Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jaribu Kutumia Jozi ya “Vitu Vyepesi”!

Jaribu Kutumia Jozi ya “Vitu Vyepesi”!

Jaribu Kutumia Jozi ya “Vitu Vyepesi”!

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA TAIWAN

USO wenye kung’aa kwa shangwe wa msichana huyo mdogo unaonyesha waziwazi kwamba anafurahia mlo. Mkono wake wa kushoto una bakuli lililojaa wali pomoni, vipande vidogo vya mboga, na samaki. Mkono wake wa kulia umeshika vijiti viwili vyembamba vya mwanzi. Msichana huyo achota mafunda ya mlo anaopenda na kuyatia kinywani barabara kwa vijiti hivyo anavyoshika kwa vidole vyake vidogo. Nyakati nyingine anasogeza bakuli karibu na kinywa, kisha anachota wali na kuutia kinywani upesi-upesi kwa vijiti hivyo. Laonekana kuwa jambo la kawaida, rahisi, na safi.

Bila shaka, msichana huyo anashika mkononi mwake vijiti mashuhuri vya kulia. Katika Kichina vinaitwa k’uai tzu (Kipinyin, kuaizi), jina limaanishalo “vitu vyepesi.” Neno la Kiingereza “chopstick” lasemwa kuwa latokana na neno chop, la lugha ya mchanganyo limaanishalo “-epesi.” Kwa vyovyote vile, vinapatikana katika karibu kila nyumba katika Kusini-Mashariki ya Asia. Huenda ulijaribu kuvitumia ulipokuwa ukila katika mkahawa wa Kichina. Lakini je, wajua wazo la kutumia vijiti vya kulia lilitoka wapi? Au ni jinsi gani na ni lini vilipotumiwa kwanza? Na je, ungependa kujua jinsi unavyoweza kuvitumia vema?

“Vitu Vyepesi”

Vijiti vya kulia ni vyembamba na vina urefu wa sentimeta 20 hadi 25 hivi. Kwa kawaida nusu ya sehemu ya juu ya kijiti hicho huwa na umbo la mraba. Umbo hilo hufanya iwe rahisi kuvishika na huvizuia kubingirika mezani. Kwa kawaida nusu ya sehemu ya chini huwa na umbo la mviringo. Mara nyingi, vijiti vya kulia vya Wajapani ni vifupi na huwa na ncha kali kuliko vya Wachina.

Kwa sababu ya uzalishaji kwa wingi siku hizi, mikahawa mingi huwa na vifurushi vya vijiti vya kulia ambavyo vingali vimeshikana kwenye sehemu ya juu. Ni sharti mlaji avitenganishe kabla ya kuvitumia. Vijiti hivyo hufanyizwa kwa mbao ya kawaida au mwanzi kwa sababu vinatumiwa mara moja tu. Kwa kawaida vijiti vinavyotumiwa kwenye mikahawa ghali zaidi au nyumbani huwa maridadi sana, hufanyizwa kwa mwanzi uliong’arishwa, mbao iliyopakwa vanishi, plastiki, chuma cha pua, au labda fedha au pembe ya tembo. Huenda vikawa na maandishi ya ushairi au vikarembeshwa kwa picha.

Jinsi ya Kutumia Vijiti vya Kulia

Watu wengi wanaozuru nchi za Mashariki kama vile China na Japani huvutiwa sana wanapoona mtoto mdogo labda mwenye umri wa miaka miwili tu akila kwa vijiti vionekanavyo kuwa vikubwa sana. Punde si punde, mlo wote huchotwa fundo baada ya jingine hadi kinywani mwake. Kwa kweli huonekana rahisi sana.

Je, ungependa kujaribu kutumia jozi ya “vitu vyepesi”? Mwanzoni huenda ukaona ugumu wa kuvitumia kwa wepesi, lakini inakuwa rahisi unapojizoeza kidogo tu na vijiti hivyo vinakuwa kama sehemu ya mkono wako.

