Kuchora Ramani za Mbingu Wakati Huo na Sasa
Kuchora Ramani za Mbingu Wakati Huo na Sasa
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UHOLANZI
MWONO wa nyota zinazosambaa kwenye anga nyeusi ya mahameli mara nyingi imemtia mwanadamu kicho, na katika historia yote imemchochea adhihirishe kuvutiwa kwake na Muumba wa uzuri wa namna hiyo. Zamani za kale, mshairi mmoja alisema hivi kwa mkazo: “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, na anga laitangaza kazi ya mikono yake.” (Zaburi 19:1) Hata hivyo, watazamaji wa kale wa anga la usiku waliona mengi zaidi ya uzuri.
Kutafuta Mifano Kwenye Anga
Katika nyakati zilizopita waastronomia waligundua kwamba gimba zima la nyota ni kana kwamba linasonga kwa njia ya utaratibu. Ijapokuwa nyota zilisafiri kwenye anga kutoka mashariki hadi magharibi, hazikubadili mahali pao kuelekeana. * Yaani, kila usiku kikundi kilekile hususa cha nyota kilionekana. Kwa kuwa mwanadamu alitaka kutokeza utaratibu fulani kwenye nyota hizo zisizo na hesabu, aliunganisha nyota katika vikundi. Kwa kuwazia kidogo, vikundi hivyo vilifanana na wanyama, watu, au vitu visivyo hai. Kwa njia hiyo kukawa na zoea la kuona idadi hususa ya nyota kuwa kundinyota.
Baadhi ya makundi ya nyota tunayoyajua leo yalifafanuliwa kwanza katika Babiloni ya kale. Miongoni mwa hayo kuna makundi ya nyota 12 yanayowakilisha ishara za nyota za unajimu. Makundi hayo yalichangia—na bado yanachangia fungu la maana katika unajimu, uaguzi wa athari inayodhaniwa kuwa hutokezwa na nyota kuelekea mambo ya binadamu. Hata hivyo, kutazama ndege kwenye nyota, ni jambo linaloshutumiwa na Biblia. (Kumbukumbu la Torati 18:10-12) Hata hivyo, waabudu wa Yehova Mungu walitambua kuwepo kwa makundi ya nyota. Mathalani, kitabu cha Biblia cha Ayubu, husema juu ya Yehova kuwa “afanyaye hizo nyota za Dubu, na Orioni, na hicho Kilimia.”—Ayubu 9:9.
Majina ya makundi mengi ya nyota tunayoyajua leo yanatokana na mithiolojia ya Kigiriki. Majina kama vile Cepheus, Cassiopeia, Andromeda, na Hercules bado yaweza kupatikana kwenye chati za kisasa za nyota.
Chati za Kale za Nyota
Yapata mwaka wa 150 W.K., mwastronomia Mgiriki Ptolemi alitoa muhtasari wa ujuzi wa astronomia uliojulikana wakati wake. Muhtasari huo, wenye kichwa Almagest, una orodha ya makundi 48 ya nyota. Chati na vitabu vya ramani ya anga vilivyochapwa katika karne nyingi baada ya Ptolemi kwa kawaida vilikuwa na makundi yaleyale 48 ya nyota. Kwa hakika, hadi kufikia karne ya 16 hivi, idadi ya makundi ya nyota haikubadilika. * Baadaye, makundi mengine 40 ya nyota yakaongezwa. Mnamo mwaka wa 1922 shirika la International Astronomical Union lilianza kutumia rasmi orodha ya makundi haya 88 ya nyota.
Mbali na makundi ya nyota, kichapo cha Ptolemi chatia ndani orodha ya nyota zaidi ya elfu moja, yenye habari kuhusu mng’ao wao na mahali pake kwenye anga. Ptolemi haonyeshi tu mahali ilipo nyota kwenye longitudo na latitudo ya kimbingu bali pia aandaa habari ya ziada. Mathalani, nyota moja katika Ursa Major, au kundinyota la Great Bear, inafafanuliwa kuwa “nyota iliyo mwanzoni mwa mkia,” na mahali ilipo nyotamkia panaitwa “upande wa kushoto wa goti la kulia la Andromeda.” Hivyo, “kila mwastronomia hodari,” chasema kitabu kimoja cha mafundisho, “alihitaji kujua anatomia ya kimbingu!”
Hata hivyo, kwa nini, vikundi vingi vya nyota vya zamani hupatikana kaskazini mwa anga? Hii ni kwa sababu zoea la kuona vikundi fulani vya nyota kuwa kundinyota lilianzia huko Mediterania, ambapo anga la kaskazini huonekana, aeleza msanifu-ramani za anga. Ni baadaye tu ndipo mwanadamu alipoanza kuvinjari kusini mwa anga na kugundua makundi mapya ya nyota. Baadhi ya makundi ya nyota yaliyogunduliwa hivi karibuni yana majina kama vile Tanuri la Kemikali, Saa ya Pinduli, Hadubini, na Darubini-Upeo.
“Anga la Kikristo Lenye Nyota Nyingi”
Mnamo mwaka wa 1627, msomi Mjerumani Julius Schiller alichapisha kitabu cha ramani za nyota chenye kichwa Coelum Stellatum Christianum (Anga la Kikristo Lenye Nyota Nyingi). Alihisi kwamba wakati ulikuwa umewadia wa kumaliza upagani kwenye mbingu. Hivyo, alianza kuondoa mifano ya kipagani kutoka kwenye anga na akaweka vitu vya Biblia mahali pake. Kitabu The Mapping of the Heavens chaeleza kwamba aligawia “sehemu ya kaskazini mwa mbingu Agano Jipya na ile iliyoko kusini mwake Agano la Kale.” “Kizio cha kusini cha Schiller kiligeuzwa kuwa mfuatano wa habari za Agano la Kale—Yobu achukua mahali pa Mhindi na Tausi, na Kentauro ageuzwa kuwa Abrahamu na Isaka.” Katika Kizio cha Kaskazini, “Cassiopeia awa Maria Magdalen, Perseus awa Mt. Paulo, huku mahali pa ishara kumi na mbili za Nyota za Unajimu pachukuliwa kwa urahisi na wale mitume kumi na wawili.”
