Kutiwa Damu Mishipani—Madaktari Wanasema Nini Sasa?
Kwa miongo mingi, Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakichambuliwa kwa sababu ya kukataa kutiwa damu mishipani. Nyakati nyingine msimamo huo unaotegemea mwongozo wa Biblia wa ‘kujiepusha na damu,’ umepingana na maoni ya madaktari wanaohangaikia masilahi ya kitiba ya wagonjwa wao.—Matendo 15:29.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wenye uzoefu wametoa sababu za kitiba za kutumia njia za matibabu zisizohusisha damu.
Toleo la mwaka wa 2013 la gazeti Stanford Medicine Magazine, linalochapishwa na Kitengo cha Kitiba cha Chuo Kikuu cha Stanford, lilikuwa na ripoti maalumu kuhusu damu, yenye kichwa “Tiba Bila Damu—Ni Nini Kilichopunguza Visa vya Kuwatia Wagonjwa Damu Mishipani?” Mwandishi wa makala hiyo, Sarah C. P. Williams, anasema: “Kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita, utafiti mkubwa uliofanywa umeonyesha kwamba katika hospitali ulimwenguni pote, damu hutumiwa mara nyingi na kwa kiasi kikubwa kuliko inavyohitajiwa, kwenye vyumba vya upasuaji na katika wadi za hospitali.”
Mwandishi wa ripoti hiyo alimnukuu Patricia Ford, M.D., mwanzilishi na mkurugenzi wa Kituo cha Matibabu na Upasuaji Usiohusisha Damu katika Hospitali ya Pennsylvania. Alisema hivi: “Kuna kasumba iliyowaingia madaktari wengi kwamba watu watakufa ikiwa hawana kiwango fulani cha damu, na kwamba damu ndiyo kitu pekee kinachoweza kuokoa uhai wao . . . Hilo ni kweli katika visa fulani hususa, * lakini si kwa wagonjwa wote.”
Pia, Dkt. Ford, anayewatibu Mashahidi wa Yehova 700 hivi kila mwaka, alisema hivi: “Madaktari wengi niliozungumza nao . . . wanaamini kimakosa kwamba wagonjwa wengi hawawezi kupona bila kutiwa damu mishipani . . . hata mimi mwenyewe nilifikiri hivyo kwa kiasi fulani. Lakini nilijifunza kuwa inawezekana kumtibu mgonjwa kwa kutumia tu njia rahisi za matibabu.”
Mnamo mwezi wa Agosti 2012, jarida la Archives of Internal Medicine (Hifadhi ya Mambo Yanayohusu Tiba ya Sehemu za Ndani za Mwili) lilichapisha matokeo ya utafiti uliofanywa kwa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa moyo kwenye kituo kimoja katika kipindi cha miaka 28. Mashahidi wa Yehova walipona haraka kuliko wagonjwa wengine waliotiwa damu mishipani na waliokuwa wakiugua magonjwa kama yao. Mashahidi walipata matatizo machache wakiwa hospitalini, walipona haraka baada ya upasuaji, na waliendelea kuwa hai baada ya miaka 20 ikilinganishwa na wagonjwa waliotiwa damu mishipani.
Makala moja ya jarida la The Wall Street Journal la Aprili 8, 2013, ilisema: “Kwa miaka mingi wagonjwa wanaokataa matumizi ya damu kwa sababu ya imani yao wamekuwa wakifanyiwa upasuaji bila damu. Sasa, hospitali nyingi zinatumia zaidi njia hiyo ya upasuaji . . . Madaktari wapasuaji wanaounga mkono upasuaji bila damu wanasema kwamba njia hiyo inapunguza hatari ya kupata maambukizi yanayotokana na kutiwa damu mishipani pamoja na matatizo mengine yanayoweza kumfanya mgonjwa akae muda mrefu hospitalini. Pia njia hiyo inapunguza gharama za kununua damu, kuihifadhi, kuigawanya katika visehemu vyake mbalimbali, kuipima, na kuitia katika mishipa ya wagonjwa.”
Haishangazi kwamba, Bw. Robert Lorenz, msimamizi wa kitengo cha damu katika Kituo cha Afya cha Cleveland, anasema hivi: “Unapomtia mgonjwa damu mishipani unahisi umemsaidia sana wakati huo . . . Lakini, takwimu za muda mrefu zimeonyesha kwamba huo si ukweli wa mambo.”
^ fu. 5 Ili kujifunza maoni ya Mashahidi wa Yehova kuhusu damu, ona makala “Maswali Yanayoulizwa Mara Nyingi—Kwa Nini Mnakataa Kutiwa Damu Mishipani?”