Pasaka Ni Nini?
Jibu la Biblia
Pasaka ni sherehe ya Kiyahudi iliyowakumbusha jinsi Mungu alivyowakomboa Waisraeli kutoka katika utumwa wa Misri mwaka wa 1513 K.W.K. Mungu aliwaagiza Waisraeli wakumbuke tukio hilo muhimu kila mwaka katika siku ya 14 ya mwezi wa Kiyahudi, Abibu, ambao baadaye uliitwa Nisani.—Kutoka 12:42; Mambo ya Walawi 23:5.
Kwa nini iliitwa Pasaka?
Neno “Pasaka” linarejelea kipindi ambacho Mungu aliwalinda Waisraeli kutokana na lile pigo kubwa la kuuawa kwa kila mzaliwa wa kwanza wa Misri. (Kutoka 12:27; 13:15) Kabla ya Mungu kuanza kutekeleza pigo hilo kubwa, aliwaambia Waisraeli wapake damu ya mwanakondoo au mbuzi kwenye milango yao. (Kutoka 12:21, 22, maelezo ya chini) Mungu angeona ishara hiyo na “kupita juu” ya nyumba zao na hivyo wazaliwa wao wa kwanza wangeokoka.—Kutoka 12:7, 13.
Pasaka ilisherehekewa jinsi gani katika nyakati za Biblia?
Mungu aliwapa Waisraeli maagizo ya jinsi ya kusherehekea Pasaka yao ya kwanza. a Yafuatayo ni baadhi ya mambo yanayotajwa katika Biblia kuhusu Pasaka:
Dhabihu: Siku ya kumi ya mwezi wa Abibu (Nisani), familia zilichagua mwanakondoo (au mbuzi) wa mwaka moja, kisha walimchinja katika siku ya 14. Katika Pasaka ya kwanza, Wayahudi walinyunyiza damu kwenye miimo ya milango na kwenye kizingiti cha juu cha mlango, wakaichoma ile nyama yote, kisha wakala.—Kutoka 12:3-9.
Chakula: Mbali na mwanakondoo (au mbuzi), Waisraeli walikula mkate usiotiwa chachu na mboga chungu za majani kama mlo wa Pasaka.—Kutoka 12:8.
Sherehe: Waisraeli walisherehekea Sherehe ya Mikate Isiyo na Chachu kwa siku saba baada ya Pasaka. Katika kipindi hicho hawakupaswa kula mkate wenye chachu.—Kutoka 12:17-20; 2 Mambo ya Nyakati 30:21.
Elimu: Wazazi walitumia pindi hiyo ya Pasaka kuwafundisha watoto wao kumhusu Yehova Mungu.—Kutoka 12:25-27.
Safari: Baadaye, Waisraeli walisafiri mpaka Yerusalemu ili kusherehekea Pasaka.—Kumbukumbu la Torati 16:5-7; Luka 2:41.
Desturi nyingine: Katika siku za Yesu, divai na kuimba kulikuwa sehemu ya sherehe ya Pasaka.—Mathayo 26:19, 30; Luka 22:15-18.
Maoni yasiyo sahihi kuhusu Pasaka
Maoni yasiyo sahihi: Waisraeli walikula mlo wa Pasaka Nisani 15.
Ukweli: Mungu aliwaagiza Waisraeli wamchinje mwanakondoo dume siku ya Nisani 14 baada ya jua kutua na wamle usiku huohuo. (Kutoka 12:6, 8) Waisraeli walipima siku kuanzia jua lilipotua hadi jua lilipotua siku iliyofuata. (Mambo ya Walawi 23:32) Hivyo, Waisraeli walimchinja mwanakondoo dume huyo na kumla mwanzoni mwa siku ya Nisani 14.
Maoni yasiyo sahihi: Wakristo wanapaswa kusherehekea Pasaka.
Ukweli: Baada ya Yesu kusherehekea Pasaka katika Nisani 14, 33 W.K., alianzisha mwadhimisho mpya: Mlo wa Jioni wa Bwana. (Luka 22:19, 20; 1 Wakorintho 11:20) Mlo huo ulichukua mahali pa Pasaka, kwa kuwa unaadhimisha dhabihu ya “Kristo mwanakondoo . . . wa Pasaka.” (1 Wakorintho 5:7) Dhabihu ya fidia ya Yesu ni kuu kuliko dhabihu ya Pasaka kwa sababu kupitia fidia ya Yesu watu wote wanaachiliwa huru kutokana na utumwa wa dhambi na kifo.—Mathayo 20:28; Waebrania 9:15.
a Hata hivyo, kadiri muda ulivyopita mabadiliko fulani yalihitajika. Kwa mfano, Waisraeli walisherehekea Pasaka ya kwanza “haraka” kwa sababu walihitaji kuwa tayari kuondoka Misri. (Kutoka 12:11) Hata hivyo, walipofika katika Nchi ya Ahadi, hawakuhitaji tena kuisherehekea kwa haraka.