Hamia kwenye habari

MSAADA KWA AJILI YA FAMILIA

Kuzungumza na Watoto Kuhusu Kileo

Kuzungumza na Watoto Kuhusu Kileo

 “Mara ya kwanza tulipozungumza na binti yetu kuhusu kileo, alikuwa na umri wa miaka sita. Tulishangaa kugundua kwamba alijua mengi kuliko tulivyotarajia.”​—Alexander.

 Unachopaswa kujua

 Kuzungumza na watoto kuhusu kileo ni muhimu. Usingoje hadi mtoto wako afikie umri wa utineja. Khamit anayeishi Urusi anasema hivi: “Afadhali tungalizungumza mapema na mwana wetu kuhusu matumizi yanayofaa ya kileo. Nilitambua umuhimu wa kufanya hivyo ilipokuwa kuchelewa mno. Niligundua kwamba mwanangu alikuwa akinywa kwa ukawaida alipokuwa na umri wa miaka 13.”

 Kwa nini jambo hilo likuhangaishe?

  •   Mtoto wako anaweza kuathiriwa na wanafunzi wenzake, matangazo ya biashara, na Televisheni, na hivyo kuwa na maoni yasiyofaa kuhusu kileo.

  •   Kulingana na Vituo vya Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukiza vya Marekani, asilimia 11 ya watu wanaokunywa kileo nchini Marekani ni vijana ambao hawajafikisha umri unaoruhusiwa na sheria.

 Haishangazi kwamba maofisa wa afya wanapendekeza wazazi wawaelimishe watoto wao tangu wanapokuwa wachanga kuhusu hatari za kileo. Unawezaje kufanya hivyo?

 Unachoweza kufanya

 Fikiria mapema maswali ambayo mtoto wako anaweza kuuliza. Watoto ni wadadisi, na watoto wakubwa ni wadadisi hata zaidi. Hivyo, ni vema utayarishe jinsi utakavyojibu. Kwa mfano:

  •   Ikiwa mtoto wako angependa kujua ladha ya kileo, unaweza kumwambia kwamba divai ni kama maji ya matunda yenye uchachu na bia ni chungu.

  •   Ikiwa mtoto wako anataka kuonja kileo, unaweza kumwambia miili ya watoto haiwezi kuhimili kileo. Taja matokeo ya kunywa: Kileo kinaweza kumfanya mtu ahisi ametulia, lakini akinywa sana anaweza kuhisi kizunguzungu, kutenda kipumbavu, au kusema na kufanya mambo ambayo atajutia.​—Methali 23:29-​35.

 Jielimishe. Biblia inasema hivi: “Mtu mwerevu hutenda kwa ujuzi.” (Methali 13:16) Tafuta habari kuhusu matumizi ya kileo, sheria, na viwango vinavyoruhusiwa katika nchi yenu. Utakuwa umejiandaa vizuri kumsaidia mtoto wako.

 Chukua hatua ya kwanza kuzungumzia jambo hilo. Mark, ambaye ni baba nchini Uingereza anasema: “Watoto wanaweza kuchanganyikiwa wanapofikiria suala la kileo. Nilimuuliza mwana wangu mwenye umri wa miaka minane ikiwa alifikiri ni sawa au si sawa kunywa kileo. Niliandaa mazingira matulivu, na hilo lilimsaidia kueleza maoni yake waziwazi.”

 Utamsaidia zaidi ukizungumzia suala hilo mara kadhaa. Ikitegemea umri wa mtoto tia ndani mazungumzo kuhusu kileo pamoja na masuala mengine maishani, kama usalama barabarani na elimu ya ngono.

 Weka kielelezo kinachofaa. Watoto ni kama sifongo, wanafyonza kila kitu kwenye mazingira, na utafiti unaonyesha kwamba wazazi ndio walio na uvutano mkubwa zaidi kwa watoto wao. Hiyo inamaanisha kwamba ikiwa kileo ndiyo njia yako ya msingi ya kutulia au kupunguza mkazo, mtoto wako ataelewa kwamba kileo ndiyo njia ya kuondoa mahangaiko maishani. Basi weka mfano mzuri wa kuigwa. Hakikisha kwamba unatumia kileo kwa hekima.

Watoto wako watajifunza kuhusu kileo kutokana na mfano wako