Hamia kwenye habari

APRILI 7, 2016
URUSI

Wenye Mamlaka Nchini Urusi Wapanga Kufunga Makao Makuu ya Mashahidi wa Yehova

Wenye Mamlaka Nchini Urusi Wapanga Kufunga Makao Makuu ya Mashahidi wa Yehova

ST. PETERSBURG, Urusi—Kwa mara ya kwanza nchini Urusi, wenye mamlaka wametishia kufunga makao makuu ya Mashahidi wa Yehova nchini humo.

Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka Mkuu ya Shirikisho la Urusi ilituma barua ya onyo Machi 2, 2016, iliyosema kwamba “shirika la dini litafungwa” ikiwa kituo cha usimamizi kitashindwa kuondoa “ukiukwaji wa sheria” ambao serikali unauona kuwa ni “msimamo mkali wa kidini” ndani ya miezi miwili. Msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi, Yaroslav Sivulskiy, anasema hivi: “Kufungwa kwa makao yetu makuu kunaweza kuhusisha kutaifishwa kwa mali zote tunazomiliki na hatimaye kupigwa marufuku kwa utendaji wa Mashahidi wa Yehova katika nchi nzima ya Urusi.”

Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova nchini Urusi.

Tukio hilo linashangaza kwa sababu limetokea Mashahidi wa Yehova nchini Urusi wanapotimiza miaka 25 baada ya kusajiliwa kisheria: Kituo cha Usimamizi kilisajiliwa rasmi kisheria Machi 27, 1991, na kikasajiliwa tena kwa mara nyingine Aprili 29, 1999. Tishio la kufunga makao makuu ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi ambayo yako katika kijiji cha Solnechnoye kilichoko kilomita 40 Kaskazini-Magharibi mwa jiji la St. Petersburg, litakuwa ni tukio la karibuni zaidi la ukandamizaji wa serikali dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Mwaka uliopita wenye mamlaka nchini Urusi walizuia machapisho ya kidini yasiingizwe nchini, kutia ndani Biblia za Kirusi, na Urusi ikawa nchi pekee duniani kupiga marufuku tovuti rasmi ya Mashahidi, jw.org. Bw. Sivulskiy, anasema hivi: “Sheria ya kupinga dini zenye msimamo mkali imetumiwa vibaya dhidi ya ibada ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi. Mashahidi wa Yehova wamepinga mashtaka hayo. Tungependa kufanya ibada na kazi yetu ya kutoa elimu ya Biblia kwa uhuru, kama ambavyo tumekuwa tukifanya hapa nchini kwa miaka 125.”

Hata hivyo, wenye mamlaka nchini Urusi wameongeza uhasama dhidi ya Mashahidi wa Yehova hasa kwa sababu ya uhusiano uliopo kati ya serikali na Kanisa Othodoksi la Urusi. Vyombo vya habari vya kimataifa kama vile The New York Times vimeripoti kwamba “ushirikiano huo kati ya serikali na Kanisa Othodoksi la Urusi,” umekuwa kichocheo kikubwa cha matendo ya jeuri na utungaji wa sheria zinazokusudiwa kuwakandamiza Mashahidi wa Yehova pamoja na dini nyingine ndogondogo zilizopo nchini Urusi. Shirika la habari la Associated Press nchini Marekani liliripoti kwamba “mipango ya serikali dhidi ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi imewashtua watu wanaopigania haki za uhuru wa kidini.” Ripoti kutoka katika shirika la habari la Reuters ilisema kwamba vitendo hivyo vinafanywa “dhidi ya Mashahidi wa Yehova na wengine wengi wanaofunguliwa mashtaka kwa msingi wa sheria ya kudhibiti vikundi vyenye msimamo mkali wa kidini.” Desemba 2015, gazeti The Independent liliripoti kuwa sheria hiyo ya Urusi ilikusudiwa “kuzuia matukio ya kigaidi na vurugu nchini humo.” Hata hivyo, sheria hiyo imetumiwa “kuwatesa washiriki wa dini zenye amani” kama Mashahidi wa Yehova, likasema gazeti la The Huffington Post katika Machi 20, 2016. Ingawa Mashahidi wa Yehova wanatafuta haki ya kisheria katika mahakama za nchi hiyo na pia katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu, gazeti la The Moscow Times la Machi 25, 2016, liliripoti kwamba serikali ya Urusi imepitisha sheria mpya “inayozipa mahakama za Urusi haki ya kupinga maamuzi ya mahakama za kimataifa.”

Wageni wakiwa kwenye eneo la mapokezi la Kituo cha Usimamizi.

Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova nchini Urusi kinatumiwa na Mashahidi kupanga na kutegemeza kazi ya elimu ya Biblia inayotolewa bila malipo kwa raia wa Urusi. Wahudumu wenye uzoefu wa kituo hicho cha usimamizi wanasaidia na kuwasiliana na Mashahidi wanaojitolea kwa hiari nchini Urusi kutoa msaada kwa watu walioathiriwa na misiba ya asili. Idadi ya watu nchini Urusi ni 146,000,000, na kati yao 175,000 ni Mashahidi wa Yehova.

David A. Semonian, msemaji wa Mashahidi wa Yehova katika makao yao makuu ya ulimwenguni pote yaliyoko jijini New York, anasema hivi: “Inavunja moyo sana kuona serikali inaweza kutoa tishio la kufunga ofisi ya tawi ya Urusi. Mashahidi wa Yehova na watu wengine wengi duniani pote wanafuatilia kwa makini ili kuona jinsi jambo hilo litakavyoendelea.”

Wanahabari wanaweza kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Urusi: Yaroslav Sivulskiy, simu +7 812 702 2691