Vijiti vya kulia hushikwa kwa mkono mmoja tu, hasa mkono wa kulia. (Ona picha kwenye ukurasa wa 15.) Kwanza, kunja mkono wako mfano wa kikombe, kidole-gumba kikiwa mbali na vidole vinginevyo. Weka kijiti kimoja kati ya kidole-gumba chako na vidole vingine, kikiwa kimelalia sehemu ya chini ya kidole chako cha shahada na ncha ya kidole chako cha pete. Halafu weka kijiti cha pili sambamba na cha kwanza, na ukishike kwa kidole-gumba chako, kidole cha shahada na cha kati, kama penseli. Lainisha ncha zake kwa kuzigongesha taratibu mezani. Kisha, sogeza kijiti cha juu kwa kujongeza kidole chako cha shahada na cha kati juu na chini pasipo kusogeza kijiti kilicho chini. Jizoeze hadi unapoweza kukutanisha ncha za vijiti vyote viwili kwa urahisi. Sasa uko tayari kutumia vifaa hivi vyenye matumizi mbalimbali ili kula kipande chochote chenye ladha kwenye mlo wa Wachina—kutoka chembe moja ya wali hadi yai la kipululu! Vijiti vya kulia na mlo wa Wachina huambatana vyema kwa sababu kwa kawaida mlo hukatwa katika vipande vyenye ukubwa unaofaa.

Namna gani mlo ambao kuku, bata, au tako la nguruwe huandaliwa likiwa zima, bila kukatakatwa vipande vidogo? Kwa kawaida mlo huo hupikwa kwa kiasi cha kwamba vijiti vya kulia huweza kukata visehemu vidogo kwa urahisi. Vijiti vya kulia hufaa kwa samaki, ambao kwa kawaida huandaliwa wazima; waweza kuepuka mifupa kwa urahisi kuliko unapotumia kisu na umma.

Vipi juu ya kula wali? Iwapo si mlo maalum, waweza kushika bakuli la wali kwa mkono wa kushoto, ulisogeze kinywani, kisha uchote wali kwa vijiti vya kulia na kutia mdomoni mwako. Hata hivyo, wakati wa mlo maalum utahitaji kuchota wali kwa vijiti hivyo kiasi kidogo-kidogo.

Namna gani mchuzi, ambao ni sehemu muhimu ya mlo wa Wachina? Kwa kawaida mtu hupewa kijiko cha kauri. Lakini endapo mchuzi una tambi za kuliwa au maandazi ya kinyunya au vipande vya mboga, nyama, au samaki, jaribu kutumia vijiti kwa mkono wa kulia ili kuchotea chakula na kijiko kwa mkono wa kushoto ili kukusaidia ukifikishe kinywani.

Adabu na Vijiti vya Kulia

Unapoalikwa kwenye mlo katika nyumba ya Wachina, yafaa ujue adabu za mezani za Wachina. Kwanza, chakula tofauti huwekwa katikati mezani. Subiri hadi mwenyeji au kichwa cha familia anapochukua vijiti vyake na kuwaashiria wote waanze. Huo ndio wakati barabara wa wageni kukubali mwaliko huo, kuchukua vijiti vyao vya kulia na kuanza kula.

Tofauti na milo fulani ya Magharibi, chakula hakipitishwi kuzunguka meza. Badala yake, wote waliopo mezani hujipakulia watakavyo. Katika mlo wa familia, ni kawaida kwa kila mshiriki wa familia kuchota vipande kutoka kwenye mlo huo kwa vijiti vyake na kuvitia kinywani mwake. Hata hivyo, kufyonza chakula kwa kelele, kuramba ncha za vijiti vyako vya kulia, au kutafuta-tafuta kipande unachopenda sana kwenye chakula huonwa kuwa utovu wa adabu. Akina mama wa nchi za Mashariki huwafunza watoto wao kutotafuna ncha za vijiti vyao, si kwa sababu ya afya tu bali pia kwa sababu kufanya hivyo huharibu umbo la vijiti hivyo.

Nyakati nyingine vijiko vya kupakulia au vijiti zaidi vya kulia huandaliwa kwa ajili ya wageni. Hivyo hutumiwa kupakulia chakula kutoka kwenye vyombo vilivyo katikati na kukitia katika sahani nyingine au bakuli lako la wali. Hata hivyo, usiudhike mwenyeji anapokupakulia kipande bora kwa vijiti vyake na kukitia katika bakuli lako. Kwa vyovyote vile, anataka kuhakikisha kwamba mgeni wake mheshimiwa anapata kipande bora!

Kumwelekezea mtu vijiti vya kulia huonwa kuwa utovu wa adabu, kama ilivyo na visu na nyuma. Ni utovu wa adabu pia kuchukua kitu kingine huku ukiwa na vijiti vya kulia mkononi. Kwa hiyo, unapohitaji kutumia kijiko cha kupakulia au kipangusia-mdomo au kikombe cha chai, kwanza weka vijiti vyako mezani. Vinara vidogo vyenye kuvutia vya kuwekea vijiti vya kulia huandaliwa kwa kusudi hilo.

Umalizapo kula, weka vijiti vyako mezani taratibu, subiri kwa utulivu. Ni utovu wa adabu kuondoka mezani kabla wengine hawajamaliza mlo. Mara nyingine tena, ni mwenyeji au kichwa cha familia anayefunga mlo kwa kuinuka na kuwaalika wote waondoke mezani.

Sasa kwa kuwa umejua namna ya kutumia vijiti vya kulia, unachohitaji kufanya tu ni kupata vijiti hivyo na kujizoeza kuvitumia. Wakati ujao mtu fulani anapokualika katika mkahawa wa Kichina au nyumbani mwao kwa ajili ya mlo wa Kichina, mbona usijaribu kutumia jozi ya “vitu vyepesi”? Huenda hata vikaongeza ladha ya mlo!

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14]

Historia Fupi ya Vijiti vya Kulia

Wasomi fulani Wachina wanaamini kuwa vijiti vya kwanza vilitumiwa si kwa kulia, bali kwa kupikia. Vipande vidogo vya chakula kibichi vilifunikwa kwa majani, na vijiti vilitumiwa kutika vijiwe vyenye moto ndani ya vifuniko hivyo. Kwa njia hiyo chakula kingeweza kupikwa bila mpishi kuungua! Baadaye katika historia, vijiti vya kulia vilitumiwa kupakulia vipande vya chakula kutoka kwenye chungu cha kupikia.

Yaelekea kwamba vijiti vya kale vilifanyizwa kwa mbao zisizodumu au mwanzi. * Hiyo ni sababu moja inayofanya iwe vigumu zaidi kubaini wakati hususa vilipotumiwa kwanza. Watu wengine huamini kwamba vijiti vya kulia vilitumiwa China mapema wakati wa utawala wa ukoo wa Shang (yapata karne ya 16 hadi ya 11 K.W.K.). Hati moja ya kihistoria ya baada tu ya kuwapo kwa Confucius (551−497 K.W.K.) ilieleza juu ya ‘kuokota’ chakula kutoka kwenye mchuzi, ikionyesha kwamba vijiti vya kulia vya aina fulani vilitumiwa.

Kwa wazi mapema wakati wa utawala wa ukoo wa Han (206 K.W.K. hadi 220 W.K.), kula kwa vijiti kulikuwa jambo la kawaida. Kaburi la kipindi hicho lililofukuliwa huko Changsha, Jimbo la Hunan, lilikuwa na seti ya vyombo vya kulia vyenye vanishi, kutia ndani vijiti vya kulia.

Wajapani, Wakorea, Wavietnamu, na wengine huko Mashariki hutumia pia vijiti vya kulia hasa kwa sababu ya uvutano wa utamaduni wa China.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 25 Herufi za Kichina za kuai katika neno kuaizi na herufi za kale za neno zhu huhusiana na mwanzi, zikidokeza kifaa kilichotumiwa kufanyizia vijiti vya kulia hapo awali.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Inakuwa rahisi unapojizoeza