Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Zawadi ya Kifalme” ya Joachim Barrande

“Zawadi ya Kifalme” ya Joachim Barrande

“Zawadi ya Kifalme” ya Joachim Barrande

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA JAMHURI YA CHEKI

“NI ZAIDI ya zawadi ya kifalme, heshima kubwa zaidi iliyotolewa kwa taifa la Cheki!” Hivyo ndivyo mwandishi mmoja wa habari alivyoueleza urithi uliotolewa na Joachim Barrande, mwanapaleontolojia mashuhuri wa karne ya 19, kwa Jumba la Makumbusho ya Taifa la Cheki. “Zawadi ya kifalme” ya Barrande kwa watu wa Cheki ilitia ndani mkusanyo wa zaidi ya masanduku 1,200 yaliyojaa visukuku ambavyo alikuwa ametumia miongo mingi kuvikusanya, kuvichunguza na kuviainisha. Ingawa huenda ukakosa shauku kuelekea mkusanyo wa visukuku vya zamani, zawadi ya Barrande ni yenye thamani zaidi kwa wanapaleontolojia kuliko dhahabu iliyogunduliwa!

Mwanapaleontolojia ni mwanasayansi ambaye hutumia visukuku kuchunguza uhai katika vipindi vilivyopita vya jiolojia. Kwa kulinganishwa, paleontolojia ni sayansi mpya. Katika Enzi za Kati, visukuku vilionwa kuwa “mizaha ya maumbile” au vilifikiriwa kuwa mabaki ya majoka wakubwa mno. Hata hivyo, kufikia karne ya 18, watu wa tabaka za juu walikuwa wameanza kupendezwa na kukusanya visukuku. Pia wanasayansi katika nchi nyingi wakaanza kupendezwa na kuchunguza visukuku. Joachim Barrande alikuwa mmoja wao. Ni mambo gani tujuayo kuhusu Barrande, na alichangia nini katika uwanja wa paleontolojia? Kwa kuwa aliishi wakati uleule na Charles Darwin, maoni ya Barrande yalikuwa nini kuhusu nadharia ya mageuzi ya Darwin?

Barrande Abadili Kazi-Maisha Yake

Joachim Barrande alizaliwa katika mwaka wa 1799 huko Saugues, mji mdogo katika kusini mwa Ufaransa. Alisomea uhandisi huko Paris, akawa mtaalamu wa kujenga barabara na madaraja. Wakati huohuo, alifanya mtaala wa sayansi ya asili. Muda si muda ikaonekana wazi kwamba alikuwa na kipawa katika uwanja huo. Baada ya kuhitimu, Barrande alianza kufanya kazi ya uhandisi, lakini familia ya kifalme ya Ufaransa ilipoona kipawa chake, alialikwa awe mfunzi wa mjukuu wa kiume wa Mfalme Charles wa 10. Somo lilikuwa sayansi ya asili. Baada ya mapinduzi ya mwaka wa 1830 huko Ufaransa, familia ya kifalme ilipelekwa uhamishoni na hatimaye ikaenda huko Bohemia. Barrande alijiunga nao huko. Barrande alianza tena kazi ya uhandisi huko Prague, mji mkuu wa Bohemia.

Akiwa mtaalamu wa kujenga barabara na madaraja, Barrande alipewa mgawo wa kukagua sehemu za mashambani zilizozunguka Prague kwa ajili ya reli ya magari ya kuvutwa na farasi iliyokusudiwa kujengwa. Alipokuwa akiendelea na kazi yake Barrande aliona kwamba kulikuwa na visukuku vingi sana katika eneo hilo. Alipochunguza kwa makini zaidi alishangaa kugundua ufanano wenye kuvutia kati ya matabaka ya Bohemia na matabaka ya Uingereza. Shauku yake kuelekea sayansi ya asili ikaamshwa tena, Barrande akaacha kabisa kazi ya uhandisi, na kwa miaka 44 iliyofuata, alijitoa kuchunguza paleontolojia na jiolojia.

Darasa la Barrande lilikuwa sehemu za mashambani za Bohemia ya kati zilizokuwa na visukuku vingi. Kila siku kulikuwa na uvumbuzi mpya wa uzuri na unamna-namna usio na kifani. Kufikia mwaka wa 1846 alikuwa tayari kuchapisha matokeo ya kwanza ya utafiti wake. Katika kazi yake alieleza na kuainisha aina zilizotoweka za athropodi wa majini, ambao wakati mmoja waliishi chini ya bahari.

Barrande aliendelea kukusanya na kuchunguza visukuku. Kisha katika mwaka wa 1852, alichapisha buku la kwanza la masimulizi ya viumbe au tasnifu yenye kichwa The Silurian System of Central Bohemia. * Buku la Kwanza lilizungumzia athropodi wa majini. Hili lilifuatwa na mabuku mengine yaliyozungumzia krasteshia, chondrichthye, cephalopod, lamellibranch, na viumbehai wengine waliofanywa kuwa visukuku. Katika muda wote wa maisha yake alichapisha mabuku 22 ambapo alieleza kinaganaga zaidi ya aina 3,500. Vitabu hivyo ni mojawapo ya masimulizi yenye habari nyingi zaidi kuhusu viumbe katika uwanja wa paleontolojia.

