Mzio wa Chakula na Tatizo la Kumeng’enya Chakula—Tofauti ni Nini?
Emily: “Baada ya kumaliza kula, nilianza kujisikia vibaya. Nilihisi mwasho mdomoni na ulimi ulianza kuvimba. Nilihisi kizunguzungu na nikashindwa kupumua. Vipele vilitokea mikononi na shingoni. Nilijaribu kutulia lakini nilitambua kwamba ninapaswa kwenda hospitalini haraka!”
WATU wengi hufurahia kula chakula. Hata hivyo, baadhi ya watu huona vyakula fulani kuwa kama “adui.” Kama Emily aliyetajwa mwanzoni mwa makala hii, wengine pia wana mzio wa chakula. Dalili kama za Emily zinazoitwa anaphylaxis ni hatari sana. Hata hivyo, aina nyingi za mizio si hatari.
Katika miaka ya hivi karibuni, visa vya mzio wa chakula au tatizo la kumeng’enya chakula vimeripotiwa kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kwamba ni wachache tu waliochunguzwa na daktari na kupatikana na mzio wa chakula.
Mzio Wa Chakula ni Nini?
Kulingana na ripoti ya The Journal of the American Medical Association, wanasayansi fulani wakiongozwa na Dr. Jennifer J. Schneider Chafen walisema: “Mzio wa chakula hauwezi kufafanuliwa kikamili.” Ingawa hivyo, wataalamu wengi wanaamini kwamba mara nyingi tatizo la mzio husababishwa na mfumo wa kinga.
Mara nyingi, mzio wa chakula husababishwa na protini zilizo kwenye chakula. Mfumo wa kinga hutambua protini fulani kuwa kama adui. Aina fulani za protini zinapoingia mwilini, mfumo huo hutokeza kinga mwili ziitwazo IgE ili kupigana na protini hizo. Mtu anapokula chakula chenye protini hizo tena, kinga mwili huchochea kutokezwa kwa kemikali kama vile histamini.
Kwa kawaida, kemikali ya histamini ina umuhimu mkubwa sana katika mfumo wa kinga. Hata hivyo, kwa sababu zisizoeleweka, IgE na kemikali ya histamini zinapotokezwa kwa pamoja mwilini, dalili za mzio huonekana hasa kwa watu ambao huathiriwa haraka na protini za aina fulani.
Ndiyo sababu huenda chakula kisimdhuru mtu mara ya kwanza, lakini kikamdhuru anapokula kwa mara nyingine.
Tatizo la Kumeng’enya Chakula Ni Nini?
Kama ilivyo kwa mzio, tatizo la kumeng’enya chakula huenda likasababishwa na aina fulani ya vyakula. Lakini, tofauti na mzio wa chakula (ambao husababishwa moja kwa moja na mfumo wa kinga), tatizo hili hutokana na mfumo wa kumeng’enya chakula, hivyo kinga mwili hazihusiki. Kwa kawaida mfumo wa kumeng’enya chakula hushindwa kumeng’enya hasa kwa sababu ya upungufu wa vimeng’enya au kwa kuwa kemikali zilizo katika chakula hazijameng’enywa. Kwa
mfano, tatizo la kumeng’enya maziwa hutokea matumbo yanapokosa kutokeza vimeng’enya ili kumeng’enya sukari ipatikanayo kwenye maziwa.Kwa kuwa kinga mwili hazihusiki, tatizo la kumeng’enya linaweza kujitokeza mtu anapokula aina fulani ya chakula kwa mara ya kwanza. Tatizo hilo hutegemea kiasi cha chakula, yaani, huenda kiasi kidogo kikameng’enywa lakini kiasi kikubwa kinaweza kusababisha tatizo. Hilo ni tofauti na mzio kwa kuwa hata kiasi kidogo cha chakula kinaweza kusababisha matatizo makubwa.
Ni Nini Dalili za Matatizo Hayo?
Ukiwa na tatizo la mzio wa chakula huenda ukaona dalili zifuatazo: mwili kuwasha; kuota vipele; kuvimba koo, macho, au ulimi; kichefuchefu; kutapika; kuharisha; na ikiwa hali ni mbaya zaidi, huenda ukapata shinikizo la damu, kizunguzungu, kuzimia na hata moyo kuacha kupiga. Tatizo hilo linaweza kuenea haraka na hata kusababisha kifo.
Kuna uwezekano kwamba vyakula vyote vinaweza kusababisha mzio. Hata hivyo, aina mbaya ya mzio husababishwa na baadhi tu ya vyakula, yaani, maziwa, mayai, samaki, samaki aina ya kamba, karanga, soya, karanga za miti na ngano. Mtu mwenye umri wowote anaweza kupata tatizo la mzio. Utafiti unaonyesha kwamba chembe za urithi zina mchango mkubwa katika tatizo hilo, huenda mtoto akarithi mzio kutoka kwa wazazi. Baada ya kukua, watoto huacha kuwa na tatizo la mzio.
Tatizo la kumeng’enya chakula si hatari kama vile ilivyo kwa mzio. Tatizo hilo hutokeza dalili kama vile kuumwa tumbo, kuvimba, gesi, kukakamaa kwa tumbo, kuumwa na kichwa, kuwashwa ngozi, na uchovu. Tatizo hilo husababishwa na baadhi ya vyakula kama vile maziwa, ngano, hamira na pombe.
Kutambua Tatizo na Kutibu
Ikiwa unadhani kwamba una mzio au tatizo la kumeng’enya chakula, unaweza kwenda kwa mtaalamu wa matatizo hayo ili kupimwa. Si vizuri kujiamulia mwenyewe kuacha kutumia vyakula fulani kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kufanya mwili wako ukose virutubisho.
Hakuna tiba hususa kwa tatizo la mzio, njia pekee inayoweza kusaidia ni kuacha kabisa kula vyakula vinavyosababisha mzio. * Kwa upande mwingine, ikiwa una tatizo dogo la mzio au kumeng’enya chakula, huenda ikafaa kupunguza kiasi au mara unazokula vyakula vinavyosababisha matatizo hayo. Lakini, katika visa fulani huenda mgonjwa akashauriwa kuacha kula aidha kabisa au kwa muda fulani, ikitegemea madhara yanayosababishwa na chakula hicho.
Hata hivyo, iwe una mzio au tatizo la kumeng’enya chakula, utafaidika kujua kwamba wengi walio na matatizo hayo wamejifunza jinsi ya kuyashughulikia nao wanafurahia kula vyakula vitamu na vyenye lishe vya aina mbalimbali.
^ fu. 19 Inapendekezwa kwamba wale walio na tatizo kubwa la mzio wabebe dawa aina ya adrenalini (epinephrine) wanayoweza kujidunga kwa sindano wanapopatwa na dharura. Baadhi ya wataalamu wa afya hupendekeza kwamba watoto walio na mzio wabebe au kuvaa alama fulani ambayo itawasaidia walimu au wanaowatunza kutambua kuhusu hali yao.