Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Bratislava Kutoka Kuwa Kivuko cha Kale cha Mto Hadi Kuwa Jiji Kuu la Kisasa

Bratislava Kutoka Kuwa Kivuko cha Kale cha Mto Hadi Kuwa Jiji Kuu la Kisasa

Bratislava Kutoka Kuwa Kivuko cha Kale cha Mto Hadi Kuwa Jiji Kuu la Kisasa

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA SLOVAKIA

HEBU wazia kwamba unaweza kurudi nyuma hadi mwaka wa 1741. Hali ni yenye kusisimua sana. Mishindo ya tarumbeta yaweza kusikiwa huku watu wakisukumana ili wakaribie zaidi barabara ambayo karibu maandamano yapitie. Wakulima wakiwa wamevalia mavazi yao bora zaidi na wakwasi wenye kiburi wakiwa wamevalia mtindo wa karibuni zaidi wako hapa, na vilevile wanaume wenye sifa ambao wamekuja kujionea na kuonekana wako hapa. Wajumbe wa kifalme wanagawanya sarafu za dhahabu na za fedha zenye picha ya bibi mchanga, huku watu wakipiga kelele kwa msisimko. Kwa nini rabsha yote hii? Maria Theresa, dyuki-mkuu wa kike wa huko Austria, anaelekea jijini akavikwe taji ili awe malkia mpya wa Hungaria.

Na turudi wakati wa sasa. Kama ungetaka kutembelea mahali palipo na sherehe hii muhimu ya kutawazwa, ungeenda wapi? Si Vienna, ambapo leo watalii wengi hupendezwa na jumba la kifalme la Maria Theresa, wala si Budapest, jiji kuu la Hungaria ya kisasa. Ingekubidi utembelee Bratislava, jiji lililo kwenye Mto Danube, zapata kilometa 56 mashariki mwa Vienna.

Bratislava la leo, jiji lenye watu wapatao nusu milioni hivi, ni jiji kuu la Slovakia yenye kuvutia sana. Linapolinganishwa na majiji makuu jirani ya—Budapest, Vienna, na Prague—sasa Bratislava laonekana kuwa changa. Hata hivyo, kwa zaidi ya karne mbili, lilikuwa jiji kuu la Hungaria na lilifurahia sifa yote inayohusiana na daraja hilo la pekee. Kwa kweli, kutawazwa kwa watawala 11 wa Hungaria kulifanyiwa katika jiji hilo. Lakini ni nini kilicholifanya liwe la pekee sana?

Kijiji cha Kale

Bratislava hujisifia sehemu yenye manufaa ya Danube, mto wa pili kwa urefu katika Ulaya. Zamani, Mto Danube ulitiririka polepole pasipo kina katika sehemu hii na kufanyiza kivuko cha asili. Watu pamoja na wanyama wao na mikokoteni, walivuka mto huo kwenye sehemu hiyo muda mrefu kabla ya madaraja kuunganisha fuko zake. Hivyo, tokea nyakati za kale eneo ambalo sasa ni Bratislava lilikuwa kivuko cha njia chenye shughuli nyingi. Mapema mwaka wa 1500 K.W.K., mojawapo ya njia za Amber Routes zilizo muhimu kwa biashara, zinazounganisha kaskazini na kusini mwa Ulaya, ilipitia jiji hilo. Baadaye msongamano kwenye kivuko ulidhibitiwa na ngome iliyo kwenye kilima cha karibu ambapo Kasri ya Bratislava ipo sasa.

Kama ungeweza kurudi nyuma kwa wakati, ungekutana na nani kwa ghafula kwenye kivuko hicho? Kama ungefika yapata karne ya nne K.W.K., ungekaribishwa na Waseltiki ambao walifanya sehemu hii kuwa kituo cha utamaduni wao. Kilima hicho kilitumika kama namna fulani ya akropoli ya jamii ya Waseltiki wenyeji, ambao walitokeza ufinyanzi na kutengeneza sarafu.

