Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Watu Hawaheshimu Uhai?

Kwa Nini Watu Hawaheshimu Uhai?

KWA NINI NI MUHIMU KUHESHIMU UHAI

Unapofanya mambo yanayodhuru afya yako au ya wengine, hilo linaonyesha kwamba hauthamini uhai wako na wa wengine.

  • Uvutaji wa sigara unasababisha saratani na kufanya iwe vigumu kwa mwili kupambana nayo. Kwa kweli, asilimia 90 ya vifo vinavyotokana na saratani ya mapafu, vimesababishwa na uvutaji wa sigara au kuwa karibu kwa muda mrefu na mtu anayevuta sigara.

  • Kila mwaka, mauaji ya halaiki yanawasababishia watu wengi maumivu ya kihisia. Ripoti moja kutoka Chuo Kikuu cha Stanford inasema hivi: “Utafiti unaonyesha kwamba wale waliookoka [mashambulizi ya risasi shuleni] bila kujeruhiwa, bado wanaathiriwa na matatizo ya kihisia na kiakili hata baada ya miaka mingi kupita.

  • Watu wanaoendesha magari wakiwa wamelewa au wakiwa wametumia dawa za kulevya, hufanya iwe hatari kwa watu wengine kutumia barabara. Watu wanapotenda bila kujali uhai, mara nyingi huwaathiri watu wasio na hatia.

JAMBO UNALOWEZA KUFANYA

Linda afya yako. Bado haujachelewa. Unaweza kuacha mazoea mabaya kama vile kuvuta sigara, kutia ndani zile za kielektroni, kulewa, au kutumia dawa za kulevya. Mazoea hayo yanadhuru afya yako na hayaheshimu uhai wa wale unaoshirikiana nao, kutia ndani familia yako.

“Acheni tujisafishe kila unajisi wa mwili.” —2 Wakorintho 7:1.

Zingatia usalama wako na wa wengine. Dumisha nyumba ikiwa katika hali nzuri ili kuepuka aksidenti. Endesha gari kwa kuzingatia usalama na hakikisha liko katika hali nzuri. Usikubali wengine wakushinikize ufanye mambo ambayo yatakuumiza au kukusababishia kifo.

“Ukijenga nyumba mpya, ni lazima pia ujenge ukuta kuzunguka ukingo wa paa lako, ili mtu asianguke kutoka kwenye paa nawe uiletee familia yako hatia ya damu.”—Kumbukumbu la Torati 22:8. a

Watendee wengine kwa fadhili. Kuheshimu uhai kunatia ndani kuwatendea kwa fadhili watu wote bila kujali jamii, nchi, hali zao za kiuchumi au elimu yao. Kwa kweli, ubaguzi na chuki ni chanzo kikuu cha ujeuri na vita vinavyoendelea leo.

“Acheni kabisa kila aina ya chuki yenye uhasama, hasira, ghadhabu, kufoka, matusi, na mambo yote yanayodhuru. Bali mtendeane kwa fadhili.” —Waefeso 4:​31, 32.

MAMBO TUNAYOFANYA

Mashahidi wa Yehova huwafundisha wengine kuishi maisha yanayofaa. Programu yetu ya kujifunza Biblia imewasaidia watu kuacha uraibu na tabia au mitindo ya maisha inayodhuru afya.

Tunafuata viwango vya juu vya usalama katika miradi yetu ya ujenzi. Wajitoleaji wanaosaidia kujenga majengo yetu ya mikutano na majengo mengine yanayotumiwa kwa ajili ya kazi ya kutoa elimu ya Biblia, wamezoezwa jinsi ya kufanya kazi bila kusababisha aksidenti. Majengo yetu hukaguliwa kwa ukawaida ili kutii sheria za eneo husika.

Tunatoa msaada. Hivi karibuni katika kipindi cha miezi 12, tulitoa msaada kwa watu walioathiriwa na misiba 200 hivi duniani na tulitumia dola za Marekani milioni 12 hivi zilizochangwa ili kutoa msaada kwa waathirika.

Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ulipoathiri watu wengi Magharibi mwa Afrika (2014) na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (2018), tuliwafundisha watu jinsi ya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo hatari. Tuliwatuma wawakilishi wetu wazungumze na vikundi vya watu kwa kutoa hotuba yenye kichwa “Utii Huokoa Uhai.” Tuliandaa vituo vya kunawia mikono katika kila mwingilio wa sehemu zetu za ibada, na tulisisitiza umuhimu wa kunawa mikono na kuchukua tahadhari nyingine.

Nchini Sierra Leone, kituo kimoja cha redio kiliwapongeza Mashahidi wa Yehova kwa jinsi walivyowasaidia waamini wenzao na watu wengine ambao si Mashahidi kuepuka kuambukizwa virusi vya ugonjwa wa Ebola.

Kituo cha kunawia mikono katika Jumba la Ufalme wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Liberia mwaka wa 2014

a Zamani, watu katika Mashariki ya Kati walitii takwa hilo lenye hekima kwa kuwa walihangaikia usalama wa washiriki wa familia zao na watu wengine.