FEBRUARI 22, 2016
URUSI
Mwendesha-Mashtaka Nchini Urusi Ataka Biblia Itambuliwe Kuwa Yenye Msimamo Mkali
Katika jitihada yao nyingine ya kudhibiti uhuru wa kidini, wenye mamlaka nchini Urusi wamefungua kesi ya mashtaka wakitaka Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya itambuliwe kuwa yenye msimamo mkali wa kidini. Kesi hiyo itaanza kusikilizwa Machi 15, 2016. Katika mwaka uliopita, kwa mara ya kwanza, maofisa wa forodha nchini Urusi walikataza kuingizwa kwa Biblia nchini humo. Hatua yao ya karibuni ya kufungua kesi hiyo ya mashtaka ni shambulizi linaloshushia heshima maadishi matakatifu ya Kikristo.
Sheria ya nchini Urusi inakataza kitendo cha kuiita Biblia kuwa ni kitabu chenye msimamo mkali wa kidini. Hata hivyo, Mwendesha-mashtaka wa Usafirishaji kwenye kituo cha Leningrad-Finlyandskiy anatetea kesi yake akitegemea maoni ya mtu ambaye si msomi wa lugha. Ikiwa kesi ya mwendesha-mashtaka huyo itashinda, Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya inaweza kupigwa marufuku nchini Urusi.