Hamia kwenye habari

Moment/Robert D. Barnes via Getty Images

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Ulimi wa Ndege Mvumaji

Ulimi wa Ndege Mvumaji

 Wakati fulani wanasayansi walifikiri ulimi wa ndege mvumaji ulifyonza nekta kwa kutumia nguvu za asili zinazopitisha umajimaji kupitia mirija myembamba. Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa baadaye umeonyesha kwamba ndege huyo hutumia mbinu bora zaidi.

 Fikiria hili: Ulimi wa ndege mvumaji unapoingia kwenye nekta, ulimi huo hugawanyika mara mbili na kufanyiza ncha mbili. Kuna aina fulani ya mirija inayoanzia kwenye ncha zote mbili kwenda hadi ndani ya ulimi wake. Kwa hiyo, ncha zake zinapoingia kwenye nekta, mirija hiyo hufunguka, na ncha za ulimi hutanuka kabisa na kumwezesha ndege huyo kunywa nekta kwa kulamba badala ya kufyonza kupitia mirija yake. Anaporudisha ulimi kinywani, ncha hizo mbili hujifunga na nekta inabaki ndani yake.

 Watafiti Alejandro Rico-Guevara, Tai-Hsi Fan, na Margaret Rubega wanasema kwamba mchakato wote huo huchukua “chini ya sehemu moja kati ya kumi ya sekunde.” Pia wanasema hivi: “Ncha ya ulimi wake ni kifaa cha kunasa umajimaji kinachobadilika . . . umbo kwa njia ya ajabu kinapoingia na kutoka ndani ya vimiminika.”

 Mbali na hilo, ndege huyo mdogo sana hatumii nishati yoyote kufanya hivyo. Ncha za ulimi wake zinapoingia na kutoka ndani ya umajimaji, zinafunguka na kufunga kwa kutegemea msukumo tata sana unaozitendesha.

 Kwa kuwa ulimi wa ndege mvumaji ni kifaa bora sana cha kunasa umajimaji, watafiti wanaamini kwamba wanaweza kutumia mambo wanayojifunza kubuni vitu katika nyanja za matibabu, kutengeneza roboti, na nyanja nyingine. Huenda pia elimu hiyo ikawasaidia kutengeneza vifaa vya kusafisha umajimaji au mafuta yanayomwagika baharini.

 Ulimi wa Ndege Mvumaji

 Una maoni gani? Je, ulimi tata wa ndege mvumaji ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?