Vipi kama ungetembea mwanzoni mwa Wakati wetu wa Kawaida? Kama ungejua Kilatini, labda ungeweza kuzungumza na wenyeji wa hapo, kwa kuwa wakati huo Waroma walikuwa wamepanua mipaka yao ya kaskazini hadi Danube. Hata hivyo, wakati uleule, labda pia ungekutana na Wajerumani wakifika kutoka magharibi.

Kama ungepanga ziara yako kuelekea Enzi za Kati, tuseme katika karne ya nane, ungejikuta katika mchanganyiko mkubwa wa wahamiaji. Kufikia wakati huo, ule uliokuja kuitwa Uhamaji Mkubwa ulikuwa umetokea, na Waslavoni kutoka mashariki walikuwa wameanza kukaa katika eneo hilo. Wahungaria walikuwa wamesitawisha makao yao kusini na pia kupenya katika eneo la Bratislava. Lakini kwa njia fulani uvutano wa Kislavoni ulidumu. Uthibitisho wa hilo ni jina la Kislavoni la kasri ya kwanza ya eneo hilo, ambayo ilijengwa katika karne ya kumi. Iliitwa Brezalauspurc, kumaanisha “Kasri ya Braslav”—yasemekana ilipewa jina kutokana na ofisa mmoja wa jeshi mwenye cheo cha juu. Kutokana na maelezo hayo, likapatikana jina Bratislava la Kislovaki.

Jiji la Enzi ya Kati

Halafu, nchi ambayo sasa yaitwa Slovakia ikawa sehemu ya Hungaria. Simulizi la historia lenye tarehe ya kuanzia 1211 K.W.K. huona Kasri ya Bratislava kuwa kasri iliyoimarishwa zaidi katika Hungaria. Miaka 30 baadaye, makadirio hayo yalithibitika kuwa ya kweli wakati kasri hiyo iliweza kuhimili shambulizi la wavamizi wa Tatar. Mafanikio hayo yalichochea ukuzi wa kijiji kilichokuwa karibu na kasri, na mwaka wa 1291, Mfalme Ondrej wa Tatu wa Hungaria aliupa mji mapendeleo kamili ukiwa manispaa. Hivyo, raia zake walipata haki ya kupigia kura meya wao wenyewe, kusafirisha bidhaa zao kupitia Mto Danube, na kufanya biashara kwa uhuru “kwenye maji na kwenye nchi kavu.” Kwa kuwa mashamba ya mizabibu yalisitawi kwenye miteremko yenye jua ya jiji, haki za raia za kuuza divai waliyotengenezea nyumbani kwao wenyewe zilithaminiwa sana.

Baadaye wafalme Wahungaria walilipa jiji mapendeleo zaidi, ambayo yalichangia upanuzi zaidi. Mwaka wa 1526, Bratislava lilianza utawala wake mrefu likiwa jiji kuu la Hungaria, hadi mwaka wa 1784. Wakati uleule, mchanganyiko wa kikabila wa Bratislava ukawa wa namna nyingi. Idadi yake ya Waslavoni na Wahungaria wengi iliongezeka wakati Wajerumani na Wayahudi walipomiminika kwa wingi. Katika karne ya 17, kadiri utawala wa Uturuki ulivyopanuka kuelekea magharibi na kaskazini, Wakroatia wengi walikimbilia eneo la Bratislava, kama walivyofanya wahamishwa Wacheki waliokimbia Vita ya Miaka 30 kati ya Wakatoliki na Waprotestanti magharibi ya mbali huko Ulaya.

Bratislava Katika Karne ya 20

Mwanzoni mwa karne ya 20, Bratislava lilikuwa limekuwa jiji la kimataifa, na tamaduni mbalimbali. Wakati huo njia hakika ya kupata kile ulichohitaji dukani ilikuwa ni kukiomba kwa Kijerumani au Kihungaria. Lakini Wacheki na Warumania (Wajipsi) pia walitimiza fungu muhimu, kama ilivyofanya jamii ya Kiyahudi. Kabla ya Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, ni karibu asilimia 15 tu ya idadi ya watu iliyokuwa Waslovaki. Lakini kufikia mwaka wa 1921, Waslovaki wakawa wengi zaidi ya watu wa mataifa yale mengine ya jiji hilo.

