Hamia kwenye habari

FEBRUARI 27, 2017
URUSI

Wizara ya Haki Imefanya Ukaguzi Mkubwa Kwenye Ofisi ya Taifa ya Mashahidi Nchini Urusi

Wizara ya Haki Imefanya Ukaguzi Mkubwa Kwenye Ofisi ya Taifa ya Mashahidi Nchini Urusi

Wizara ya Haki ya Urusi inafanya ukaguzi mkubwa kwenye ofisi ya kitaifa ya Mashahidi nchini Urusi. Kupitia amri ya Mwendesha-Mashtaka Mkuu, Wizara hiyo iliwapa taarifa Mashahidi Februari 1, 2017, kwamba watafanya ukaguzi katika Kituo chao cha Usimamizi. Ikiwa ni sehemu ya ukaguzi huo ambao ulipangwa kufanyika Februari 8 hadi 27, Wizara hiyo iliagiza Kituo cha Usimamizi kitoe rekodi zote kuhusu mali wanazomiliki, ripoti za fedha, muundo wa tengenezo, shughuli za elimu, na mambo wanayoamini. Kituo cha Usimamizi kiliwasilisha nyaraka muhimu zenye zaidi ya kurasa 73,000 kwa wenye mamlaka mnamo Februari 15, 2017.

Ukaguzi huu mkubwa unakuja baada ya uamuzi wa karibuni wa Mahakama ya Jiji la Moscow ambao uliunga mkono onyo la Mwendesha-Mashtaka Mkuu dhidi ya Kituo cha Usimamizi lililotolewa Machi 2016. Kwenye onyo hilo, Mwendesha-Mashtaka Mkuu alitishia kukifunga Kituo cha Usimamizi kwa mashtaka ya kuchochea msimamo mkali wa kidini. Tangu wakati huo, mahakama katika maeneo mbalimbali ya Urusi yamefanya uamuzi wa kuyafunga baadhi mashirika ya kisheria ya Mashahidi kwa madai ya kuhusika katika “utendaji unaochochea msimamo mkali wa kidini,” licha ya ushahidi wa wazi kabisa kwamba msingi mashtaka hayo ni uthibitisho wa uwongo.

Kwa sababu ya ukaguzi huu, Mashahidi wa Yehova nchini Urusi wanahofu kwamba tishio la kufungwa kwa ofisi yao ya taifa linakaribia kutekelezwa. Wenye mamlaka nchini Urusi wameonyesha wazi kwamba wana nia ya kupuuza viwango vya kimataifa vya haki za kibinadamu kwa kuishambulia na ikiwezekana hata kuizuia ibada ya Mashahidi wa Yehova inayoendeshwa kwa amani.