Hamia kwenye habari

JUNI 28, 2016
URUSI

Uamuzi Unaotarajiwa Katika Kesi ya Kujaribu Kufunga Makao Makuu ya Mashahidi Nchini Urusi

Uamuzi Unaotarajiwa Katika Kesi ya Kujaribu Kufunga Makao Makuu ya Mashahidi Nchini Urusi

Mahakama ya Wilaya ya Tver jijini Moscow itatoa hukumu hivi karibuni katika kesi ya rufaa waliyofungua Mashahidi wa Yehova nchini Urusi ili kupinga jitihada za kutaka kufunga ofisi yao ya taifa. Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu ilitoa onyo, ikatishia kufunga Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova nchini Urusi kwa madai ya “utendaji wenye msimamo mkali.”

Mashahidi wa Yehova wanaomba mahakama itangaze kwamba onyo la mwendesha mashtaka mkuu linakiuka sheria. Onyo hilo linapingana na haki ya uhuru wa ibada ya Mashahidi na linategemea kutumiwa vibaya kimakusudi kwa sheria ya Urusi ya kupambana na shughuli zenye msimamo mkali.

“Hatujawahi kujihusisha na utendaji wowote wenye msimamo mkali,” anasema Vasiliy Kalin, mwakilishi wa Kituo cha Usimamizi. “Tunatumaini kwamba mahakama itarekebisha ukosefu huo wa haki.”