Mwangalifu Sana na Mwenye Nidhamu

Njia za Barrande zilimtofautisha na watafiti wengine. Alitumia elimu ya uhandisi kufanya kazi yake ya mwanaviumbe. Akiwa msanii hangeweza kukubali mikokotoo au michoro isiyo sahihi. Akiwa mwanapaleontolojia, alijitahidi sana kufikia kiwango cha juu katika michoro yake, akijitahidi sana kuhakikisha kwamba ilikuwa sahihi kabisa. Yeye binafsi alifanya upya michoro iliyotiwa ndani katika masimulizi ya viumbe hata ingawa nakala za awali zilikuwa zimechorwa na msanii stadi.

Hata hivyo, uangalifu mkubwa wa Barrande haukuhusu tu kwa michoro yake. Baada ya kila buku la masimulizi ya viumbe kuchapishwa, yeye binafsi alichunguza maandishi yake. Ikiwa hakupendezwa, alirudisha sehemu ambazo hazikumridhisha zikachapishwe tena. Mradi wa Barrande ulikuwa kuhakikisha kwamba kila kitabu alichochapisha kilikuwa sahihi kabisa iwezekanavyo. Kwa kupendeza alifaulu. Leo karibu miaka 150 baadaye, watafiti wangali wanatumia Silurian System kuwa kitabu cha marejezo.

Namna Gani Mageuzi?

Wakati kitabu cha Charles Darwin The Origin of Species kilipochapishwa katika mwaka wa 1859, wanasayansi wengi walikubali nadharia ya mageuzi. Hata hivyo, Barrande hakuikubali. Kuanzia mwanzo, aliikataa nadharia ya mageuzi kwa sababu hakuona jambo lolote katika visukuku ambalo lilithibitisha kwamba nadharia hiyo ni ya kweli. Barrande alisema kwamba kusudi la kazi yake lilikuwa ni “kutafuta uhalisi na sio kujenga nadharia za muda mfupi tu.” (Italiki ni zetu.) Kwa kweli, katika ukurasa wa kwanza wa kila buku la Silurian System, aliandika wito: “C’est ce que j’ai vu” (Haya ndiyo nimeona).

Barrande aligundua tofauti katika miili ya wanyama wengi waliokuwa katika hatua mbalimbali za ukuzi. Hata hivyo, alikata kauli kwa usahihi kwamba viumbe wote walikuwa wa aina moja lakini katika hatua tofauti ya ukuzi. Hakuona uthibitisho wowote kwamba aina moja ya mnyama iligeuka na kuwa aina nyingine. Kikitoa muhtasari juu ya falsafa ya Barrande, kitabu A Petrified World chasema: “Kazi yote ya Barrande . . . imejengwa juu ya mambo ya hakika, na hiyo ndiyo sehemu kuu ya maana zaidi. Katika hatua hii ya utafiti wa msingi hakuna nafasi ya kuwazia au kukisia au hata kwa nadharia za ujumla tu.”

Mwanamume Mnyenyekevu Atoa “Zawadi ya Kifalme”

Ijapokuwa Barrande alifaulu sana, hakuwa mwenye kiburi wala kukosa uaminifu. Ingawa alijihisi huru akiwa pamoja na watu wenye akili wa Ulaya na aliweza kuzungumza lugha mbalimbali, alichangamana na watu wengine pia bila shida. Alijifunza lugha ya Cheki ili awe na uhusiano wa karibu zaidi na watu wa huko. Hili lilimsaidia katika kazi yake kwani lilimwezesha kuwasiliana na wachimba-mawe waliomsaidia kupata violezo vipya katika mkusanyo wake.

Barrande alikuwa mtu wa kidini, na mambo aliyoona kutokana na vitu vya asili yaliimarisha imani yake katika Mungu. Aliviita visukuku “medali kubwa sana za uumbaji wa kwanza.” Isitoshe, katika utangulizi wa kitabu chake, alirejezea shauku iliyomsukuma aendelee kuchunguza: “Ni hisia ya kustaajabisha, kuridhisha na utambuzi ambao umeenea kote na unapendeza yule anayegundua au kuufikiria kwa makini sehemu ya kazi za Muumba.”

Joachim Barrande alikufa mwaka wa 1883, akiacha mali ghafi ya kisayansi yenye thamani ya juu sana. Mfikio wake wenye uangalifu sana kwa kazi yake, unathaminiwa sana na wanasayansi ulimwenguni pote. Kwa sababu ya mfikio wenye ukweli aliochukua, Joachim Barrande aliandika kwa umakini uvumbuzi ambao ungali watumika na watafiti hata leo. Kwa mtazamo wa kisayansi, haikuwa kutilia chumvi kuurejezea urithi wa Barrande kuwa “zaidi ya zawadi ya kifalme.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 “Silurian” ni mtajo wa jiolojia wa mojawapo ya vipindi vinavyodhaniwa kuwa vya kale zaidi vya sayari yetu.

[Picha katika ukurasa wa 12, 13]

Michoro ya Barrande ya athropodi wa majini, 1852

[Hisani]

Michoro: S laskavým svolením Národní knihovny v Praze

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]

Picha: Z knihy Vývoj české přírodovědy, 1931