Maswali Kutoka kwa Wasomaji
Waisraeli walipokuwa nyikani, je, walikula chakula kingine mbali na mana na kware?
Mana ndicho kilikuwa chakula kikuu cha Waisraeli katika miaka 40 waliyokuwa nyikani. (Kut. 16:35) Pia, Yehova aliwaandalia kware katika pindi mbili. (Kut. 16:12, 13; Hes. 11:31) Hata hivyo, pia Waisraeli walikuwa na vyakula vingine.
Kwa mfano, wakati mwingine Yehova aliwaongoza watu wake kwenda “mahali pa kupumzika” ambapo palikuwa na maji ya kunywa na chakula. (Hes. 10:33) Mojawapo ya sehemu hizo ni eneo lililokuwa na maji huko Elimu, “mahali palipokuwa na chemchemi 12 za maji na mitende 70.” (Kut. 15:27) Kitabu Plants of the Bible kinasema kwamba “mitende ambayo inapatikana katika maeneo mengi sana, . . . ndiyo mimea mikuu ambayo inatokeza chakula jangwani, nayo huandaa chakula, mafuta, na makao kwa mamilioni ya watu.”
Huenda pia Waisraeli, walisimama kwenye chemchemi kubwa ambayo leo inaitwa Feiran, iliyo sehemu ya Wadi Feiran. a Kuhusu wadi, au bonde hilo la mto, kitabu Discovering the World of the Bible, kinasema hivi: “Lina urefu wa kilomita 130, na ni mojawapo ya bonde refu zaidi la mto, maridadi zaidi, na linalofahamika zaidi huko Sinai.” Kitabu hicho kinaendelea kusema hivi: “Katika bonde hilo la mto, kilomita 45 hivi kuanzia sehemu linapoingia baharini, kuna kilomita 4.8 za eneo maridadi, lenye mitende linaloitwa Feiran Oasis, lililo mita 610 hivi juu ya usawa wa bahari. Hiyo ndiyo Edeni ya Sinai. Maelfu ya mitende imewavutia watu kuhamia katika eneo hilo tangu nyakati za kale.”
Waisraeli walipokuwa wakiondoka Misri, walibeba unga uliokandwa, vyombo vya kukandia, na labda baadhi ya nafaka na mafuta. Bila shaka, vitu hivyo havikukaa kwa muda mrefu. Pia, watu waliondoka na “kondoo na ng’ombe, naam, mifugo wengi sana.” (Kut. 12:34-39) Hata hivyo, kwa sababu ya hali ngumu iliyokuwa nyikani, inaelekea kwamba idadi ya wanyama hao ilipungua kwa kiasi kikubwa. Huenda Waisraeli walikula baadhi ya wanyama hao. Na wakawatoa wanyama wengine dhabihu, hata kwa miungu ya uwongo. b (Mdo. 7:39-43) Ingawa hivyo, Waisraeli walifuga baadhi ya wanyama, kama inavyoonekana katika maneno haya ambayo Yehova aliwaambia watu walipokosa kumtii: “Wana wenu watakuwa wachungaji nyikani kwa miaka 40.” (Hes. 14:33) Kwa hiyo inawezekana kwamba, mifugo yao iliwaandalia maziwa na pindi fulani nyama, lakini ni wazi kwamba mifugo hiyo haingeweza kuwalisha watu milioni tatu hivi kwa kipindi cha miaka 40. c
Wanyama wao walipata wapi chakula na maji? d Wakati huo huenda kulikuwa na kiwango kikubwa zaidi cha mvua na hivyo inawezekana kulikuwa na mimea mingi zaidi nyikani. Kitabu Insight on the Scriptures, Buku la 1, kinasema kwamba miaka 3,500 iliyopita, “kiwango cha maji huko Arabia kilikuwa cha juu zaidi, kuliko ilivyo leo. Kuwepo kwa mabonde makubwa ya mito ambayo zamani yalikuwa mito, kunatoa uthibitisho kwamba pindi fulani wakati uliopita kulikuwa na kiwango cha kutosha cha mvua ambacho kingeweza kutokeza vijito vya maji.” Ingawa hivyo, nyika hiyo haikuwa na watu na ilikuwa mahali panapotisha. (Kum. 8:14-16) Bila maji ambayo Yehova aliwaandalia kimuujiza, inawezekana kwamba Waisraeli pamoja na wanyama wao wangekufa.—Kut. 15:22-25; 17:1-6; Hes. 20:2, 11.
Musa aliwaambia Waisraeli kwamba Yehova aliwalisha mana “ili awafundishe kwamba mwanadamu haishi kwa mkate tu bali huishi kwa kila neno linalotoka katika kinywa cha Yehova.”—Kum. 8:3.
a Tazama gazeti Mnara wa Mlinzi la Mei 1, 1992, uku. 24-25.
b Biblia inataja pindi mbili ambazo wanyama walitolewa dhabihu kwa Yehova nyikani. Pindi ya kwanza ni wakati ukuhani ulipoanzishwa rasmi; na pindi ya pili ni siku ya Pasaka. Matukio hayo mawili yalifanyika mwaka wa 1512 K.W.K., mwaka wa pili baada ya Waisraeli kuondoka Misri.—Law. 8:14–9:24; Hes. 9:1-5.
c Karibu na mwisho wa ile miaka 40 waliyokuwa nyikani, Waisraeli walichukua nyara ya mamia ya maelfu ya wanyama vitani. (Hes. 31:32-34) Ingawa hivyo, waliendelea kula mana hadi walipoingia katika Nchi ya Ahadi.—Yos. 5:10-12.
d Hakuna jambo lolote linaloonyesha kwamba wanyama walikula mana, kwa kuwa iliandaliwa kulingana na kiasi ambacho kila mtu angeweza kula.—Kut. 16:15, 16.