JE, NI KAZI YA UBUNI?
Kiota cha Ndege Anayeitwa Mallee
Ndege anayeitwa Mallee anapatikana kusini mwa Australia, naye hudumisha hali ya joto ya kiota chake ikiwa nyuzi 34 Selsiasi hivi. Ndege huyo hudumishaje kiwango hicho cha joto mchana na usiku mwaka mzima?
Katika majira ya baridi kali, ndege hao huchimba shimo kubwa lenye kina cha mita moja hivi na upana wa karibu mita tatu, kisha ndege wa kiume hulijaza shimo hilo nyasi na majani. Mvua za mwisho mwisho za majira ya baridi kali huyalowesha majani hayo. Baada ya hapo, ndege huyo huchimba shimo dogo humo ambalo wataweka mayai kisha analifukia kwa mchanga. Muda si muda, majani hayo yanaanza kuoza na yanatokeza joto ambalo litasaidia mayai kuanguliwa.
Ndege jike anapotaka kutaga yai, ndege wa kiume hufukua mchanga ili yai litagwe karibu na mayai mengine yaliyokuwa yamefukiwa. Na baada tu ya yai kutagwa anafukia tena shimo hilo. Ndege jike anaweza kutaga hadi mayai 35 kati ya miezi ya Septemba na Februari. a
Mara kwa mara, ndege hao huingiza mdomo wao kwenye mchanga ili kupima joto lililo ndani ya kiota. Kisha wanafanya mabadiliko yanayohitajika ikitegemea majira. Kwa mfano:
Katika majira ya kuchipua, majani yale yanapoanza kuoza, joto lililo kwenye kiota linakuwa jingi sana, kwa hiyo, ndege wa kiume anaondoa mchanga ulio juu ya mayai ili kupunguza joto. Baadaye, anafukia kiota hicho tena kwa mchanga uliopoa.
Katika majira ya joto, ndege wa kiume huongeza mchanga kwenye kiota ili mayai yasiathiriwe na joto la jua. Kila asubuhi, anapunguza mchanga na kisha kuurudisha baada ya kiota na mchanga wenyewe kupoa.
Katika majira ya kupukutika, baada ya majani yote kuoza, ndege wa kiume anaondoa mchanga karibia wote ili joto la jua lifikie mayai na mchanga ambao ametoa. Baadaye, anafukia kiota hicho kwa mchanga ambao umepata joto la jua na hivyo kiota kinapata joto usiku.
Kwa wastani, kila siku ndege wa kiume hutumia zaidi ya saa tano kufukua na kufukia zaidi ya kilogramu 850 za mchanga. Kuhamisha-hamisha mchanga huo kuna faida nyingine: Kunafanya udongo uwe laini na hilo linawawezesha vifaranga kutoka kwenye kiota baada ya kutotolewa.
Tazama Mallee wakiondoa mchanga kwenye kiota chao
Una maoni gani? Je, uwezo wa ndege anayeitwa Mallee wa kudhibiti joto kwenye kiota chake ulijitokeza wenyewe? Au je, ulibuniwa?
a Mayai yanaanguliwa baada ya majuma saba au nane na hilo linamaanisha kazi ya kudumisha kiota inaendelea kufanywa hadi Aprili.