Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Ni gari la aina gani ambalo towashi Mwethiopia alikuwa akitumia Filipo alipomkaribia?

NENO la awali lililotafsiriwa “gari” katika Tafsiri ya Ulimwengu Mpya linaweza kurejelea aina mbalimbali za magari ya kukokotwa na farasi. (Mdo. 8:28, 29, 38) Hata hivyo, inaonekana kwamba towashi Mwethiopia alikuwa akiendesha gari kubwa, si gari dogo la kukokotwa lililotumiwa vitani au kwenye mashindano. Fikiria baadhi ya sababu za kufikia mkataa huu.

Towashi Mwethiopia alikuwa ofisa wa cheo cha juu aliyekuwa amesafiri umbali mrefu. Alikuwa “mwanamume aliyekuwa na mamlaka chini ya Kandake, malkia wa Waethiopia, na ambaye alisimamia hazina yote ya malkia.” (Mdo. 8:27) Ethiopia ya kale ilitia ndani maeneo ya nchi ambayo sasa inaitwa Sudan na baadhi ya maeneo ya upande wa kusini kabisa wa nchi ya sasa ya Misri. Ingawa huenda mwanamume huyo hakutumia gari lilelile katika safari yake yote, lazima alikuwa na mizigo kwa ajili ya safari hiyo ndefu. Baadhi ya magari yaliyotumiwa kusafirisha abiria katika karne ya kwanza W.K. yalikuwa na magurudumu manne. Kitabu kinachoitwa Actsy​—An Exegetical Commentary kinasema hivi: “Magari hayo ya kukokotwa yalikuwa na nafasi ya kutosha ya kubeba mizigo na kufanya safari iwe yenye kustarehesha zaidi, na huenda yalimwezesha mtu kusafiri umbali mrefu zaidi.”

Towashi Mwethiopia alikuwa akisoma, Filipo alipomkaribia. Simulizi hilo linasema kwamba “Filipo akakimbia kandokando na kumsikia [towashi] akimsoma kwa sauti kubwa nabii Isaya.” (Mdo. 8:30) Magari ya kukokotwa kwa ajili ya safari hayakutengenezwa ili yaende kasi. Mwendo huo wa polepole ulimwezesha towashi asome na pia Filipo aliyekuwa akitembea kwa miguu aweze kumfikia.

Towashi Mwethiopia “akamsihi Filipo apande aketi pamoja naye.” (Mdo. 8:31) Katika gari la kukokotwa la mashindano, waendeshaji walisimama. Hata hivyo, kwenye gari la kukokotwa kwa ajili ya safari kungekuwa na nafasi ambayo towashi na Filipo wangeweza kuketi.

Kulingana na rekodi iliyoongozwa na roho inayopatikana kwenye Matendo sura ya 8 na uthibitisho wa kihistoria unaopatikana, machapisho yetu ya hivi karibuni yanaonyesha towashi Mwethiopia akitumia gari kubwa badala ya gari dogo la kukokotwa la kivita au la mashindano.