Hamia kwenye habari

Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya katika Kirusi

NOVEMBA 18, 2016
URUSI

SEHEMU YA 2

Wataalamu Wapinga Tishio la Urusi la Kupiga Marufuku Biblia TakatifuTafsiri ya Ulimwengu Mpya

Wataalamu Wapinga Tishio la Urusi la Kupiga Marufuku Biblia TakatifuTafsiri ya Ulimwengu Mpya

Hii ni Sehemu ya 2 ya mfuatano wa mahojiano ya pekee yaliyo na sehemu tatu pamoja na wasomi maarufu wa mambo ya dini, siasa, na soshiolojia na pia wataalamu wanaofahamu ule uliokuwa Muungano wa Sovieti na hali baada ya kuvunjika kwa Muungano wa Sovieti.

ST. PETERSBURG, Urusi—Wenye mamlaka nchini Urusi wametishia kupiga marufuku Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya iliyochapishwa na Mashahidi wa Yehova kwa madai ya kwamba ni yenye “msimamo mkali.”

Dakt. Ekaterina Elbakyan

Ikiwa mahakama itawapa ushindi wanaoendesha mashtaka, marufuku yoyote dhidi ya Tafsiri ya Ulimwengu Mpya “yatakiuka marekebisho ya Kifungu cha 3 cha Sheria ya Shirikisho Kuhusu Msimamo Mkali kilichotiwa sahihi na Bw. Putin mwaka wa 2015,” anaeleza Dakt. Ekaterina Elbakyan, profesa wa soshiolojia na usimamizi wa mipango ya jamii wa Kituo cha Elimu ya Kazi na Mahusiano ya Kijamii cha Moscow (Moscow Academy of Labor and Social Relations). Marekebisho ya Kifungu hicho cha 3 yanasema hivi waziwazi: “Biblia, Kurani, Tanakh, na Kangyur, pamoja na habari zilizomo na manukuu kutoka humo hazipaswi kuonwa habari zenye msimamo mkali.”

Dakt. Roman Lunkin

Dakt. Roman Lunkin, mkuu wa Kituo cha Dini na Jamii kilicho katika Taasisi ya Ulaya ya Chuo cha Sayansi cha Urusi jijini Moscow anasema hivi: “Ni nani angeweza kuwazia kwamba kuwekwa kwa sheria inayolinda baadhi ya maandiko matakatifu kungechochea kupigwa marufuku kwa maandiko mengine matakatifu? Watu wa kwanza kuathiriwa na sheria hii ni Mashahidi wa Yehova na tafsiri yao ya Biblia.”

Dakt. Jeffrey Haynes

Kwa kuongezea, Dakt. Jeffrey Haynes, profesa wa siasa na mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Dini, Vita na Ushirikiano kilicho katika Chuo Kikuu cha London Metropolitan anasema hivi: “Kwa kuwa Urusi ni nchi mwanachama wa ICCPR [Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa], kujaribu kupiga marufuku Biblia kama hiyo kungekuwa kukiuka mikataba ya uhuru wa kidini.”

Kesi dhidi ya Tafsiri ya Ulimwengu Mpya inasikilizwa kwenye Mahakama ya Jiji la Vyborg, kilomita 138 kaskazini-magharibi mwa jiji la St. Petersburg. Aprili 26, 2016, siku ya pili ya kusikizwa kwa kesi hiyo mara ya kwanza, hakimu alikubali ombi la mwendesha-mashtaka la kusimamishwa kwa kesi hiyo ili kuipa mahakama wakati wa kutosha kuifanyia uchunguzi Tafsiri ya Ulimwengu Mpya. Mashahidi hawakupewa nafasi ya kujitetea, na mahakama iliamuru uchunguzi huo ufanywe na Kituo cha Masomo ya Kitaalamu ya Jamii na Utamaduni. Kwa kuamua Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ichunguzwe tena kituo hicho, mahakama hiyo ilikiuka mwelekezo uliowekwa na Mahakama Kuu ya Urusi kwamba mtaalamu yeyote hapaswi kuruhusiwa kutoa maoni kuhusu jambo linalojadiliwa mahakamani ikiwa alifanya hivyo hapo awali. Mwendesha-mashtaka tayari alikuwa ametumia mikataa isiyofaa ya kituo hicho kuwa msingi wa kesi yake dhidi ya Tafsiri ya Ulimwengu Mpya.

Dakt. Gerhard Besier

Uchunguzi huo wa mahakama unaposubiriwa, wasomi wameeleza maoni yao kuhusu tafsiri ya Mashahidi. Msomi mmoja, Dakt. Gerhard Besier, mkurugenzi wa Taasisi ya Sigmund Neumann ya Uchunguzi wa Uhuru na Demokrasia, anaeleza hivi: “Tafsiri ya Ulimwengu Mpya imesifiwa sana na wasomi wa Biblia wa dini mbalimbali kutoka duniani pote.”

Vivyo hivyo, Kituo cha SOVA cha Moscow cha Habari na Uchunguzi kilisema hivi katika toleo la Februari 2016 la jarida la kila mwezi linaloitwa Kutumiwa Vibaya kwa Sheria ya Kupambana na Msimamo Mkali: “Hatujapata kitu chochote kinachoonyesha kwamba Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ina msimamo mkali.” Tangu wakati huo, katika karibu kila toleo la mwezi, kituo cha SOVA kimeeleza tena na tena msimamo wake thabiti dhidi ya matendo ya Urusi. Jarida la Juni 2016 lilisema hivi: “Tungependa kurudia kusema kwamba tunaona mateso dhidi ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi na kupigwa marufuku kwa machapisho yao na jamii yao kuwa ni ubaguzi wa kidini.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, 1-718-560-5000

Urusi: Yaroslav Sivulskiy, 7-812-702-2691