Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Teknolojia Inawaathirije Watoto Wako?

Teknolojia Inawaathirije Watoto Wako?

Kwa sababu ya uwezo wao wa kutumia teknolojia na programu mpya, mara nyingi watoto huitwa “kizazi cha kidigitali,” lakini si rahisi kwa watu wazima kutumia programu hizo.

Wakati huohuo, watoto wanaotumia muda mwingi mtandaoni . . .

  • wanakuwa waraibu wa vifaa vya kielektroni.

  • wanaweza kunyanyaswa au kuwanyanyasa wengine mtandaoni.

  • wanaweza kutazama ponografia kwa urahisi, iwe wamekusudia au la.

UNACHOPASWA KUJUA

URAIBU

Baadhi ya mambo yanayopatikana mtandaoni kama vile michezo ya video, yamekusudiwa kuwafanya watu wawe waraibu. Hilo halishangazi. Kitabu kimoja (Reclaiming Conversation) kinasema hivi: “Programu kwenye simu zetu zimekusudiwa kutufanya tutumie simu zetu wakati wote.” Kadiri tunavyotumia programu hizo kwa muda mrefu, ndivyo watengenezaji wake wanavyopata faida zaidi.

JAMBO LA KUFIKIRIA: Je, watoto wako wanatumia vifaa vya kielektroni kupita kiasi? Unaweza kuwasaidiaje watumie muda wao kwa njia bora zaidi?​—WAEFESO 5:15, 16.

KUNYANYASWA AU KUWANYANYASA WENGINE MTANDAONI

Baadhi ya watu huwa wakali, wenye tabia mbaya, na wasiojali hisia za wengine wanapotumia mitandao​—mambo yanayofanya wawanyanyase wengine.

Watu wengine wanatumia vibaya mitandao ya kijamii kwa sababu wanataka wajulikane au wawe maarufu. Au mtu anaweza kuhisi ametengwa na wengine​—kwa mfano, ikiwa ataona mtandaoni marafiki wake wote wamealikwa kwenye tafrija lakini yeye hakualikwa huenda akafikiri amenyanyaswa.

JAMBO LA KUFIKIRIA: Je, watoto wako wanawanyanyasa wengine mtandaoni? (Waefeso 4:31) Wanakabilianaje na hisia za kutengwa na wengine?

PONOGRAFIA

Ni rahisi sana kupata au kuona mambo machafu mtandaoni. Wazazi wanapaswa kutambua kwamba ingawa baadhi ya programu huwasaidia kudhibiti mambo ambayo watoto wao hutazama, haziwezi kudhibiti mambo yote, na bado watoto wanaweza kuona mambo machafu.

Kutuma au kupokea ujumbe au picha chafu, mara nyingi kupitia simu ya mkononi, kunaweza kuwa kosa kisheria. Katika visa fulani, kwa kutegemea sheria za eneo ambalo mtu anaishi au umri wake, mtu anayetuma ujumbe au picha chafu anaweza kushtakiwa kwa kosa la kusambaza ponografia ya watoto.

JAMBO LA KUFIKIRIA: Unaweza kumsaidiaje mtoto wako aepuke kishawishi cha kutazama au kutuma picha chafu mtandaoni?​—WAEFESO 5:3, 4.

UNACHOWEZA KUFANYA

WAZOEZE WATOTO WAKO

Ingawa watoto wanaweza kutumia teknolojia kwa urahisi, bado wanahitaji mwongozo. Kitabu kinachoitwa Indistractable kinasema kwamba kumpatia mtoto wako simu ya mkononi au kifaa kingine cha kielektroni kabla hajawa na uwezo wa kukitumia kwa njia inayofaa, ni “jambo la kipumbavu kama kumruhusu mtoto asiyejua kuogelea kutumbukia bwawani.”

KANUNI YA BIBLIA: “Mzoeze mtoto njia anayopaswa kuifuata; hata atakapozeeka hataiacha.”​—METHALI 22:6, MAELEZO YA CHINI.

Weka alama kwenye mapendekezo ambayo ungependa kutumia, au andika mawazo yako kwenye sehemu iliyoachwa wazi.

  • Kuzungumza na mtoto wangu kuhusu jinsi ya kujiendesha kwa njia inayofaa mtandaoni

  • Kumsaidia mtoto wangu kukabiliana na hisia za kutengwa na wengine

  • Kujitahidi kadiri niwezavyo kumlinda mtoto wangu kutokana na mambo machafu mtandaoni

  • Kukagua simu ya mtoto wangu mara kwa mara

  • Kumpangia mtoto wangu muda hususa wa kutumia kifaa chake cha kielektroni

  • Kumzuia mtoto wangu asitumie kifaa chake akiwa peke yake usiku

  • Kuweka sheria kwamba mtu yeyote haruhusiwi kutumia simu wakati familia inapokula pamoja