Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Akina Baba Sababu Inayofanya Watoweke

Akina Baba Sababu Inayofanya Watoweke

Akina Baba Sababu Inayofanya Watoweke

“Sikumbuki nikiona Mama na Baba wakipigana au kubishana. Ninachojua ni kwamba Baba alikuwako—kisha akatoweka ghafula siku moja. Sijui mahali alipo baba hadi leo hii. Najua kwamba sina hisia zozote kumwelekea.”—Bruce.

“Katika shule nilikuwa mtoto pekee ambaye hakuwa na wazazi wawili na ambaye hakuishi nyumbani . . . Sikuzote nilihisi kana kwamba nilikuwa wa kipekee. Sikuzote nilihisi nikiwa tofauti kabisa na marika wangu wote.”—Patricia.

MVUVUMKO wa kiviwanda ndio chanzo cha familia zisizo na baba. Wanaume walipoanza kuvutiwa na kazi za viwanda waliondoka nyumbani mwao, daraka la baba katika familia likaanza kupungua; akina mama wakawa na fungu kubwa zaidi la kulea watoto. * Ijapokuwa hivyo, baba wengi walibaki na familia zao. Hata hivyo, katikati ya miaka ya 1960, kiwango cha talaka kilianza kuongezeka sana huko Marekani. Vizuizi vya kidini, kiuchumi, na kijamii dhidi ya talaka vikaanza kudidimia. Kwa kuchochewa na shauri la watu waliojitangaza wenyewe kuwa wataalamu ambao walisisitiza kwamba talaka haikuathiri watoto tu bali kwa kweli ingeweza kuwafaa, wenzi walianza kutalikiana kwa kiwango kisicho na kifani. Chasema kitabu Divided Families—What Happens to Children When Parents Part, cha Frank F. Furstenberg, Jr., na Andrew J. Cherlin: “Katika Ubelgiji, Ufaransa, na Uswisi viwango [vya talaka] vimeongezeka maradufu [tangu miaka ya 1960], huku katika Kanada, Uholanzi, na Uingereza vimeongezeka mara tatu.”

Ingawa kwa kawaida watoto hukaa na mama yao baada ya talaka, baba wengi wanaoondoka wanataka kudumisha uhusiano pamoja na watoto. Kushirikiana kulea watoto ni mojawapo ya utatuzi unaopendwa sana. Hata hivyo, baba wengi waliotalikiana hudumisha uhusiano mdogo sana pamoja na watoto wao. Uchunguzi mmoja ulifunua kwamba ni mtoto 1 tu kati ya watoto 6 ambaye huona baba yake aliyetalikiana kila juma. Karibu nusu ya watoto hawakuwa wamewaona baba yao kwa mwaka mzima!

Kushindwa Kulea Watoto kwa Kushirikiana

Ili wenzi waliotalikiana washirikiane kulea watoto, ushirikiano na itibari kubwa sana hutakiwa—sifa ambazo ni adimu mara nyingi. Watafiti Furstenberg na Cherlin wasema hivi: “Sababu kuu ambayo hufanya akina baba waache kuwaona watoto wao ni kwamba hawataki ushirika wowote na wake zao wa zamani. Na wanawake wengi huwa na mtazamo huo huo kuelekea waume zao wa zamani.”

Ni kweli kwamba baba wengi waliotaliki huwaona watoto wao kwa ukawaida. Lakini kwa sababu hawajihusishi tena na maisha ya kila siku ya watoto wao, inakuwa vigumu kwa baadhi yao kujiendesha kama baba wanapokuwa nao. Wengi huamua kuwa wachezaji-wenzi, wakitumia karibu muda wote pamoja katika tafrija au kununua vitu. Ari mwenye umri wa miaka 14 afafanua ziara za mwisho-juma pamoja na baba yake, akisema hivi: “Hakuna ratiba iliyowekwa, hakuna ‘kuambiwa uwe nyumbani ifikapo saa fulani. Hakuna kufuatwa-fuatwa. Hakuna vizuizi. Na baba yangu huninunulia zawadi daima.”—How It Feels When Parents Divorce, cha Jill Krementz.

