Hamia kwenye habari

DESEMBA 2, 2015
URUSI

Mahakama ya Jiji la Taganrog Yawahukumu Mashahidi wa Yehova kwa Utendaji wa Kidini

Mahakama ya Jiji la Taganrog Yawahukumu Mashahidi wa Yehova kwa Utendaji wa Kidini

Baada ya miezi 11 ya kusikiliza kesi upya, Mahakama ya Jiji la Taganrog iliwahukumu Mashahidi wa Yehova 16 kuwa na hatia ya kupanga na kuhudhuria mikutano ya kidini kwa amani. Uamuzi huo wa mahakama ulitegemea sheria inayowaadhibu watu wanaopanga na kushiriki katika utendaji wenye msimamo mkali. Mashtaka hayo yalifunguliwa kwa msingi wa kesi nyingine iliyoendeshwa katika mahakama ya wilaya mwaka 2009, iliyotumia vibaya sheria ya Urusi ya kuwaadhibu watu wenye msimamo mkali. a

Novemba 30, 2015, Hakimu A. V. Vasyutchenko aliwahukumu Mashahidi wanne vifungo vya zaidi ya miaka mitano gerezani kwa hatia ya kupanga mikutano ya ibada na kuwatoza kila mmoja faini ya rubo 100,000 (dola 1,511 za Marekani). Washtakiwa wengine 12 walitozwa faini za kuanzia rubo 20,000 hadi 70,000 (dola 300 hadi 1,050 za Marekani) kila mmoja. Hata hivyo, mara moja hakimu huyo aliahirisha vifungo hivyo vya gerezani na faini, na kwa sasa haijulikani jinsi kufanya hivyo kutakavyowaathiri washtakiwa. Licha ya uamuzi huo bado washtakiwa hao wamehukumiwa hatia ya kosa la uhalifu.

Wakabili Maamuzi Magumu

Zaidi ya Mashahidi 800 jijini Taganrog wanaokutana kwa amani kuzungumzia Biblia na kusali pamoja, wanakabili vitisho vya kuadhibiwa. Walipokuwa mahakamani washtakiwa wote walieleza wazi wataendelea kuabudu wakiwa Mashahidi wa Yehova. Hukumu hiyo itajaribu azimio hilo. Aleksandr Skvortsov, aliyehukumiwa kuwa na hatia, anasema hivi: “Mahakama ilituambia hivi wazi, ‘Kana imani yako au utahukumiwa kuwa mkosaji anayerudia kosa.’”

Baada ya hukumu hiyo ya Taganrog kutolewa, Mashahidi wengine nchini Urusi wana wasiwasi. Wenye mamlaka katika majiji ya Samara na Abinsk wamefuata maoni ya Taganrog ya kutumia vibaya Sheria ya Kudhibiti Vikundi Vyenye Msimamo Mkali kama msingi wa kusitisha ibada inayofanywa kwa amani na Mashahidi na kufunga mashirika yao ya kisheria. Ikiwa wenye mamlaka nchini Urusi wataendelea kutumia vibaya sheria hiyo, itakuwa vigumu kwa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi kufurahia uhuru wa ibada.

Tutaendelea Kupigania Uhuru wa Kidini

Hukumu hiyo iliyotolewa inaonyesha jinsi wenye mamlaka nchini Urusi walivyoazimia kukomesha dini ya Mashahidi wa Yehova. Mwaka uliopita, wenye mamlaka nchini Urusi wamedai kwamba mashirika mawili wa kisheria ya Mashahidi ni yenye msimamo mkali. Tangu Machi 2015, wenye mamlaka wamewakataza Mashahidi kuingiza nchini machapisho yoyote ya kidini kutia ndani Biblia. Mwezi wa Julai, Urusi ilikuwa nchi ya kwanza na pekee ulimwenguni kupiga marufuku tovuti rasmi ya Mashahidi wa Yehova, jw.org. Mashahidi wa Yehova wamepinga maamuzi hayo katika mahakama nchini humo na wamepeleka maombi 28 kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu, ili kupata utatuzi wa ukiukwaji huo wa haki za kibinadamu nchini Urusi.

Mashahidi hao 16 jijini Taganrog watakata rufani kupinga hukumu hiyo na kuanza hatua nyingine katika pigano hili refu la kisheria. Yaroslav Sivulskiy, mwakilishi wa Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova nchini Urusi alieleza hivi: “Kesi imekuwa ikiendeshwa kwa miaka miwili na nusu sasa. Na inasikitisha kwamba bado watarudi tena mahakamani ili kutetea haki yao ya uhuru wa kuabudu ambayo imo katika katiba ya nchi.”

Mashahidi wa Yehova hawana msimamo mkali wa kidini. Ibada yao inafundisha watu kumpenda Mungu na jirani zao. Mashahidi wa jijini Taganrog wanazungumzia habari zilezile ambazo waabudu wenzao ulimwenguni pote wanazungumzia kila juma katika mikutano yao. Licha ya visa zaidi ya 1,700 vilivyorekodiwa vya kutendewa vibaya na wenye mamlaka nchini Urusi, Mashahidi wa Yehova hawajatenda kwa njia yoyote ile kinyume cha sheria.

Mashahidi wa Yehova wanatarajia kwamba mamlaka nchini Urusi zitaona wazi jinsi ambavyo utendaji wao wa kidini ni wenye amani na kuacha kuwafungulia mashtaka jijini Taganrog na katika sehemu nyingine. Mamlaka hizo zinapaswa kuwapatia Mashahidi wa Yehova haki ileile ya msingi ya uhuru wa ibada kama zinavyopatia dini nyingine zinazotambulika.

Mfuatano wa Kusikilizwa kwa Kesi b

  1. Januari 22, 2015

    Kesi iliyosikilizwa upya ya Mashahidi 16 wa Yehova yaanza katika Mahakama ya Jiji la Taganrog.

  2. Juni 2015

    Hakimu aahirisha kusikiliza kesi hiyo hadi Oktoba.

  3. Novemba 13, 2015

    Hakimu asimamisha usikilizaji wa kesi ili kufanya uamuzi.

  4. Novemba 30, 2015

    Mahakama ya Jiji la Taganrog yawahukumu Mashahidi wote 16 kuwa na hatia. Wote wanatozwa faini, na wanne wahukumiwa vifungo vya zaidi ya miaka mitano gerezani. Hakimu anaahirisha faini na vifungo hivyo.

b Kupata mfululizo wa matukio wakati kesi iliposikilizwa kwa mara ya kwanza, ona “Uamuzi wa Kesi Iliyosikilizwa Upya ya Mashahidi wa Yehova 16 huko Taganrog, Waahirishwa.”