Esta 7:1-10

  • Esta afunua uovu wa Hamani (1-6a)

  • Hamani atundikwa kwenye mti alioutengeneza (6b-10)

7  Basi mfalme na Hamani+ wakaja kwenye karamu ya Malkia Esta.  Mfalme akamuuliza tena Esta siku ya pili wakati wa karamu ya divai: “Malkia Esta, una ombi gani? Utapewa unachoomba. Unataka nini? Hata ukiomba nusu ya ufalme wangu utapewa!”+  Malkia Esta akajibu: “Ikiwa nimepata kibali chako, Ee mfalme, nawe mfalme ukipenda, naomba uuokoe uhai wangu,* na pia uhai wa watu wangu.+  Kwa maana tumeuzwa,+ mimi na watu wangu, tuangamizwe, tuuawe, na kufutiliwa mbali.+ Kama tungeuzwa tuwe watumwa wa kiume na wa kike, ningekaa kimya. Lakini msiba huu haufai, kwa sababu utamletea mfalme hasara.”  Ndipo mfalme Ahasuero akamuuliza Malkia Esta: “Ni nani huyo, na yuko wapi mwanamume aliyethubutu kufanya jambo hilo?”  Esta akasema: “Mpinzani na adui ni huyu Hamani mwovu.” Hamani akaogopa sana kwa sababu ya mfalme na malkia.  Mfalme akasimama kwa hasira na kutoka kwenye karamu ya divai, akaenda kwenye bustani ya jumba la mfalme, lakini Hamani akasimama ili kumsihi Malkia Esta auokoe uhai wake,* kwa maana alijua mfalme alikuwa ameazimia kumwadhibu.  Mfalme aliporudi kutoka kwenye bustani ya jumba la mfalme na kuingia katika nyumba ya karamu ya divai na kumwona Hamani akiwa amejiangusha kwenye kochi, mahali alipokuwa Esta. Mfalme akasema: “Je, sasa anataka kumbaka malkia katika nyumba yangu mwenyewe?” Mara tu maneno hayo yalipotoka kinywani mwa mfalme, wakaufunika uso wa Hamani.  Harbona,+ mmoja wa maofisa wa makao ya mfalme akasema: “Pia Hamani alitengeneza mti kwa ajili ya Mordekai+ aliyetoa habari iliyomwokoa mfalme.+ Mti huo wenye kimo cha mikono 50* umesimamishwa nyumbani kwa Hamani.” Ndipo mfalme akasema: “Mtundikeni juu yake.” 10  Basi wakamtundika Hamani kwenye mti aliokuwa ameutengeneza ili kumtundika Mordekai juu yake, na hasira ya mfalme ikatulia.

Maelezo ya Chini

Au “nafsi yangu.”
Au “nafsi yake.”
Karibu mita 22.3 (futi 73). Angalia Nyongeza B14.