Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuiga Ubuni Ajabu wa Uhai

Kuiga Ubuni Ajabu wa Uhai

Kuiga Ubuni Ajabu wa Uhai

Watoto wanaoanza kutembea huanguka ghafula na kujigonga vichwa. Watoto wakubwa zaidi huanguka kutoka mitini na juu ya baiskeli. Wanariadha hugongana uwanjani. Madereva hupatwa na aksidenti nyingi barabarani. Lakini, licha ya visa hivyo vyote vya kuanguka, kugongana, na aksidenti, mara nyingi sisi hunusurika bila majeraha mabaya. Sisi huelekea kupuuza ugumu na ujirekebishaji wa miili yetu. Lakini wanasayansi wameanza kugundua kwamba kwa kweli tulibuniwa kwa njia bora ajabu, kuanzia kwa mifupa hadi kwa ngozi yetu.

VITU vyote vya kiasili—vina nguvu na uthabiti—vijapokuwa na uzito wa kadiri. Miche myororo hupenya nyufa kwenye saruji na miamba na hupasua kabisa nyufa hizo inapokomaa. Miti inaweza kustahimili upepo unaong’oa nguzo za umeme na kubomoa kabisa nyumba. Vigogota hutoboa mbao kwa nguvu ziwezazo kusaga kabisa ubongo wa kawaida. Ngozi ya mamba na aligeta haipenyi mikuki, mishale, na hata risasi. (Linganisha Ayubu 41:1, 26.) Mambo hayo yamewastaajabisha na kuwakanganya wanadamu kwa maelfu ya miaka.

Maendeleo makubwa ya tekinolojia ambayo yamefanywa kwa miaka 40 iliyopita, yamewaandalia wanasayansi vifaa vipya vya kutumia wanapochunguza mafumbo ya ubuni huu, hasa ulio katika chembe hai. Hadubini hufunua ubora unaoshangaza na utata wenye kustaajabisha wa ubuni. Hata hivyo, lengo la sayansi si kufunua tu siri ya vitu bora vya kiasili bali kuviiga—angalau kuiga kanuni yake. Fani hii ya elimu imetokeza matumaini kiasi cha kwamba imeanzisha sayansi mpya inayoitwa biomimetics, kutokana na neno la Kigiriki biʹos, limaanishalo “uhai,” na miʹme·sis, limaanishalo “mwigo.”

Biomimetics Yaahidi Ulimwengu Bora

“Biomimetics ni elimu ya miundo ya kibiolojia [na] utendaji wake,” chaeleza kitabu Biomimetics: Design and Processing of Materials. Chaongezea kwamba kusudi la elimu hii ni ‘kubuni mawazo mapya na kutumia mawazo hayo ili kutokeza mifumo sanisia iliyo sawa na mifumo ya kibiolojia.’

Mwanasayansi Stephen Wainwright asema kwamba “biomimetics itatia ndani biolojia ya molekuli na itachukua mahali pake na kuwa sayansi ya kibiolojia ya Karne ya 21 iliyo ngumu na muhimu zaidi.” Profesa Mehmet Sarikaya adai hivi: “Tuko kwenye ukingo wa mabadiliko ya vitu ambayo yatalingana na Enzi ya Chuma na Mvuvumko wa Kiviwanda. Tunapiga hatua kufikia enzi mpya ya vitu. Nafikiri kwamba biomimetics itabadili kabisa namna tunavyoishi katika karne inayofuata.”

Kwa kweli, tayari imeanza kubadili ulimwengu wetu, kama tutakavyoona. Lakini kwanza, acheni tupitie kwa ufupi baadhi ya vitu vichache vya kustaajabisha visivyofahamika ambavyo vinachunguzwa sana na wanasayansi. Tutachunguza pia maana mantiki ya neno “ubuni” na jinsi ambavyo linatoa kusudi la ulimwengu wa kustaajabisha unaotuzunguka.