5 Je, Kuteseka Kutakwisha?
Kwa Nini ni Muhimu Kupata Jibu la Swali Hilo?
Ikiwa kuna sababu ya kuamini kwamba kuteseka kutakwisha, tumaini hilo litatusaidia kuwa na mtazamo mzuri kuhusu maisha yetu na kumhusu Mungu.
Jambo la Kufikiria
Watu wengi wangependa kuondoa mateso, lakini hawana uwezo wa kufanya hivyo. Fikiria mambo yafuatayo:
Licha ya maendeleo ya kitiba . . .
-
Ugonjwa wa moyo bado ni chanzo kikuu cha vifo vya watu wengi.
-
Kansa inaua mamilioni ya watu kila mwaka.
-
Dkt. David Bloom aliandika hivi katika jarida la Frontiers in Immunology: “Watu ulimwenguni wanaendelea kukabili magonjwa hatari ya kuambukiza yaliyosumbua zamani na magonjwa mapya yanayozidi kuibuka.”
Licha ya hali nzuri ya kiuchumi katika baadhi ya nchi . . .
-
Mamilioni ya watoto wanakufa kila mwaka, na mara nyingi wale wanaoishi katika mazingira magumu ndio wanaoathirika zaidi.
-
Mabilioni ya watu wanaishi katika maeneo ambayo hayana huduma bora ya vyoo.
-
Mamia ya mamilioni ya watu hawapati maji safi.
Licha ya watu wengi kujua haki za binadamu . . .
-
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa inasema kwamba biashara ya kuuza watu inaendelea katika nchi nyingi, na baadhi ya nchi zimeshindwa kuwashtaki wale wanaofanya biashara hiyo kwa sababu “wenye mamlaka hawajui au hawana uwezo wa kuwashtaki.”
JIFUNZE MENGI ZAIDI
Tazama video Ufalme wa Mungu Ni Nini? inayopatikana kwenye jw.org/sw.
Mambo Ambayo Biblia Inafundisha
Mungu anatujali.
Anahisi maumivu na kilio chetu.
“[Mungu] hajadharau . . . mateso ya yule anayekandamizwa; hajauficha uso wake kutoka kwake. Alipomlilia amsaidie, alisikia.”—ZABURI 22:24.
“[Tupeni] mahangaiko yenu yote juu yake, kwa sababu yeye anawajali ninyi.”—1 PETRO 5:7.
Kuteseka hakutaendelea milele.
Biblia inaahidi kwamba kusudi la Mungu kwa wanadamu litatimia.
“Mungu . . . atafuta kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala maombolezo wala kilio wala maumivu hayatakuwapo tena.”—UFUNUO 21:3, 4.
Mungu ataondoa mambo yanayosababisha wanadamu wateseke.
Atafanya hivyo kupitia Ufalme wake, ambao Biblia inataja kuwa ni serikali halisi.
“Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa kamwe. Na ufalme huo hautakabidhiwa watu wengine wowote. . . . Nao pekee utasimama milele.”—DANIELI 2:44.