Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Manyoya ya Fisi Maji wa Baharini

Manyoya ya Fisi Maji wa Baharini

WANYAMA wengi wanaoishi katika maji ya baridi wana tabaka jembamba la mafuta lililo ndani ya ngozi linalowasaidia kudumisha joto. Lakini fisi maji wa baharini hutumia mbinu nyingine. Yeye hutegemea manyoya yake yaliyobanana.

Fikiria jambo hili: Manyoya ya fisi wa baharini yamebanana zaidi kuliko ya mnyama mwingine yeyote. Ana manyoya karibu milioni moja katika kila inchi ya mraba (155,000 kwa kila sentimita ya mraba). Anapoogelea, manyoya yake huungana na kufanyiza tabaka la hewa katikati ya manyoya na ngozi yake. Hivyo, tabaka hilo la hewa huwa kama koti linalomkinga, kwa kuzuia maji ya baridi kugusa moja kwa moja ngozi yake na hivyo kuathiri joto la mwili.

Wanasayansi wanaamini kwamba kuna jambo tunaloweza kujifunza kutokana na manyoya ya fisi maji wa baharini. Wamejaribu kuiga kwa kutengeneza makoti yaliyo na manyoya yenye urefu mbalimbali, na manyoya yaliyobanana au kuachiana nafasi. Watafiti wamefikia mkataa wa kwamba, “kadiri manyoya yanavyobanana na kuwa marefu, ndivyo inavyokuwa vigumu zaidi kwa maji kupita.” Hilo ni sawa na kusema kwamba, fisi maji wa baharini ana koti bora sana.

Watafiti wanatumaini kwamba utafiti wao utasaidia kuboresha teknolojia ya kubuni na kutokeza vitambaa visivyoweza kupenya maji. Huenda hili likachochea watu fulani wafikirie kwamba ni bora wale wanaopiga mbizi kwenye maji ya baridi wavae mavazi yenye manyoya, kama vile fisi maji wa baharini!

Una maoni gani? Je, mfumo wa kutunza hewa ndani ya manyoya ya fisi maji ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?