Waamuzi 17:1-13
-
Sanamu za Mika na kuhani wake (1-13)
17 Kulikuwa na mtu mmoja katika eneo lenye milima la Efraimu+ aliyeitwa Mika.
2 Siku moja alimwambia hivi mama yake: “Vile vipande 1,100 vya fedha ulivyoibiwa na ukamlaani aliyekuibia, nikiwa nasikia—mimi ndiye niliyevichukua.” Mama yake akamwambia, “Yehova na akubariki mwanangu.”
3 Basi akamrudishia mama yake vile vipande 1,100 vya fedha, lakini mama yake akasema, “Nitazitakasa fedha hizi kwa ajili ya Yehova zitoke mikononi mwangu ili mwanangu azitumie kutengeneza sanamu ya kuchongwa na sanamu ya chuma.*+ Sasa nakurudishia fedha hizi.”
4 Baada ya kumrudishia mama yake fedha hizo, mama yake akachukua vipande 200 vya fedha na kumpa mfua fedha. Naye akatengeneza sanamu ya kuchongwa na sanamu ya chuma;* na sanamu hizo zikawekwa katika nyumba ya Mika.
5 Na Mika alikuwa na nyumba ya miungu, naye akatengeneza efodi*+ na sanamu za terafimu*+ na kumweka mmoja wa wanawe awe kuhani wake.+
6 Siku hizo hakukuwa na mfalme katika Israeli.+ Kila mtu alifanya jambo aliloona ni jema machoni pake.*+
7 Basi kulikuwa na kijana fulani kutoka Bethlehemu+ kule Yuda aliyetoka katika ukoo wa Yuda. Alikuwa Mlawi+ na alikuwa ameishi huko kwa muda.
8 Kijana huyo akaondoka katika jiji la Bethlehemu katika nchi ya Yuda ili atafute mahali pengine pa kuishi. Alipokuwa akisafiri, alifika katika eneo lenye milima la Efraimu, katika nyumba ya Mika.+
9 Mika akamuuliza, “Unatoka wapi?” Akamjibu, “Mimi ni Mlawi kutoka Bethlehemu kule Yuda, natafuta mahali pa kuishi.”
10 Basi Mika akamwambia, “Kaa pamoja nami, uwe kama baba* na kuhani wangu. Nitakupa vipande kumi vya fedha kwa mwaka, mavazi, na chakula.” Kwa hiyo Mlawi huyo akaingia nyumbani mwake.
11 Mlawi huyo akakubali kukaa na Mika, naye akawa kama mmoja wa wanawe.
12 Isitoshe, Mika akamweka Mlawi huyo kuwa kuhani wake,+ akaishi nyumbani mwa Mika.
13 Basi Mika akasema, “Sasa najua kwamba Yehova atanitendea mema, kwa maana Mlawi amekuwa kuhani wangu.”
Maelezo ya Chini
^ Au “sanamu ya kuyeyushwa.”
^ Au “sanamu ya kuyeyushwa.”
^ Au “miungu ya familia; sanamu.”
^ Au “kizibao cha kuhani.”
^ Au “alilofikiri linafaa.”
^ Au “mshauri.”