JE, NI KAZI YA UBUNI?
Muundo wa Meno ya Koanata
Koanata ni konokono wa kawaida wa majini aliye na kombe lenye umbo la pia, lakini ana meno yenye nguvu isivyo kawaida. Meno hayo yametengenezwa kwa nyuzinyuzi zilizoshikamana sana za madini fulani yanayoitwa goethite yaliyofumwa ndani ya nyuzi za protini.
Fikiria hili: Koanata ana mpangilio wa meno madogo-madogo, unaofanana na ulimi. Meno hayo yamejikunja na yamepangwa kwa mistari, na kila jino lina urefu unaokaribia milimita moja, na ni lenye ncha kali. Kila jino linahitaji kuwa gumu na imara sana ili koanata aweze kukwangua miani kutoka kwenye mawe anapokula.
Wachunguzi walitumia darubini inayotumia nguvu ya atomu ili kupima ikiwa meno hayo yatavunjika baada ya kuvutwa kwa nguvu kubwa. Waligundua kwamba meno ya koanata yana uwezo mkubwa sana kuhimili uvutano mkubwa kuliko ule wa viumbe vingine ambavyo vimewahi kufanyiwa uchunguzi. Yana nguvu hata kuliko utando wa buibui. Mchunguzi aliyeongoza katika utafiti huo alisema: “Tunapaswa kuanza kufikiria kuhusu uwezekano wa kutengeneza vifaa vyetu kwa kutegemea muundo huohuo.”
Wachunguzi wanaamini kwamba vitu vilivyobuniwa kwa kutegemea muundo wa meno ya koanata vinaweza kutumiwa kutengeneza magari, mashua, na ndege na hata kurekebisha meno.
Una maoni gani? Je, muundo wenye kustaajabisha wa meno ya koanata ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?