Waamuzi 8:1-35

  • Waefraimu wamlalamikia Gideoni (1-3)

  • Wafalme Wamidiani wafuatiliwa na kuuawa (4-21)

  • Gideoni akataa kuwa mfalme (22-27)

  • Historia fupi ya maisha ya Gideoni (28-35)

8  Ndipo watu wa Efraimu wakamuuliza Gideoni, “Kwa nini umetutendea hivi? Kwa nini hukutuita ulipoenda kupigana na Wamidiani?”+ Nao wakamshutumu vikali.+  Lakini akawaambia, “Mimi nimefanya nini nikilinganishwa nanyi? Je, masalio ya Efraimu+ si bora kuliko mavuno ya zabibu ya Abiezeri?+  Mungu aliwatia mikononi mwenu Orebu na Zeebu,+ wakuu wa Midiani, lakini mimi nimefanya nini nikilinganishwa nanyi?” Gideoni aliposema hivyo* hasira yao ikapoa.*  Gideoni na wale wanaume 300 waliokuwa pamoja naye wakafika Yordani na kuvuka. Ingawa walikuwa wamechoka, waliendelea kuwafuatia maadui wao.  Akawaambia watu wa Sukothi, “Tafadhali wapeni mikate watu walio pamoja nami, kwa kuwa wamechoka nami ninawafuatia Zeba na Zalmuna, wafalme wa Midiani.”  Lakini wakuu wa Sukothi wakamwambia, “Je, tayari umewakamata Zeba na Zalmuna ili tuwape wanajeshi wako mikate?”  Ndipo Gideoni akawaambia, “Ni sawa, lakini Yehova atakapowatia Zeba na Zalmuna mikononi mwangu, nitawacharaza ninyi kwa miiba na michongoma ya nyikani.”+  Naye akatoka huko na kwenda Penueli, akawaomba pia mikate, lakini watu wa Penueli wakamjibu kama watu wa Sukothi walivyomjibu.  Basi akawaambia pia watu wa Penueli, “Nitakaporudi baada ya kushinda, nitaubomoa mnara huu.”+ 10  Basi Zeba na Zalmuna walikuwa Karkori pamoja na wanajeshi wao wapatao 15,000. Hao tu ndio waliobaki wa jeshi lote la watu wa Mashariki,+ kwa kuwa wenzao 120,000 waliotumia upanga waliuawa. 11  Gideoni akaendelea kupanda kupitia eneo la watu waliokaa mahemani upande wa mashariki wa Noba na Yogbeha+ na kushambulia kambi ya maadui ambao hawakuwa wamejitayarisha kupigana. 12  Zeba na Zalmuna walipokimbia, Gideoni aliwafuatia na kuwakamata hao wafalme wawili wa Midiani, Zeba na Zalmuna, na jeshi lao lote likaogopa. 13  Kisha Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani kupitia njia inayopanda kwenda Heresi. 14  Alipokuwa njiani, alimkamata kijana mmoja wa Sukothi na kumuuliza maswali. Basi kijana huyo akamwandikia majina 77 ya wakuu na wazee wa Sukothi. 15  Ndipo akarudi kwa watu wa Sukothi na kuwaambia, “Ndio hawa Zeba na Zalmuna ambao mlinidhihaki kuwahusu mkisema, ‘Je, tayari umewakamata Zeba na Zalmuna ndipo tuwape mikate wanaume wako waliochoka?’”+ 16  Ndipo akawachukua wazee wa jiji hilo na kuwacharaza kwa miiba na michongoma ya nyikani, akawafunza somo wanaume wa Sukothi.+ 17  Kisha akabomoa mnara wa Penueli+ na kuwaua watu wa jiji hilo. 18  Akawauliza Zeba na Zalmuna, “Watu mliowaua kule Tabori walikuwaje?” Wakasema, “Walikuwa kama wewe, walikuwa kama wana wa mfalme.” 