Kitabu cha Pili cha Wafalme 7:1-20

  • Elisha atabiri mwisho wa njaa kali (1, 2)

  • Chakula chapatikana katika kambi iliyoachwa ya Wasiria (3-15)

  • Unabii wa Elisha watimizwa (16-20)

7  Sasa Elisha akasema: “Sikiliza neno la Yehova. Yehova anasema hivi: ‘Kesho karibu wakati kama huu sea moja* ya unga laini itakuwa na thamani ya shekeli moja, na sea mbili za shayiri zitakuwa na thamani ya shekeli moja* katika lango la* Samaria.’”+  Ndipo kamanda msaidizi ambaye mfalme alimtegemea akamwambia hivi mtu wa Mungu wa kweli: “Hata Yehova akiyafungua malango ya mbinguni ya mafuriko, je, kweli jambo hilo linaweza kutokea?”*+ Ndipo Elisha akamwambia, “Utaona kwa macho yako mwenyewe,+ lakini hutakula vyakula hivyo.”+  Kulikuwa na watu wanne wenye ukoma kwenye lango la jiji,+ nao wakaambiana: “Kwa nini tuketi hapa mpaka tufe?  Tukisema, ‘Acheni tuingie jijini,’ na bado kuna njaa kali jijini,+ tutafia humo. Nasi tukiketi hapa, bado tutakufa. Basi sasa twende zetu kwenye kambi ya Wasiria. Wakituruhusu tuishi, tutaishi; lakini wakituua, basi tutakufa.”  Kwa hiyo wakaondoka jioni giza lilipoanza kuingia, wakaingia kwenye kambi ya Wasiria. Walipofika kandokando ya kambi ya Wasiria, hakukuwa na mtu yeyote.  Kwa maana Yehova alikuwa amesababisha kambi ya Wasiria isikie sauti ya magari ya vita na farasi, sauti ya jeshi kubwa.+ Basi wakaambiana: “Tazama! Mfalme wa Israeli amekodi wafalme wa Wahiti na wafalme wa Misri watushambulie!”  Mara moja wakaondoka na kukimbia katika giza la jioni, wakaacha mahema yao, farasi wao, punda wao, na kambi yote kama ilivyokuwa, wakakimbia ili kuokoa maisha yao.*  Watu hao wenye ukoma walipokaribia kambi hiyo, wakaingia ndani ya hema moja na kuanza kula na kunywa. Wakachukua fedha, dhahabu, na mavazi kutoka humo, wakaenda na kuficha vitu hivyo. Kisha wakarudi na kuingia katika hema lingine, wakachukua vitu kutoka humo na kwenda kuvificha.  Mwishowe wakaambiana: “Jambo tunalofanya si sawa. Leo ni siku ya habari njema! Tukisitasita na kusubiri mpaka mapambazuko, tutastahili kuadhibiwa. Twendeni sasa tukaiambie nyumba ya mfalme habari hizi.” 10  Basi wakaenda na kuwaita kwa sauti walinzi wa malango ya jiji na kuwaambia: “Tulienda kwenye kambi ya Wasiria, lakini hakukuwa na mtu yeyote huko—hatukusikia sauti ya yeyote. Kulikuwa tu na farasi na punda waliofungwa na mahema yaliyoachwa kama yalivyokuwa.” 11  Mara moja walinzi hao wa malango wakatangaza habari hizo, nazo zikafika nyumbani kwa mfalme. 12  Mara moja mfalme akaamka usiku na kuwaambia watumishi wake: “Acheni niwaambie yale ambayo Wasiria wametutendea. Wanajua kwamba tuna njaa,+ kwa hiyo walitoka kambini na kujificha shambani, wakisema, ‘Watatoka jijini, nasi tutawakamata wakiwa hai na kuingia jijini.’”+ 13  Ndipo mmoja wa watumishi wake akasema: “Tafadhali, waruhusu baadhi ya wanaume wachukue farasi watano kati ya wale waliobaki jijini. Hali itakayowapata itakuwa sawa na hali itakayoupata umati wa Waisraeli unaobaki hapa. Hali yao itakuwa sawa na ya umati wa Waisraeli ambao waliangamia. Basi na tuwatume waende tuone hali itakavyokuwa.” 14  Wakachukua magari mawili pamoja na farasi, na mfalme akawatuma kwenye kambi ya Wasiria na kuwaambia: “Nendeni mwone hali ilivyo.” 15  Wakawafuata mpaka Yordani, na mavazi na vyombo ambavyo Wasiria walikuwa wametupa walipokuwa wakikimbia kwa hofu vilikuwa vimetapakaa njia yote. Kisha wajumbe hao wakarudi na kumletea mfalme habari. 16  Ndipo watu wakatoka na kuipora kambi ya Wasiria, hivi kwamba sea moja ya unga laini ikawa na thamani ya shekeli moja, na sea mbili ya shayiri ikawa na thamani ya shekeli moja, kulingana na neno la Yehova.+ 17  Mfalme alimweka yule kamanda msaidizi awe msimamizi wa lango, kamanda ambaye mfalme alimtegemea, lakini watu wakamkanyaga-kanyaga langoni hadi akafa, kama yule mtu wa Mungu wa kweli alivyokuwa amemwambia mfalme alipokwenda kumwona. 18  Ilitendeka kama mtu wa Mungu wa kweli alivyokuwa amemwambia mfalme: “Kesho wakati kama huu, sea mbili za shayiri zitakuwa na thamani ya shekeli moja, na sea moja ya unga laini itakuwa na thamani ya shekeli moja katika lango la Samaria.”+ 19  Lakini yule kamanda msaidizi alikuwa amemwambia mtu wa Mungu wa kweli: “Hata Yehova akiyafungua malango ya mbinguni ya mafuriko, je, kweli jambo hilo linaweza kutokea?”* Elisha akamjibu: “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini hutakula vyakula hivyo.” 20  Hivyo ndivyo ilivyotokea kwake, kwa maana watu walimkanyaga-kanyaga langoni hadi akafa.

Maelezo ya Chini

Sea moja ilikuwa sawa na lita 7.33 (vibaba 6.66). Angalia Nyongeza B14.
Shekeli moja ilikuwa na uzito wa gramu 11.4. Angalia Nyongeza B14.
Au “masoko ya.”
Tnn., “kweli neno hilo linaweza kutimia?”
Au “nafsi zao.”
Tnn., “kweli neno hilo linaweza kutimia?”