UNAWEZA KUKABILIANA NA MKAZO—JINSI GANI?
Mkazo Ni Nini?
Mkazo hutokea mwili unapojitayarisha kuchukua hatua ili kukabiliana na changamoto au hatari fulani. Ubongo husababisha tezi zitoe homoni nyingi na kusafirishwa sehemu mbalimbali mwilini. Homoni hizo huongeza kasi ya mapigo ya moyo, hudhibiti shinikizo la damu, hufanya mtu apumue haraka-haraka, na misuli kukaza. Hata kabla ya mtu kutambua kinachoendelea, mwili unakuwa tayari kuchukua hatua. Hali inayoleta mkazo inapokwisha, mwili hurudia hali yake ya kawaida.
MKAZO UNAOFAA NA USIOFAA
Mkazo ni hali ya asili ambayo mwili hujitayarisha kuchukua hatua dhidi ya changamoto au hatari fulani. Hali hiyo huanzia kwenye ubongo. Mkazo unaofaa hukuwezesha kutenda au kuchukua hatua haraka. Kiwango fulani cha mkazo kinaweza kukusaidia pia kufikia malengo yako au kufanya vizuri, labda wakati wa mtihani, mahojiano ya kazi au katika mchezo.
Hata hivyo, mkazo mwingi sana na unaoendelea kwa muda mrefu unaweza kukudhuru. Ikiwa mwili unakuwa katika hali ya ‘tahadhari’ kwa sababu ya mkazo mwingi mara kwa mara, huenda mtu akaanza kuugua kimwili, kihisia na kiakili pia. Tabia yako kutia ndani jinsi unavyowatendea wengine huenda ikabadilika. Mtu anapokuwa na mkazo kupita kiasi anaweza kuanza kutumia kileo sana, dawa za kulevya au kujihusisha na mazoea mengine mabaya. Pia, mkazo unaweza kusababisha mtu ashuke moyo, achoke kupita kiasi au hata kuwa na mawazo ya kujiua.
Ingawa mkazo huathiri watu kwa njia tofauti-tofauti, unaweza kusababisha matatizo ya afya kwa kiasi kikubwa. Na unaweza kuathiri karibu kila sehemu ya mwili.