Ayubu 3:1-26

  • Ayubu ajuta kuzaliwa (1-26)

    • Auliza kwa nini anateseka (20, 21)

3  Baada ya hayo Ayubu alianza kuongea na kuilaani siku aliyozaliwa.*+  Ayubu akasema:   “Na itokomee siku niliyozaliwa,+Pia usiku ambao mtu alisema: ‘Mimba iliyotungwa ni ya mwanamume!’   Siku hiyo na iwe giza. Mungu aliye juu asiihangaikie siku hiyo;Na nuru isiiangazie.   Na imilikiwe na giza zito sana.* Wingu la mvua na litande juu yake. Na chochote kinacholeta giza mchana kiitie hofu siku hiyo.   Usiku huo—na ushikwe na giza;+Na isishangilie miongoni mwa siku nyingine za mwaka,Nayo isihesabiwe miongoni mwa siku za miezi.   Kwa kweli! Usiku huo na uwe tasa;Kelele za shangwe zisisikiwe usiku huo.   Wale wanaolaani siku na wailaani,Wale wanaoweza kumwamsha Lewiathani.*+   Nyota zake za alfajiri na ziwe giza;Usiku huo ungojee nuru bila mafanikio,Nao usione miale ya mapambazuko. 10  Kwa maana haukufunga milango ya tumbo la uzazi la mama yangu;+Wala haukuficha taabu kutoka machoni pangu. 11  Kwa nini sikufa nilipozaliwa? Kwa nini sikuangamia nilipotoka tumboni?+ 12  Kwa nini mama yangu alinipakata mapajaniNa kuninyonyesha? 13  Kwa maana sasa ningekuwa nimelala chini bila usumbufu;+Ningekuwa nimelala na kupumzika+ 14  Pamoja na wafalme wa dunia na washauri wao,Waliojijengea majengo ambayo sasa ni magofu,* 15  Au pamoja na wakuu waliomiliki dhahabu,Ambao nyumba zao zilijaa fedha. 16  Au kwa nini sikuwa kama mimba iliyoharibika ambayo imefichika,Kama watoto ambao hawajawahi kamwe kuona nuru? 17  Katika kifo hata waovu hawasumbui tena;Na humo waliochoka hupumzika.+ 18  Humo wafungwa hukaa pamoja kwa utulivu;Hawasikii sauti ya mtu anayewalazimisha kufanya kazi. 19  Humo wadogo ni sawa na wakubwa,+Na humo mtumwa yuko huru kutoka kwa bwana wake. 20  Kwa nini anampa nuru anayetesekaNa kuwapa uhai wale wanaoteseka kwa uchungu mwingi?*+ 21  Kwa nini wanatamani sana kifo, lakini hakiji?+ Wanachimba wakikitafuta kuliko hazina zilizofichika, 22  Wale wanaoshangilia sana,Wanaofurahi wanapopata kaburi. 23  Kwa nini anampa nuru mwanamume aliyepotea njia,Ambaye Mungu amemzingira kwa ukuta?+ 24  Kwa maana badala ya chakula changu majonzi hunijia,+Na kilio changu cha uchungu+ humwagika kama maji. 25  Kwa maana ninachoogopa sana kimenijia,Na ninachohofu kimenipata. 26  Sijawa na amani, wala utulivu, wala sijapumzika,Lakini taabu inaendelea kuniandama.”

Maelezo ya Chini

Tnn., “kuilaani siku yake.”
Au “giza na kivuli cha kifo.”
Inaeleweka kwamba maneno haya yanamrejelea mamba au mnyama mwingine mkubwa mwenye nguvu anayekaa ndani ya maji.
Au labda, “Waliojijengea mahali palipo ukiwa.”
Au “wale walio na uchungu nafsini.”