Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Utiaji-Damu Mishipani Historia Ndefu Yenye Ubishi

Utiaji-Damu Mishipani Historia Ndefu Yenye Ubishi

Utiaji-Damu Mishipani Historia Ndefu Yenye Ubishi

“Ikiwa chembe nyekundu za damu zingekuwa dawa mpya leo, ingekuwa vigumu sana kuziidhinisha.”—Dakt. Jeffrey McCullough.

MNAMO majira ya baridi kali ya mwaka wa 1667, mtu fulani mwenye kichaa na jeuri anayeitwa Antoine Mauroy alipelekwa kwa Jean-Baptiste Denis, tabibu mheshimiwa wa Mfalme Louis wa 14 wa Ufaransa. Denis alikuwa na “ponyo” kamili la kichaa cha Mauroy—kumtia damu ya ndama mishipani, ambayo alifikiri ingetuliza mgonjwa wake. Lakini mambo hayakumwendea sawa Mauroy. Kwa kweli, baada ya kutiwa damu mishipani mara ya pili, alipata nafuu. Lakini punde si punde mwanamume huyo Mfaransa alipatwa na kichaa tena, na baada ya muda mfupi akafa.

Hata ingawa baadaye iligunduliwa kwamba kwa kweli Mauroy alikufa kutokana na kemikali yenye sumu, majaribio ya Denis ya kutumia damu ya mnyama yalizusha ubishi mkali sana katika Ufaransa. Hatimaye, mnamo mwaka wa 1670 hatua hiyo ilipigwa marufuku. Baada ya muda, Bunge la Uingereza, na hata papa alipiga marufuku hatua hiyo pia. Miaka 150 iliyofuata karibu utiaji-damu mishipani usahaulike.

Hatari za Mapema

Katika karne ya 19, utiaji-damu mishipani ulianza kutumiwa tena. Urudishaji huo uliongozwa na tabibu wa uzazi kutoka Uingereza anayeitwa James Blundell. Akitumia mbinu zilizoboreshwa na vifaa vya hali ya juu—na kusisitiza kwamba ni damu ya binadamu tu inayopasa kutumiwa—Blundell alifanya utiaji-damu mishipani ujulikane tena na umma.

Lakini mnamo mwaka wa 1873, F. Gesellius, daktari kutoka Poland, alipunguza mwendo wa kurudishwa kwa utiaji-damu mishipani kwa kutoa ugunduzi wenye kuogofya: Zaidi ya nusu ya visa vya utiaji-damu mishipani vilisababisha vifo. Baada ya kupata habari hizo, matabibu waheshimiwa walianza kushutumu hatua hiyo. Kwa mara nyingine tena, watu wakaacha kupendezwa na zoea la utiaji-damu mishipani.

Kisha, mnamo mwaka wa 1878, tabibu Mfaransa Georges Hayem alikamilisha mchanganyiko wa chumvi, ambao alidai ungeweza kutumiwa badala ya damu. Tofauti na damu, mchanganyiko huo wa chumvi haukuwa na athari zozote, haukuganda, na ilikuwa rahisi kuusafirisha. Basi inaeleweka ni kwa nini mchanganyiko wa chumvi wa Hayem ulianza kutumiwa sana. Hata hivyo, kwa kushangaza, punde si punde watu wakavutiwa na damu tena. Kwa nini?

Mnamo mwaka wa 1900, mwanapatholojia wa Austria Karl Landsteiner aligundua aina mbalimbali za damu, na akagundua kwamba aina moja ya damu haipatani na nyingine daima. Kwa hiyo haishangazi kwamba wakati uliopita utiaji-damu mishipani ulitokeza misiba mingi! Sasa mambo yangeweza kubadilishwa, kwa kuhakikisha kwamba damu ya mtoaji inapatana na ya mpokeaji. Wakiwa na ujuzi huo, matabibu walikuwa na imani mpya kuhusu utiaji-damu mishipani—wakati barabara kwa ajili ya Vita ya Ulimwengu ya Kwanza.

Utiaji-Damu Mishipani na Vita

Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, askari-jeshi waliojeruhiwa walitiwa damu kwa wingi. Bila shaka, damu huganda haraka, na wakati uliotangulia karibu ilikuwa haiwezekani kusafirisha damu kwenye uwanja wa mapigano. Lakini mapema katika karne ya 20, Dakt. Richard Lewisohn, wa Hospitali ya Mount Sinai huko New York City, alifanikiwa kufanyia majaribio dutu ya kuzuia kuganda inayoitwa sitrati natiri. Uvumbuzi huo wenye kusisimua ulionwa kuwa muujiza na madaktari fulani. “Ilikuwa kana kwamba karibu jua lilikuwa limefanywa lisimame tuli,” akaandika Dakt. Bertram M. Bernheim, tabibu mashuhuri wa wakati huo.

Uhitaji wa damu uliongezeka wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili. Umma ulijionea mabango mengi yenye shime kama vile “Toa Damu Sasa,” “Damu Yako Inaweza Kumwokoa,” na “Alitoa Damu Yake. Je, Utatoa Yako?” Watu wengi walitii mwito wa kutoa damu. Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, takriban lita 6,500,000 zilitolewa huko Marekani. Inakadiriwa kwamba katika London zaidi ya lita 260,000 zilikusanywa na kugawanywa. Bila shaka, utiaji-damu mishipani ulihusisha hatari kadhaa za afya, kama ilivyoonekana waziwazi punde si punde.