Ni kundinyota moja tu lililookoka utakasaji
huo. Kundi hilo lilikuwa Columba (Njiwa), linalodhaniwa kuwa linawakilisha njiwa aliyetumwa na Noa kutafuta nchi kavu.Ramani Zinazobadilika
Baada ya muda, chati za nyota zilibadilika. Katika karne ya 17, baada ya kuvumbuliwa kwa darubini-upeo, kulitokea uhitaji wa chati zilizoandaa msimamo ulio sahihi wa mahali zilipo nyota. Kwa kuongezea, madoido yaliyopangwa kwa uangalifu ambayo yalijaza chati za zamani yakapoteza umashuhuri wake na hatimaye yakatoweka. Leo, vitabu vingi vya ramani za nyota vina nyota peke yake, vikundi vya nyota, jamii za nyota, galaksi, na vitu vingine vinavyovutia mtazamaji kwenye anga la usiku.
Katikati ya karne ya 19, orodha za vitu zenye mambo mengi zilianza kufanyizwa. Mmojawapo wa watangulizi katika uwanja huu alikuwa mwastronomia Mjerumani Friedrich Wilhelm Argelander. Akishirikiana na wasaidizi kadhaa, alianza mradi mkubwa sana wa kutengeneza orodha ya nyota zilizo kwenye anga la kaskazini. Kwa kutumia darubini-upeo, walipata takriban nyota 325,000 na kupima mahali zilipo na kiasi cha mng’ao wa kila moja. Kwa kuwa mahali pa kuangalia nyota ambapo walifanyia kazi palikuwa katika jiji la Ujerumani la Bonn, orodha hiyo ilikuja kujulikana kuwa Bonner Durchmusterung (Ukaguzi wa Jumla wa Bonn). Ilichapishwa mwaka wa 1863. Baada ya kifo cha Argelander, kazi yake iliendelezwa na mmojawapo wa wasaidizi wake. Alichora ramani ya nyota zilizo sehemu ya kusini mwa anga na kuchapisha kitabu chake kikiwa na kichwa Südliche Bonner Durchmusterung (Ukaguzi wa Jumla wa Kusini mwa Bonn). Ukaguzi wa mwisho ulichapishwa mnamo mwaka wa 1930. Ulitolewa huko Cordoba, Argentina. Orodha hizo zingali na thamani hadi leo hii.
Sasa na Wakati Ujao
Uchoraji-ramani wa Argelander pamoja na wasaidizi wake ulifuatiwa na orodha zilizokuwa nzuri hata zaidi. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni zaidi, baada ya darubini-upeo kutokezwa, kazi kubwa za kuchora ramani ambazo hazikuwa zimesikiwa ziliwezekana. Kwa kutumia Darubini-Upeo ya Angani ya Hubble, sasa waastronomia wametengeneza orodha yenye nyota zipatazo milioni 15!
Maendeleo ambayo yamefanywa hivi karibuni katika kuchora ramani za mbingu ni kuchapishwa kwa orodha mbili mpya na Shirika la Anga la Ulaya. Zategemea mambo yaliyoonwa kwa kutumia darubini-upeo za anga za setilaiti ya Hipparcos. Kufikia sasa orodha hizi zina usahihi usio na kifani. Vitabu vipya vya ramani za nyota vimechapishwa, kwa kutegemea orodha hizo. Mojawapo ni kitabu cha ramani chenye mambo mengi kilicho katika mabuku matatu kinachoitwa Millennium Star Atlas.
Kichwa hicho chaweza kuwakumbusha wasomaji wa Biblia juu ya Milenia, au Utawala wa Miaka Elfu wa Kristo wenye amani, unaotajwa katika Biblia. (Ufunuo 20:4) Wakati huo bila shaka mwanadamu atajifunza mengi zaidi kuhusu ulimwengu wote mzima wenye kutisha, ambao hata vitabu vikubwa zaidi vya ramani vya leo vyaweza kuwa sehemu ndogo tu yake.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 5 Watu wa kale hawakujua kwamba kusafiri kwa nyota husababishwa na kuzunguka kwa dunia kwenye mihimili yake. Kwa sababu hiyo hiyo, jua huonekana likichomoza na kutua.
^ fu. 9 Makundi haya 48 ya nyota yalijulikana katika Mesopotamia, Mediterania, na Ulaya. Baadaye, yalijulikana pia na wale waliohamia Amerika Kaskazini na Australia. Hata hivyo, watu wengine, kama vile Wachina na Wahindi wa Amerika ya Kaskazini walifuata mpangilio tofauti wa kugawa anga.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Chati ya Nyota ya Apia, 1540
[Hisani]
By permission of the British Library (Maps C.6.d.5.: Apian’s Star Chart)
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kizio cha Kusini kama kilivyochorwa katika karne ya 19
[Hisani]
© 1998 Visual Language
[Picha katika ukurasa wa 27]
Kundinyota la Orion kama lionekanavyo kwenye chati ya kisasa ya nyota
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26-27]
Picha zilizo nyuma ya maandishi kwenye ukurasa wa 25-27: Courtesy of ROE/Anglo-Australian Observatory, photograph by David Malin