Upesi tisho la Vita ya Ulimwengu ya Pili likasambaa Ulaya. Ndivyo ilivyoanza sehemu yenye kuhuzunisha ya historia ya Bratislava, ambayo ilivuruga upatano wa kikabila wa jiji hilo. Kwanza, Wacheki walilazimishwa kuondoka. Kisha Warumania na wakazi Wayahudi wakafukuzwa nchini, na hatimaye maelfu wakafa katika kambi za mateso. Baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili kwisha, wakazi wengi waliosema Kijerumani pia walifukuzwa. Hatimaye, washiriki wa kila kikundi cha kikabila walirudi kwenye miji yao ya zamani, na kuwapo kwao kungali kwasitawisha mazingira ya Bratislava.

Kutembelea Bratislava Leo

Kwa nini usijiunge nasi tufanyapo matembezi mafupi katika Bratislava la leo? Kwanza, twatembelea Kasri ya Bratislava iliyojengwa upya. Kutoka kwenye bustani ya kasri, twafurahia mandhari yenye kupendeza ya jiji pande zote mbili za Mto Danube.

Kwenye mteremko wa kilima, chini tu ya eneo la kasri, twajikuta katika Jiji la Zamani, kituo cha historia cha Bratislava. Tukitembea kwenye barabara nyembamba zenye unamna-namna, twahisi kana kwamba twaishi katika karne zilizopita. Twapendezwa na usanifu wenye kuvutia wa majengo ya majumba ya wafalme na nyumba za wakwasi. Ukipenda, twaweza kutua kwenye mkahawa mmoja wa kihistoria tupate kikombe cha kahawa au chai na baadhi ya vitumbua vyenye kupendwa sana vya Bratislava vilivyojazwa walnuts au mbegu za poppy.

Mwaka wote mzima, wageni hufurahia kutembea-tembea ufukoni mwa Danube karibu na Jiji la Zamani. Wakiwa hapo, hawawezi kukosa ishara ya Bratislava ya kisasa—lile Daraja Jipya lenye mkahawa ulio juu ya mnara unaoegama. Usanifu huo huleta wazo la kwamba mkahawa huo unazunguka hewani juu ya sehemu ya nyumba ya Petržalka upande wa pili wa mto.

Ikiwa wafikiri kwamba kuna ujenzi mwingi unaoendelea Bratislava, hujakosea. Mbali na sehemu zilizojengwa karibuni za Jiji la Zamani, majengo yenye kupendeza ya chuma na glasi yalienea upesi miaka ya 1990, na mengi zaidi yatarajiwa kujengwa. Ni ofisi hizo, vituo hivyo vya kibiashara, na mabenki yanayolipa jiji sura yake ya kisasa.

Bila shaka, utapenda kuwa na kitu chenye kuvutia cha ukumbusho wa ziara yako. Kwa hiyo, twaweza kupitia kwenye maduka yanayouza vitu vilivyotengenezwa kwa mikono, kama vile vitambaa vya mezani vya lesi au wanasesere waliovalishwa nguo za kitamaduni. Au ukipenda, twaweza kwenda kwenye soko lililo wazi liitwalo Main Square Market, ambapo unaweza kununua vitu kama vile ambavyo wakazi wa Bratislava wamekuwa wakinunua kwa karne nyingi. Labda wewe pia ungetaka kutembelea ofisi ya tawi maridadi ya Watch Tower Society iliyo katika jiji hili.

Labda siku moja utatembelea Bratislava kihalisi. Ukifanya hivyo, bila shaka utafurahia jiji hilo kuu la kisasa lenye unamna-namna ambalo lilianzia kwenye kivuko cha kale cha mto.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Maria Theresa

[Hisani]

North Wind Picture Archives

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Ukumbi wa Maonyesho wa Kitaifa wa Slovak

[Picha katika ukurasa wa 17]

Barabara moja katika Jiji la Zamani

[Picha katika ukurasa wa 18]

Daraja Jipya na mnara unaoegama

[Hisani ya Picha katika kurasa za 15-18]

Ofisi ya tawi na Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova