Mambo ya Walawi 12:1-8
-
Kutakaswa kwa mwanamke baada ya kuzaa mtoto (1-8)
12 Yehova akaendelea kumwambia Musa:
2 “Waambie Waisraeli, ‘Mwanamke akipata mimba na kuzaa mtoto wa kiume, mwanamke huyo hatakuwa safi kwa siku saba, atakuwa kama anavyokuwa katika siku zake za hedhi.+
3 Siku ya nane, mtoto huyo atatahiriwa.+
4 Kisha kwa siku 33 mwanamke huyo ataendelea kujitakasa kwa sababu ya damu aliyopoteza. Asiguse kitu chochote kitakatifu, wala asiingie mahali patakatifu mpaka atakapokamilisha siku zake za kujitakasa.
5 “Akizaa mtoto wa kike, mwanamke huyo hatakuwa safi kwa siku 14, atakuwa kama anavyokuwa katika siku zake za hedhi. Kisha ataendelea kujitakasa kwa siku 66 kwa sababu ya damu aliyopoteza.
6 Siku zake za kujitakasa zitakapokwisha baada ya kuzaa mtoto wa kiume au wa kike, atamletea kuhani mwanakondoo dume wa mwaka mmoja kwa ajili ya dhabihu ya kuteketezwa+ na hua mchanga au njiwa tetere kwa ajili ya dhabihu ya dhambi kwenye mlango wa hema la mkutano.
7 Kuhani atatoa dhabihu hizo mbele za Yehova ili kufunika dhambi ya mwanamke huyo, kisha atakuwa safi kutokana na damu yake. Hiyo ndiyo sheria kuhusu mwanamke anayezaa mtoto wa kiume au wa kike.
8 Lakini ikiwa hawezi kuleta kondoo, basi anapaswa kuleta njiwa tetere wawili au hua wawili wachanga,+ mmoja kwa ajili ya dhabihu ya kuteketezwa na wa pili kwa ajili ya dhabihu ya dhambi, naye kuhani atamtolea dhabihu hizo ili kufunika dhambi yake, kisha atakuwa safi.’”