Maradhi Yanayopitishwa kwa Damu

Baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, maendeleo makubwa ya kitiba yaliwezesha upasuaji fulani ufanywe ambao hapo awali haukuwazika. Basi, kiwanda cha tufeni pote chenye kupata faida ya mabilioni ya dola kwa mwaka mmoja kiliibuka ili kutoa damu kwa ajili ya utiaji-damu mishipani ambao matabibu walianza kuuona kuwa kiwango cha upasuaji.

Hata hivyo, punde si punde, hangaiko juu ya maradhi yanayohusiana na kutiwa damu mishipani likajulikana sana. Kwa mfano, wakati wa Vita ya Korea, takriban asilimia 22 ya wale waliotiwa plazima walipatwa na mchochota wa ini—karibu mara tatu ya wale waliopatwa nao wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili. Kufikia miaka ya 1970, Vitovu vya Kudhibiti Maradhi vya Marekani vilikadiria idadi ya vifo vilivyosababishwa na utiaji-damu mishipani na maradhi ya mchochota wa ini kuwa 3,500 kwa mwaka. Wengine walikadiria tarakimu hiyo kuwa mara kumi zaidi.

Kwa sababu ya uchunguzi wa damu ulio bora na kuteua watoaji-damu kwa umakini, visa kadhaa vya ambukizo la mchochota wa ini-B vilipungua. Lakini aina mpya ya virusi ambavyo nyakati nyingine ni vyenye kufisha—mchochota wa ini C—vilisababisha vifo vingi. Inakadiriwa kwamba Wamarekani milioni nne waliambukizwa virusi hivyo, mamia ya maelfu kati yao kwa kutiwa damu mishipani. Ni kweli kwamba upimaji madhubuti hatimaye ulipunguza kuenea kwa mchochota wa ini C. Hata hivyo, wengine wanahofu kwamba hatari mpya zitatokea na zitajulikana tu baada ya kuchelewa mno.

Kashfa Nyingine: Damu Iliyoambukizwa HIV

Mnamo miaka ya 1980, ilijulikana kwamba damu inaweza kuambukizwa HIV, virusi inayosababisha UKIMWI. Mwanzoni, benki za damu zilichukizwa na wazo la kwamba damu yao ingeweza kuwa imeambukizwa. Hapo mwanzoni wengi wao walishuku tisho la HIV. Kwa mujibu wa Dakt. Bruce Evatt, “ilikuwa kana kwamba mtu fulani alikuwa amepotea kutoka jangwani na kusema, ‘nimeona kiumbe kutoka anga la nje.’ Walisikia, lakini wakakosa kuamini.”

Hata hivyo, kumekuwa na kashfa katika nchi nyingi ambazo zimefunua damu iliyoambukizwa HIV. Inakadiriwa kwamba katika Ufaransa, kati ya watu 6,000 na 8,000 waliambukizwa HIV kwa kutiwa damu mishipani baina ya mwaka wa 1982 na 1985. Utiaji-damu mishipani huchangia asilimia 10 ya maambukizo ya HIV katika Afrika kote na asilimia 40 ya visa vya UKIMWI huko Pakistan. Leo, kwa sababu njia ya kuchunguza damu imeboreshwa, kupitishwa kwa HIV kwa kutiwa damu mishipani ni jambo lililo nadra katika nchi zilizositawi. Hata hivyo, kupitishwa kwa HIV kwa njia hiyo kwaendelea kuwa tatizo miongoni mwa mataifa yanayositawi ambayo hayana mbinu za kuchunguza damu.

Basi yaeleweka ni kwa nini katika miaka ya karibuni watu wengi wamependezwa zaidi na tiba na upasuaji bila damu. Lakini je, hii ni njia badala iliyo salama?

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Utiaji-Damu Mishipani—Hakuna Kiwango cha Kitiba

Kila mwaka huko Marekani pekee, zaidi ya chembe nyekundu za damu 11,000,000 hutiwa ndani ya mishipa ya wagonjwa 3,000,000. Kwa kuzingatia idadi hiyo kubwa, mtu angedhani kwamba kuna kiwango mahususi miongoni mwa matabibu cha utiaji-damu mishipani. Hata hivyo, jarida la The New England Journal of Medicine lasema kwamba kwa kushangaza kuna habari kidogo “ya kuelekeza maamuzi yanayohusu utiaji-damu mishipani.” Kwa kweli, kuna kubadilika-badilika katika kazi hiyo, si kuhusu tu ni damu gani hususa itakayotiwa mishipani na kiasi chake bali pia ikiwa utiaji-damu mishipani utafanywa kwa vyovyote vile. “Utiaji-damu mishipani wategemea daktari, wala si mgonjwa,” lasema jarida la kitiba Acta Anæsthesiologica Belgica. Kwa kuzingatia yaliyo juu, haishangazi hata kidogo kwamba uchunguzi uliochapishwa katika jarida The New England Journal of Medicine ulifunua kwamba “asilimia 66 ya visa vya utiaji-damu mishipani hufanywa kwa njia isiyofaa.”

[Picha katika ukurasa wa 5]

Uhitaji wa damu uliongezeka wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili

[Hisani]

Imperial War Museum, London

U.S. National Archives photos