Baba mwenye upendo apaswa ‘kujua jinsi ya kuwapa watoto wake zawadi zilizo nzuri.’ (Mathayo 7:11) Lakini zawadi haziwezi kuchukua mahali pa mwongozo na nidhamu inayohitajiwa. (Mithali 3:12; 13:1) Mtu anapobadili daraka lake akiwa mzazi na kuwa mchezaji-mwenzi au mgeni, uhusiano wa baba na mwana utaelekea kuzorota. Uchunguzi mmoja ulifikia mkataa huu: “Talaka yaweza kuharibu daima uhusiano wa baba na mwana.”—Journal of Marriage and the Family, Mei 1994.

Wanaume fulani huacha familia zao, wakikataa kuandaa msaada wa kifedha kwa sababu ya maumivu au hasira ya kutenganishwa na watoto wao—au labda kuonyeshwa ubaridi tu. * (1 Timotheo 5:8) “Baba hana uzuri wowote unaonipendeza ambao naweza kufikiri juu yake,” akasema mvulana mmoja tineja mwenye uchungu. “Kwa kweli hajihusishi na chochote, hatutegemezi wala kufanya chochote, nafikiri jambo hilo linachukiza sana.”

Wazazi Ambao Hawajafunga Ndoa

Idadi isiyo na kifani ya watoto haramu imesababisha ongezeko kubwa la watoto wasio na baba. “Karibu thuluthi ya watoto wanaozaliwa [Marekani] sasa huzaliwa nje ya ndoa,” chasema kitabu Fatherless America. Miongoni mwa watoto wapatao 500,000 wanaozaliwa kila mwaka na wazazi wenye umri unaoanzia miaka 15 hadi 19, asilimia 78 ni wa matineja ambao hawajafunga ndoa. Hata hivyo, mimba za matineja ni tatizo la tufeni pote. Na programu zinazofundisha watu kuzuia mimba, au kuwahimiza waepuke ngono hazijafua dafu katika kubadili mwenendo wa kingono wa matineja.

Kitabu Teenage Fathers, cha Bryan E. Robinson, chaeleza hivi: “Mimba zinazopatikana nje ya ndoa haziaibishi tena kama ilivyokuwa katika miaka ya 1960 kwa sababu ya mitazamo ya kijamii inayoruhusu zaidi ngono na mimba kabla ya ndoa. . . . Pia vijana wa leo hukabiliwa daima na utendaji wa kingono kupitia matangazo ya biashara, muziki, sinema, na televisheni. Vyombo vya habari vya Marekani huwaambia wabalehe kwamba ngono inapendeza na inasisimua hisia bila kuwaonyesha kamwe matokeo halisi ya mwenendo wa kingono wa kihobelahobela usiodhibitiwa.”

Vijana wengi wanafurahia ngono haramu bila kujua matokeo yake. Ona baadhi ya maelezo ambayo mwandishi Robinson alipokea: “‘Hakuonekana kama wale wanaoweza [kupata mimba]’; ‘Tulifanya ngono mara moja tu kwa juma’; au ‘Sikudhani ungeweza kupata mimba mara ya kwanza.’” Bila shaka, vijana fulani wanafahamu vizuri kabisa kwamba ngono yaweza kutokeza mimba. Kitabu Young Unwed Fathers chasema: “Kwa wavulana wengi [katika sehemu ya jiji yenye watu wengi], ngono ni ishara muhimu ya hadhi ya kijamii; kuvutiwa na ngono huonwa kuwa mafanikio. Wasichana wengi hujitolea kufanya ngono ikiwa zawadi ili wapate kupendwa na mwanamume kijana.” Katika sehemu fulani za jiji zenye watu wengi, wavulana ambao hawajazaa mtoto huenda hata wakadhihakiwa kuwa “bikira”!

Hali inakuwa mbaya hata zaidi unapofikiria matokeo ya uchunguzi wa 1993 uliofanyiwa akina mama wenye umri wa kwenda shuleni huko California. Inatukia kwamba thuluthi mbili ya wasichana walipata mimba, si kutoka kwa rafiki zao wa kiume matineja, bali kutoka kwa wanaume wenye umri unaozidi miaka 20! Kwa kweli, uchunguzi fulani ulionyesha kwamba mama wengi wasiofunga ndoa ambao ni matineja hubakwa kwa nguvu—au hata hutendwa vibaya wanapokuwa watoto. Hali hiyo iliyoenea pote hufunua jinsi ambavyo jamii ya siku hizi imefisidika kiadili na kupotoka.—2 Timotheo 3:13.

Sababu Inayofanya Vijana Waondoke

Ni nadra sana kwa vijana matineja ambao huzaa watoto kuchukua daraka la muda mrefu kuelekea watoto wao. Asema mvulana mmoja ambaye rafiki yake wa kike alipata mimba: “Nilimwambia tu ‘kwaheri,’ ‘uhusiano umekwisha.’” Hata hivyo, kama isemavyo makala moja katika kichapo Family Life Educator, “baba wengi wachanga hudhihirisha tamaa kubwa ya kuwa na uhusiano wa karibu pamoja na watoto wao.” Kulingana na uchunguzi mmoja wa akina baba ambao hawajafunga ndoa, asilimia 70 walitembelea mtoto wao mara moja kwa juma. “Hata hivyo,” yaonya makala hayo, “kadiri watoto wanavyokua, ziara hupungua.”

Baba mmoja mwenye umri wa miaka 17 alisema kwa ufupi kwa nini hali huwa hivyo, akisema: “Ikiwa ningejua namna hali ingekuwa ngumu, singekubali jambo hili litukie kamwe.” Ni vijana wachache waliokomaa na walio na uzoefu wa kushughulika na madai ya kuwa mzazi. Wala wengi hawana elimu wala stadi za kazi zinazohitajiwa ili kujiruzuku. Badala ya kukabiliana na aibu ya kutofaulu, wanaume wengi wachanga huwaacha watoto wao. “Maisha yangu yamejaa matatizo na taabu,” akiri baba mmoja mchanga. Mwingine aomboleza hivi: “Siwezi kujitunza kamwe; sijui ningefanya nini ikiwa ningehitaji kumtunza [mwanangu] pia.”

Zabibu Mbichi

Katika nyakati za Biblia Wayahudi walikuwa na msemo: “Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa ganzi la meno.” (Ezekieli 18:2) Mungu aliwaambia Wayahudi kwamba haikupasa kuwa hivyo, kwamba makosa ya wakati uliopita hayahitaji kurudiwa wakati ujao. (Ezekieli 18:3) Hata hivyo, mamilioni ya watoto leo wanaonja uchungu wa “zabibu mbichi” za wazazi wao—wakilipia kutokomaa kwa wazazi wao, kutochukua madaraka, na kutofaulu kwa ndoa. Utafiti unadhihirisha kwa dhati kwamba watoto wanaokua bila baba hukabili hatari nyingi sana za kimwili na kihisia-moyo. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 7.) Jambo lenye kutaabisha hasa ni uhakika wa kwamba urithi wa kutokuwa na baba nyumbani mara nyingi hupitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine—zoea lenye maumivu na taabu.

Je, familia zisizo na baba haziwezi kufaulu? Sivyo hata kidogo. Kwa hakika, habari njema ni kwamba zoea la familia zisizo na baba laweza kukomeshwa. Makala yetu ifuatayo itazungumzia jinsi inavyowezekana.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Kwa kupendeza, kabla ya mvuvumko wa kiviwanda, vitabu vya maagizo ya kulea watoto huko Marekani kwa kawaida vilielekezwa kwa akina baba, wala si kwa akina mama.

^ fu. 10 Kulingana na watafiti Sara McLanahan na Gary Sandefur, huko Marekani, “karibu asilimia 40 ya watoto ambao kulingana na kanuni wanapaswa kutegemezwa wakiwa watoto hawana [kibali cha mahakama] hata kidogo cha utegemezo wa mtoto, na robo ya wale walio na kibali hicho hawapati chochote. Watoto wanaopungua thuluthi moja ndio hupokea kiasi kamili wanachowiwa.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

HATARI ZA KUKUA BILA BABA

Kukua bila baba hutokeza hatari kubwa kwa watoto. Ingawa habari ifuatayo yaweza kuhuzunisha watu fulani wanapoifikiria, kufahamu hatari hizo ndiyo hatua ya kwanza ya kuzuia au angalau kupunguza madhara hayo. Pia, ng’amua kwamba takwimu zahusu vikundi wala si watu mmoja-mmoja. Watoto wengi hukua katika nyumba zisizo na baba bila kupatwa na mojawapo ya matatizo hayo. Kama makala yetu ya mwisho yatakavyoonyesha, mzazi anapoingilia kati na kutumia kanuni za Biblia anaweza kufanya mengi ili kupunguza magumu hayo yawezayo kutokea. Basi, fikiria baadhi ya hatari ambazo huenda mtoto asiye na baba akakabili.

Hatari Kubwa Zaidi za Kutendwa Vibaya Kingono

Utafiti unaonyesha wazi kwamba kutokuwa na baba huongeza hatari za kutenda mtoto vibaya kingono. Uchunguzi mmoja ulifunua kwamba miongoni mwa visa 52,000 vya kutenda watoto vibaya, “asilimia 72 ilihusisha watoto wanaoishi katika nyumba isiyo na mzazi mmoja wa asili au wote wawili.” Kitabu Fatherless America chasisitiza: “Kuongezeka kwa hatari ya kutendwa vibaya utotoni katika jamii yetu hutokana hasa na ongezeko la baba ambao hawajafunga ndoa na ongezeko la baba wa kambo, marafiki wa kiume, na wanaume wengine wasio wa ukoo.”

Kuongezeka kwa Hatari ya Mapema ya Mwenendo wa Kingono

Kwa kuwa hakuna usimamizi wa kutosha kutoka kwa mzazi katika nyumba zenye mzazi mmoja, mara nyingi vijana wanakuwa na fursa za kujihusisha katika mwenendo usio wa adili. Mazoezi yasiyotosha ya mzazi yaweza kuchangia pia. “Wasichana ambao hawana baba maishani wanakabili uwezekano mara mbili na nusu wa kupata mimba,” yasema Wizara ya Afya na Huduma za Jamii ya Marekani.

Umaskini

Uchunguzi uliofanyiwa wasichana weusi matineja huko Afrika Kusini ulifikia mkataa kwamba umaskini ni tokeo la kawaida linalowapata wazazi wasiofunga ndoa. “Katika asilimia 50 ya visa,” wasema waandishi wa uchunguzi huo, “tineja haelekei kurudi shuleni,” na mama wengi ambao hawajafunga ndoa huishia katika maisha ya ukahaba na ulanguzi wa dawa za kulevya. Hali iko namna moja katika nchi za Magharibi. Huko Marekani, “asilimia 10 ya watoto katika familia zenye wazazi wawili walikuwa maskini [mwaka wa 1995], kwa kulinganishwa na asilimia 50 katika familia zenye mama peke yake.”—America’s Children: Key National Indicators of Well-Being 1997.

Kupuuzwa

Wanapolazimika kujitafutia riziki wenyewe, mara nyingi wazazi wasio na wenzi hulemewa na madaraka yao na hushindwa kutumia wakati wa kutosha pamoja na watoto wao. Mwanamke mmoja aliyetalikiwa akumbuka hivi: “Nilikuwa nikifanya kazi mchana na kwenda shuleni usiku—nikapatwa na mkazo mkubwa. Kwa wazi niliwapuuza watoto.”

Madhara ya Kihisia-Moyo

Kinyume cha madai ya wataalamu fulani kwamba watoto hurudia hali ya kawaida baada ya talaka, watafiti kama vile, Dakt. Judith Wallerstein, wameona kwamba talaka hutokeza vidonda vya kihisia-moyo vinavyodumu muda mrefu. “Zaidi ya thuluthi ya wanaume na wanawake wachanga wenye umri wa kati ya miaka 19 na 29 wanakuwa na miradi michache au hawawi na miradi yoyote miaka kumi baada ya talaka ya wazazi wao. Wanaishi bila kuweka miradi yoyote maishani . . . na hisi ya kutojiweza.” (Second Chances, cha Dakt. Judith Wallerstein na Sandra Blakeslee) Kutojistahi, kushuka moyo, tabia ya uhalifu, na hasira za daima ni mambo yaliyoonekana miongoni mwa watoto wengi ambao wazazi wao wametalikiana.

Kitabu The Single-Parent Family chasema: “Uchunguzi mwingi waonyesha kwamba wavulana ambao wamelelewa bila baba katika maisha yao hukosa usalama kuhusu jinsia yao, kutojistahi, na baadaye maishani mwao, wanaona ugumu wa kuwa na mahusiano ya kindani. Matatizo ambayo huenda wasichana wakawa nayo kwa kuishi bila baba kwa kawaida hayaonekani hadi wanapobalehe au baadaye, na yanatia ndani ugumu wa kuanzisha uhusiano mzuri na wanaume na wanawake wakati wa utu uzima.”