Hamia kwenye habari

Mahakama Kuu ya Zimbabwe iliyo Mutare. Picha ndogo (kushoto hadi kulia): Ndugu Jabulani Sithole, Ndugu Wonder Muposheri, na Ndugu Tobias Gabaza

NOVEMBA 18, 2022
ZIMBABWE

Mahakama Kuu Nchini Zimbabwe Yawaunga Mkono Mashahidi wa Yehova Katika Kesi ya Haki za Kidini

Mahakama Kuu Nchini Zimbabwe Yawaunga Mkono Mashahidi wa Yehova Katika Kesi ya Haki za Kidini

Septemba 29, 2022, Mahakama Kuu nchini Zimbabwe iliyo Mutare ilitoa uamuzi uliowaunga mkono Ndugu Tobias Gabaza, Ndugu Wonder Muposheri, na Ndugu Jabulani Sithole, ambao walitendewa isivyo haki kwa kuwa walikataa kushiriki katika sherehe ya kidini kwa sababu ya dhamiri zao.

Mnamo Oktoba 2020, ndugu hao watatu waliagizwa wafike mbele ya mahakama ambayo inasimamiwa na chifu wa kijiji baada ya ofisa mmoja wa kijiji kusisitiza kwamba walipaswa kushiriki katika sherehe ya kitamaduni kijijini humo. Sherehe hiyo inatia ndani ibada ya roho za wafu kwa kusudi la kuleta majira ya mvua na kila mwanakijiji anatazamiwa kushiriki. Ndugu zetu walikataa kushiriki katika sherehe hiyo. Walifanya uamuzi huo kwa kutegemea dhamiri zao zilizozoezwa kulingana na kanuni za Biblia.

Chifu wa kijiji hicho alitoa uamuzi dhidi ya ndugu zetu na kuwatisha akitaka kuwalazimisha kushiriki. Ndugu zetu waliamua kukata rufaa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi iliyo Chipinge.

Januari 5, 2021, Mahakama ya Hakimu Mkazi ilitoa uamuzi uliowaunga mkono ndugu zetu. Hata hivyo, maofisa wa kijiji walikataa kutii uamuzi wa mahakama hiyo na wakaendelea kuwashinikiza ndugu zetu. Isitoshe, wanakijiji wengine walianza kuwabagua na kuwatendea isivyo haki.

Kwa kuwa ndugu zetu waliendelea kutendewa isivyo haki, walikata rufaa kwenye Mahakama Kuu. Mahakama hiyo ilisema kwamba maofisa wa kijiji walikiuka haki za ndugu zetu. Vilevile, iliwaagiza maofisa wa kijiji wasiwahusishe ndugu zetu katika sherehe zozote za kitamaduni zisizopatana na dhamiri zao na pia ikawaamuru wawalipe fidia.

Tunaamini kwamba uamuzi huu utawanufaisha ndugu na dada zetu kotekote nchini Zimbabwe, kwa sababu tamaduni hizo zinafuatwa katika nchi nzima. Tunamshukuru Yehova kwa sababu ya ushindi huo.​—Methali 2:8.