19  Ndipo akasema, “Ni ndugu zangu, wana wa mama yangu. Kwa hakika kama Yehova anavyoishi, ikiwa hamngewaua, mimi pia singewaua ninyi.” 20  Kisha akamwambia Yetheri mzaliwa wake wa kwanza, “Haya, waue.” Lakini kijana huyo hakuchomoa upanga wake; aliogopa kwa sababu alikuwa kijana tu. 21  Basi Zeba na Zalmuna wakamwambia, “Tuue wewe mwenyewe, kwa maana mwanamume hujulikana kwa nguvu zake.”* Basi Gideoni akawaua Zeba na Zalmuna+ na kuchukua mapambo yenye umbo la mwezi mwandamo yaliyokuwa shingoni mwa ngamia wao. 22  Baadaye Waisraeli wakamwambia Gideoni, “Tutawale, wewe na mwana wako na mjukuu wako pia, kwa maana umetuokoa kutoka mikononi mwa Wamidiani.”+ 23  Lakini Gideoni akawaambia, “Mimi sitawatawala, wala mwanangu. Yehova ndiye atakayewatawala.”+ 24  Pia akawaambia, “Ningependa kuomba jambo moja: Kila mmoja wenu anipe pete ya puani aliyochukua nyara.” (Walikuwa na pete za puani za dhahabu kwa sababu walikuwa Waishmaeli.)+ 25  Wakasema, “Tutakupa.” Basi wakatandaza nguo na kila mmoja wao akaweka pete ya puani aliyochukua nyara. 26  Na zile pete za puani za dhahabu ambazo aliwaomba zilikuwa na uzito wa shekeli 1,700 za dhahabu,* mbali na yale mapambo yenye umbo la mwezi mwandamo, hereni, mavazi ya sufu ya rangi ya zambarau yaliyovaliwa na wafalme Wamidiani, na mikufu iliyokuwa shingoni mwa ngamia.+ 27  Basi Gideoni akatumia dhahabu hiyo kutengeneza efodi*+ na kuiweka hadharani katika jiji lake la Ofra;+ na huko Waisraeli wote wakafanya nayo ukahaba wa kiroho,+ ikawa mtego kwa Gideoni na kwa nyumba yake.+ 28  Hivyo Wamidiani+ wakashindwa na Waisraeli, na hawakupigana nao* tena; na nchi ikawa na amani* kwa miaka 40 katika siku za Gideoni.+ 29  Basi Yerubaali+ mwana wa Yoashi akarudi nyumbani kwake na kukaa huko. 30  Gideoni akawa na wana 70,* kwa sababu alikuwa na wake wengi. 31  Na suria* wake aliyekuwa Shekemu akamzalia mwana, na Gideoni akamwita Abimeleki.+ 32  Gideoni mwana wa Yoashi akafa baada ya kuishi maisha marefu, akazikwa katika kaburi la Yoashi baba yake katika jiji la Ofra la Waabiezeri.+ 33  Mara tu baada ya Gideoni kufa, Waisraeli wakaanza tena kufanya ukahaba wa kiroho na Mabaali,+ nao wakamfanya Baal-berithi kuwa mungu wao.+ 34  Na Waisraeli hawakumkumbuka Yehova Mungu wao+ aliyewaokoa kutoka mikononi mwa maadui wao waliowazunguka;+ 35  wala hawakuwa na upendo mshikamanifu kwa nyumba ya Yerubaali, yaani, Gideoni, aliyewatendea Waisraeli mambo mengi mema.+

Maelezo ya Chini

Tnn., “neno hilo.”
Tnn., “roho yao ikatulia.”
Tnn., “kwa maana jinsi mwanamume alivyo, ndivyo zilivyo nguvu zake.”
Shekeli moja ilikuwa na uzito wa gramu 11.4. Angalia Nyongeza B14.
Au “kizibao cha kuhani.”
Tnn., “hawakuinua kichwa chao.”
Tnn., “ikapumzika.”
Tnn., “alikuwa na wana 70 waliotoka katika viuno vyake.”
Angalia Kamusi.