSI

Mahakama Kuu ya Urusi Imeamua Kufunga Shirika Lingine la Kisheria kwa Madai ya Msimamo Mkali

Mahakama Kuu ya Urusi Imeamua Kufunga Shirika Lingine la Kisheria kwa Madai ya Msimamo Mkali

Februari 9, 2017, Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi ilitoa uamuzi wa kufunga shirika la kidini la Mashahidi wa Yehova Local Religious Organization (LRO) la Birobidzhan. Mahakama hiyo Kuu iliunga mkono uamuzi uliotolewa na mahakama ya chini ambayo ilitangaza kwamba shirika hilo lilikuwa likichochea msimamo mkali wa kidini na ilipiga marufuku utendaji wake.

Uamuzi huo unategemea uthibitisho wa uwongo. Mwezi wa Februari 2015 na Januari 2016, polisi walipandikiza machapisho ya kidini yaliyopigwa marufuku kwenye majengo yaliyokodiwa na Mashahidi kwa ajili ya ibada na kisha kujifanya kuwa wameyakamata machapisho hayo. Katika tukio la Januari, polisi maalumu walioziba nyuso zao walivuruga mkutano wa kidini na kupandikiza chapisho chini ya kiti huku wahudhuriaji wakiwatazama.

Shirika hilo la Birobidzhan, lipo kwenye Eneo Lililotengewa Wayahudi Nchini Urusi, na ndilo shirika la kwanza la kidini kufungwa tangu Mahakama ya Jiji la Moscow ilipoamua kwamba onyo la Mwendesha-Mashtaka Mkuu dhidi ya makao makuu ya Mashahidi litekelezwe.