Mwanzo 38:1-30
-
Yuda na Tamari (1-30)
38 Karibu wakati huo, Yuda aliwaacha ndugu zake na kupiga hema lake karibu na mwanamume Mwadulamu aliyeitwa Hira.
2 Akiwa huko, Yuda akamwona binti ya Mkanaani fulani+ aliyeitwa Shua. Basi akamwoa na kulala naye,
3 akapata mimba. Baadaye akazaa mwana, akampa jina Eri.+
4 Akapata mimba tena, akazaa mwana na kumpa jina Onani.
5 Kwa mara nyingine tena akazaa mwana na kumpa jina Shela. Shela alipozaliwa, Yuda alikuwa Akzibu.+
6 Baada ya muda, Yuda akamtafutia Eri mzaliwa wake wa kwanza mke aliyeitwa Tamari.+
7 Lakini Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alimchukiza Yehova; kwa hiyo Yehova akamuua.
8 Kwa hiyo, Yuda akamwambia Onani: “Lala na mke wa ndugu yako na ufunge naye ndoa ya ndugu mkwe, umpe ndugu yako mzao.”+
9 Lakini Onani alijua kwamba mzao huyo hangehesabiwa kuwa wake.+ Kwa hiyo alipolala na mke wa ndugu yake, alimwaga shahawa zake ardhini ili asimpe ndugu yake mzao.+
10 Jambo alilofanya lilikuwa ovu machoni pa Yehova, kwa hiyo akamuua pia.+
11 Yuda akamwambia Tamari binti mkwe wake: “Ishi ukiwa mjane katika nyumba ya baba yako mpaka Shela mwanangu atakapokua,” kwa maana Yuda alisema moyoni mwake: ‘Huenda yeye pia akafa kama ndugu zake.’+ Basi Tamari akaenda kuishi katika nyumba ya baba yake.
12 Muda fulani ukapita, na mke wa Yuda, aliyekuwa binti ya Shua,+ akafa. Yuda alizingatia kipindi cha maombolezo, kisha akaenda Timna+ kwa watumishi wake waliokata kondoo manyoya akiwa pamoja na rafiki yake, Hira, Mwadulamu.+
13 Tamari akaambiwa: “Baba mkwe wako anapanda kwenda Timna kuwakata kondoo wake manyoya.”
14 Ndipo akayavua mavazi yake ya ujane, akajifunika uso kwa shela na kujifunika mabegani kwa mtandio, akaketi chini kwenye lango la kuingia Enaimu, jiji lililo katika barabara inayokwenda Timna, kwa sababu aliona kwamba Shela amekuwa mtu mzima lakini hajaruhusiwa amwoe.+
15 Yuda alipomwona, mara moja alifikiri yeye ni kahaba, kwa sababu alikuwa ameufunika uso wake.
16 Kwa hiyo, akamkaribia kando ya barabara na kumwambia: “Niruhusu tafadhali nilale nawe,” kwa maana hakujua kwamba alikuwa binti mkwe wake.+ Hata hivyo, Tamari akamuuliza: “Utanipa nini ili ulale nami?”
17 Akamjibu: “Nitakutumia mwanambuzi kutoka katika kundi langu.” Lakini akamuuliza: “Je, utanipa rehani kabla hujamleta?”
18 Yuda akamuuliza: “Ungependa nikupe nini kama rehani?” akasema: “Pete yako ya muhuri+ na kamba yako na fimbo uliyoshika mkononi.” Basi akampa vitu hivyo na kulala naye, Tamari akapata mimba.
19 Baada ya hayo Tamari akainuka na kwenda zake, akavua mtandio aliojifunika na kuvaa mavazi yake ya ujane.
20 Basi Yuda akamtuma rafiki yake Mwadulamu+ ampelekee mwanamke huyo mwanambuzi ili amrudishie vitu alivyompa kama rehani, lakini hakumpata kamwe.
21 Akawauliza watu wa jiji hilo: “Yuko wapi yule kahaba wa hekaluni anayekaa kando ya barabara hapa Enaimu?” Lakini wakamjibu: “Hatujawahi kumwona kahaba yeyote wa hekaluni mahali hapa.”
22 Mwishowe akarudi kwa Yuda na kumwambia: “Sikumpata, na isitoshe watu wa jiji hilo waliniambia, ‘Hatujawahi kumwona kahaba yeyote wa hekaluni mahali hapa.’”
23 Basi Yuda akasema: “Mwache avichukue vitu hivyo, tusije tukadharauliwa. Usijali, nilikutuma umpelekee mwanambuzi huyu, lakini hukumpata.”
24 Hata hivyo, baada ya miezi mitatu hivi, Yuda aliambiwa: “Tamari binti mkwe wako amefanya ukahaba, na pia amepata mimba kwa sababu ya ukahaba wake.” Yuda akasema: “Mtoeni nje achomwe moto.”+
25 Alipokuwa akitolewa nje, akatuma ujumbe huu kwa baba mkwe wake: “Mwenye vitu hivi ndiye aliyenipa mimba.” Kisha akasema: “Tafadhali chunguza vitu hivi ni vya nani, yaani, pete hii ya muhuri na kamba na fimbo hii.”+
26 Basi Yuda akavichunguza na kusema: “Yeye ni mwadilifu kuliko mimi, kwa sababu sikumruhusu Shela mwanangu amwoe.”+ Yuda hakufanya ngono naye tena baada ya hayo.
27 Wakati ulipofika wa Tamari kuzaa, mapacha walikuwa tumboni mwake.
28 Alipokuwa akizaa, mtoto mmoja alitoa mkono wake nje, na mara moja mkunga akachukua uzi mwekundu na kuufunga mkono huo, akisema: “Huyu alitoka kwanza.”
29 Lakini mara tu alipourudisha mkono wake, ndugu yake akatoka, mkunga akasema kwa mshangao: “Lo! Umejipasulia njia!” Basi akapewa jina Perezi.*+
30 Kisha ndugu yake aliyefungwa uzi mwekundu mkononi akatoka, akapewa jina Zera.+
Maelezo ya Chini
^ Maana yake “Mpasuko,” labda linarejelea hali ya kupasuka msamba.