Waamuzi 19:1-30
-
Wabenjamini wabaka katika jiji la Gibea (1-30)
19 Katika siku hizo, wakati ambapo hakukuwa na mfalme katika Israeli,+ Mlawi fulani aliyekuwa akiishi mbali katika eneo lenye milima la Efraimu+ alimwoa suria kutoka Bethlehemu+ kule Yuda.
2 Lakini suria huyo hakuwa mwaminifu kwake, akamwacha mume wake na kurudi Bethlehemu nyumbani kwa baba yake kule Yuda. Naye akakaa huko kwa miezi minne.
3 Basi mume wake akaenda kumsihi arudi; alienda na mtumishi wake wa kiume na punda wawili. Mwanamke huyo akamkaribisha katika nyumba ya baba yake. Baba yake alifurahi kumwona.
4 Basi baba mkwe wake, yaani, baba ya yule msichana, akamshawishi akae hapo kwa siku tatu; wakala na kunywa; naye akalala huko.
5 Siku ya nne, walipoamka asubuhi na mapema ili waanze safari, baba ya yule msichana akamwambia hivi mkwe wake: “Kula chakula kidogo ili upate nguvu,* kisha uende.”
6 Basi wakaketi, na wote wawili wakala na kunywa; kisha baba ya yule msichana akamwambia huyo mwanamume, “Tafadhali, lala hapa usiku huu, ustarehe.”*
7 Mwanamume huyo alipotaka kuondoka, baba mkwe wake akamsihi sana abaki, naye akalala tena usiku huo.
8 Alipoamka asubuhi na mapema siku ya tano ili aende, baba ya msichana huyo akasema, “Tafadhali, kula chakula kidogo ili upate nguvu.”* Nao wakakaa mpaka jioni sana, na wote wawili wakaendelea kula.
9 Yule mwanamume alipotaka kuondoka pamoja na suria* wake na mtumishi wake, baba mkwe wake, yaani, baba ya yule msichana, akamwambia, “Tazama! Mchana umekwisha, jioni inakaribia. Tafadhali, lala hapa usiku huu, ustarehe. Amkeni mapema kesho na kuanza safari yenu ya kwenda nyumbani kwenu.”*
10 Hata hivyo, mwanamume huyo hakutaka kulala huko tena, basi akaondoka na kusafiri mpaka Yebusi, yaani, Yerusalemu.+ Alikuwa na punda wake wawili wenye matandiko, suria wake, na mtumishi wake.
11 Walipokaribia Yebusi, ilikuwa jioni sana. Basi yule mtumishi akamuuliza bwana wake, “Tunaweza kulala katika jiji hili la Wayebusi usiku huu?”
12 Lakini bwana wake akamjibu hivi: “Hatutalala katika jiji la watu ambao si Waisraeli. Tutaendelea na safari mpaka Gibea.”+
13 Kisha akamwambia hivi mtumishi wake: “Twende, tujitahidi kufika Gibea au Rama; tulale katika mojawapo ya majiji hayo.”+
14 Basi wakaendelea na safari, na jua likaanza kutua walipokaribia Gibea, jiji la Wabenjamini.
15 Wakaingia Gibea ili walale humo usiku. Wakaketi katika uwanja wa jiji, lakini hakuna yeyote aliyewakaribisha ili walale nyumbani mwake usiku.+
16 Baadaye jioni hiyo, mzee fulani aliingia jijini kutoka shambani mwake. Alizaliwa katika eneo lenye milima la Efraimu,+ na kwa muda fulani alikuwa akiishi Gibea; lakini wenyeji wa jiji hilo walikuwa Wabenjamini.+
17 Alipotazama na kumwona yule msafiri katika uwanja wa jiji, mzee huyo akamuuliza, “Unaenda wapi, na umetoka wapi?”
18 Akajibu, “Tunatoka Bethlehemu kule Yuda nasi tunaenda mbali katika eneo lenye milima la Efraimu, nyumbani kwetu. Nilienda Bethlehemu katika nchi ya Yuda,+ nami ninaenda kwenye nyumba ya Yehova,* lakini sijakaribishwa na yeyote.
19 Tuna nyasi na chakula cha kutosha kwa ajili ya punda wetu,+ na pia nina mkate+ na divai kwa ajili yangu, suria* wangu, na mtumishi wangu. Hatujapungukiwa na kitu chochote.”
20 Hata hivyo, mzee huyo akasema, “Uwe na amani! Nitawapa chochote mnachohitaji. Lakini msilale hapa kwenye uwanja wa jiji.”
21 Ndipo akamkaribisha nyumbani mwake na kuwalisha* punda wake. Kisha wakanawa miguu, wakala, na kunywa.
22 Walipokuwa wakila na kunywa, wanaume fulani wahuni katika jiji hilo wakaizingira nyumba na kuugonga mlango kwa fujo, huku wakimwambia hivi mzee huyo mwenye nyumba, “Mtoe nje yule mwanamume aliyeingia nyumbani mwako, ili tufanye ngono naye.”+
23 Ndipo mwenye nyumba akatoka nje na kuwaambia, “Sivyo, ndugu zangu, msifanye uovu. Tafadhali, mtu huyu ni mgeni wangu. Msifanye jambo hili la aibu.
24 Hapa nina binti bikira na pia suria wa mwanamume huyu. Acheni niwatoe nje, ili mwatendee mambo ya aibu, ikiwa mnataka kufanya hivyo.*+ Lakini msimtendee mwanamume huyu jambo hili la aibu.”
25 Lakini wanaume hao hawakumsikiliza, basi yule mtu akamtoa nje kwa nguvu suria* wake.+ Wakambaka na kumtendea vibaya usiku kucha mpaka asubuhi. Kisha kulipopambazuka wakamwacha aende zake.
26 Asubuhi na mapema, mwanamke huyo akaja kwenye nyumba ya yule mtu alimokuwa bwana wake, akaanguka chini mlangoni, akalala hapo mpaka kulipopambazuka.
27 Bwana wake alipoamka asubuhi na kufungua milango ya nyumba ili atoke na kuendelea na safari, akamwona yule mwanamke, suria wake, akiwa amelala mlangoni, mikono yake ikiwa kwenye kizingiti.
28 Akamwambia, “Amka twende.” Lakini hakusema lolote. Kwa hiyo mwanamume huyo akamwinua na kumweka juu ya punda, wakaondoka na kuelekea nyumbani.
29 Alipofika nyumbani kwake, akachukua kisu na kuikatakata ile maiti ya suria wake vipande 12, akapeleka kipande katika kila eneo* la Israeli.
30 Wote walioona jambo hilo wakasema, “Jambo kama hili halijawahi kutokea kamwe wala kuonekana tangu Waisraeli walipotoka Misri mpaka leo. Fikirieni jambo hili,* mshauriane,+ kisha mtuambie tutakalofanya.”
Maelezo ya Chini
^ Au “ili moyo wako uendelee kuishi.”
^ Au “uchangamshe moyo wako.”
^ Au “ili moyo wako uendelee kuishi.”
^ Au “mke.”
^ Tnn., “katika hema lenu.”
^ Au labda, “ninatumikia katika nyumba ya Yehova.”
^ Au “mke.”
^ Au “na kuwapa chakula cha mifugo.”
^ Au “muwatendee vibaya kama mnavyotaka.”
^ Au “mke.”
^ Au “kabila.”
^ Tnn., “Wekeni moyo wenu juu ya jambo hili.”