Teknolojia Inaathirije Uhusiano Wako na Wengine?
Leo, watu wanaweza kuwasiliana kwa urahisi kupitia ujumbe mfupi, barua pepe, video, na mitandao ya kijamii hata ikiwa wanaishi katika mabara mawili tofauti. Kwa upande wao, teknolojia huwasaidia.
Kwa upande mwingine, baadhi ya watu ambao wanatumia teknolojia kama njia kuu ya kudumisha urafiki . . .
-
hawana hisia-mwenzi au hawaelewi hisia za marafiki wao.
-
huhisi upweke na wameshuka moyo.
-
hujifikiria wenyewe tu badala ya kuwafikiria wengine.
UNACHOPASWA KUJUA
HISIA-MWENZI
Hisia-mwenzi ni sifa inayotulazimu tutulie, na kwa subira tumfikirie mtu mwingine. Huenda isiwe rahisi kuwa na hisia-mwenzi hasa ikiwa tunataka kuangalia kila kitu kilichowekwa kwenye mitandao ya kijamii na kujibu kila ujumbe haraka-haraka.
Ukitumia teknolojia kupita kiasi, baada ya muda, itakuwa vigumu kujibu jumbe zote unazopokea. Lengo lako litaanza kuwa kujibu kila ujumbe unaoingia badala ya kumsaidia rafiki mwenye uhitaji.
JAMBO LA KUFIKIRIA: Unaweza kudumishaje “hisia-mwenzi” unapotumia teknolojia kuwasiliana na marafiki wako?—1 PETRO 3:8.
KUSHUKA MOYO
Ripoti moja ya utafiti ilisema kwamba watu wengi hujisikia vibaya zaidi baada ya kutumia muda mwingi kuangalia picha na video kwenye kurasa za mitandao ya kijamii zinazopendwa na watu wengi. Watafiti hao walifikia mkataa kwamba kutazama picha na mambo mapya ambayo wengine huweka mtandaoni hufanya mtu “ahisi amepoteza muda wake.”
Isitoshe, kuangalia picha za kusisimua ambazo watu wameweka kwenye mitandao ya kijamii hufanya watu waanze kujilinganisha na wengine. Inaweza kuonekana kila mtu anafurahia maisha, huku wewe ukichoshwa na maisha yako.
JAMBO LA KUFIKIRIA: Unawezaje kuepuka kujilinganisha na wengine unapotumia mitandao ya kijamii?—WAGALATIA 6:4.
KUJIFIKIRIA MWENYEWE
Mwalimu mmoja alisema kwamba baadhi ya wanafunzi wake walikuwa wabinafsi na walitaka tu marafiki ambao wangefanya mambo kwa ajili yao. * Urafiki kama huo unategemea kile ambacho mtu anapata kutokana na uhusiano huo. Kisha, anaanza kuwaona rafiki zake kama programu za simu ambazo anaweza kuzitumia na kuzizima wakati wowote.
JAMBO LA KUFIKIRIA: Je, mambo unayoweka mtandaoni yanaonyesha kwamba una roho ya ushindani au unajifikiria mwenyewe kupita kiasi?—WAGALATIA 5:26.
UNACHOWEZA KUFANYA
CHUNGUZA JINSI UNAVYOTUMIA TEKNOLOJIA
Ikiwa teknolojia inakusaidia badala ya kukutawala, itakuwezesha kuwasiliana na marafiki wako na kuboresha urafiki wenu.
KANUNI YA BIBLIA: “Upendo . . . hautafuti faida zake wenyewe.”—1 WAKORINTHO 13:4, 5.
Weka alama kwenye mapendekezo ambayo ungependa kutumia, au andika mawazo yako kwenye sehemu iliyoachwa wazi.
-
Kuzungumza na marafiki wangu uso kwa uso (badala ya kutegemea tu ujumbe mfupi au barua pepe)
-
Kuweka simu yangu mbali (au kuzima sauti) ninapozungumza na wengine
-
Kupunguza muda ninaotumia kuangalia kurasa za mitandao ya kijamii
-
Kuwa msikilizaji mzuri
-
Kuwasiliana na rafiki anayekabili hali ngumu
^ fu. 17 Imeripotiwa na kitabu Reclaiming Conversation.