JE, DUNIA YETU ITAOKOKA?
Maji Safi
KUSINGEKUWA na uhai duniani ikiwa maji yasingekuwepo, hasa maji safi. Kwa kweli, maji ni muhimu kwa viumbe hai. Maziwa, mito, maeneo yenye maji mengi, na hifadhi za maji zilizo chini ya ardhi, hutokeza maji ya kunywa kwa ajili ya wanadamu na wanyama na kwa ajili ya kumwagilia mazao yetu.
Kwa Nini Tunahitaji Kulinda Maji Safi
Sehemu kubwa ya dunia yetu ina maji. Hata hivyo, kulingana na Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Ulimwenguni, “ni asilimia 0.5 tu ya maji Duniani yaliyo safi na yanayoweza kutumiwa.” Ijapokuwa kiwango hicho cha maji safi kinapaswa kutosha kutegemeza uhai duniani, kiasi kikubwa cha maji hayo yamechafuliwa au hayapatikani kwa urahisi kwa sababu ya kuongezeka kwa mahitaji au mabadiliko ya hali ya hewa. Wataalamu wanasema kwamba ndani ya miaka 30, huenda watu bilioni tano wasiwe na uwezo wa kupata maji safi.
Dunia Yetu Imeumbwa Ikiwa na Uwezo wa Kuokoka
Dunia ina mifumo ya asili inayohakikisha kwamba kuna maji ya kutosha. Pia, udongo, wanyama wanaoishi katika maji, na hata mwangaza wa jua, hushirikiana ili kusafisha maji yetu. Ona baadhi ya uthibitisho unaoonyesha jinsi dunia yetu ilivyotengenezwa ikiwa na uwezo wa kuokoka.
-
Inaonekana kwamba udongo unaweza kuondoa uchafu mwingi ulio katika maji. Katika maeneo yenye maji mengi, mimea fulani inajulikana kwa uwezo wake wa kuondoa nitrojeni, fosforasi, na dawa za kuua wadudu.
-
Wanasayansi wamejifunza jinsi maji yanavyodumu yakiwa safi kwa njia ya asili. Uchafu huchanganywa katika mkondo wa maji na kisha humeng’enywa na vijidudu.
-
Chaza na kome walio katika maji safi wana uwezo wa kuondoa kemikali hatari zilizo katika maji ndani ya siku chache—na huenda wanafanya hivyo kwa ufanisi zaidi kuliko hata mitambo inayotumika kusafisha maji.
-
Dunia yetu inahifadhi maji kupitia mzunguko wa maji usiobadilika. Mzunguko huo na mifumo mingine ya kiasili, huzuia maji yasipotee au kuondoka katika angahewa.
Hatua Zinazochukuliwa Sasa
Wataalamu wanapendekeza kuhifadhi na kutumia vizuri maji kadiri inavyowezekana. Ili kupunguza uchafu katika maji, wanashauri kurekebisha sehemu zozote zinazovuja mafuta katika magari yetu na kutotupa dawa tusizotumia msalani au kumwaga sumu katika mfereji.
Wahandisi wamebuni njia nzuri za kuondoa chumvi kwenye maji ya bahari. Lengo lao ni kuongeza kiwango cha maji safi.
Lakini mengi yanahitajika. Kuondoa chumvi katika maji ya bahari si suluhisho linalofaa kwa sababu jambo hilo linagharimu nishati na pesa nyingi. Chanzo kimoja cha Umoja wa Mataifa, kilisema hivi kuhusu ripoti ya mwaka wa 2021 iliyozungumzia jinsi ya kulinda maji safi: “Jitihada zinahitaji kuongezwa zaidi duniani kote.”
Sababu za Kuwa na Tumaini—Biblia Inasema Nini
“Mungu . . . huvuta juu matone ya maji; yanaganda na kuwa mvua kutokana na ukungu wake; kisha mawingu huyamwaga chini; yanawanyeshea wanadamu.”—Ayubu 36:26-28.
Mungu aliumba mizunguko ya asili kulinda maji yaliyo duniani.—Mhubiri 1:7.
Fikiria hili: Ikiwa Muumba ameweka mifumo ya kusafisha maji, bila shaka anaweza na yuko tayari kurekebisha madhara yanayosababishwa na wanadamu. Ona makala yenye kichwa, “Mungu Anaahidi Kwamba Dunia Yetu Itaokoka,” katika ukurasa wa 15.