Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Quetzal Ndege Anayeng’aa

Quetzal Ndege Anayeng’aa

Quetzal Ndege Anayeng’aa

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KOSTA RIKA

INGAWA Kosta Rika ina eneo linalopungua asilimia 0.03 ya eneo la dunia, ina jamii 875 za ndege wajulikanao. Kwa mujibu wa kichapo kimoja, idadi hiyo inapita jumla ya jamii za ndege wapatikanao Kanada na Marekani. Hivyo, haishangazi kwamba watu wanaopenda kuangalia ndege huzuru sana Kosta Rika. Jiunge nasi kwenye safari ya kuangalia mojawapo ya ndege hawa, quetzal anayeng’aa.

Mshindi Mhispania Hernán Cortés, aliwasili Mexico mapema miaka ya 1500. Alipowasili, Waazteki walimpa zawadi ya kilemba cha manyoya ya quetzal. Ni familia za kifalme tu za Waazteki zilizokuwa na pendeleo la kuvalia mapambo hayo yenye kustahiwa sana. Huenda manyoya ya kijani-kibichi ya quetzal yalionwa kuwa na thamani kuliko dhahabu.

Leo ndege huyu maridadi isivyo kawaida huishi katika eneo pana kutoka Mexico hadi Panama. Ndege quetzal aweza kupatikana katika misitu yenye ukungu kwenye mwinuko wa kati ya meta 1,200 hadi 3,000. Ukungu ulio kwenye misitu hiyo hutokana na kupoa haraka kwa hewa yenye joto inayoelekea juu. Hilo hutokeza mimea inayositawi yenye majani mabichi mwaka mzima na miti mikubwa inayofikia urefu wa meta 30 au zaidi ukunguni.

Hifadhi ya Msitu ya Santa Elena iliyo umbali wa kilometa 200 hivi kaskazini ya San José—ni mahali panapofaa pa kuwatazama quetzal wakiwa katika mazingira ya asili. Twaanza safari ya kumtafuta quetzal anayeng’aa kwa msaada wa kiongozi. Ndege huyo haonekani kwa urahisi kwa sababu ya rangi yake ya kijani-kibichi inayofanana na majani ya msitu. Kiongozi wetu aanza kuiga mlio wake mwororo na laini. Mlio huo washabihi kilio cha kitoto cha mbwa. Kwa kweli, mwanamke mmoja katika kikundi chetu anaposikia itikio la quetzal, yeye afikiri kwamba kuna mbwa aliyepotea msituni!

Punde si punde, tukiwa tumepanda meta 15 hivi, twamwona quetzal wa kiume akitua kwa woga kwenye tawi ili achunguze hali. Rangi zake zenye kung’aa zastaajabisha hata zaidi ya tulivyofikiri tunapomtazama kwa darubini. Kidari chake ni cha rangi nyekundu iliyoiva, tofauti na manyoya yake ya kijani-kibichi. Manyoya yake meupe ya mkiani yanayotofautiana na yale mawili ya kijani-kibichi yanayometameta na kuzidisha uzuri wake wenye kustaajabisha. Huwa membamba na marefu kama bendera yakiwa na urefu wa meta 0.6. Kutazama manyoya marefu ya mkia wa quetzal aliye kwenye tawi yakipeperushwa taratibu na upepo mwanana huvutia ajabu.

Ni jambo la pekee sana kumwona quetzal. Kwa kweli, kiongozi wetu alisema kwamba unaweza kumwona tu baada ya kumtafuta msituni mara kadhaa. Wakati bora wa kuwaona quetzal ni msimu wa kutaga mayai, unaoanza Machi hadi Juni. Wakati huo huenda wakawa na makundi mawili yenye mayai mawili-mawili.

Turudipo kwenye ofisi ya hifadhi, twamsikia quetzal mwingine. Anyiririka kwa madaha huku akiwa na manyoya marefu ya kijani-kibichi mkiani, kisha atua kwenye tawi lililo umbali wa meta tano hivi kutoka mahali tunapoketi! Kiongozi atuambia kuwa kinda limepotea kutoka kwenye kiota chake. Baba atafuta kinda lake kutoka mti mmoja hadi mwingine. Twajulishwa kwamba ni takriban asilimia 25 tu ya mayai yanayofikia ukomavu. Mengineyo huliwa na wanyama kama kuchakuro, toucanet wa kijani-kibichi, jay wa kahawia, weasel, na tayra. Jambo jingine linalohatarisha kuokoka kwa quetzal ni mahali pa viota vyao, mashimo yafananayo na yale ya kigogota yanayotengenezwa na quetzal katika mashina ya miti yaliyozeeka ambayo yanaoza, yenye urefu wa kati ya meta 3 hadi 20 kutoka ardhini. Mvua kubwa inaponyesha, mashimo hayo hufurika maji au huporomoka.

Tunajifunza pia kwamba quetzal hupenda sana kula maparachichi ya porini. Hutulia kwenye tawi huku akitazama parachichi linaloning’inia kwenye mparachichi ulio karibu. Kisha, kwa mvumo wa mabawa yanayopigapiga, hurukia tunda lile, hulichopoa kwa kinywa na kurejea kiotani. Hubugia parachichi lote kisha hutapika mbegu yake kubwa baada ya dakika 20 hadi 30 hivi.

Quetzal huhama kutoka bara moja hadi jingine akitafuta maparachichi ya porini. Kwa mfano, kuanzia Julai hadi Septemba, wao huishi karibu na Bahari ya Pasifiki. Kisha mnamo Oktoba wao huhamia sehemu ya Karibea ili kula maparachichi mengine.

Tunapovuka daraja linaloning’inia lenye urefu wa meta 30 hivi kwenye msitu, karibu tugongane na quetzal anayepuruka karibu! Yaonekana kwamba ndege huyo alikuwa akifukuza windo lake tulipopitana naye. Yule wa kike ametua tu juu yetu, akitutazama kwa ukali kwa sababu ya kuingilia faragha yao.

Twaelezwa pia kwamba wao hupenda kula tunda la blackberry, linalokua kwenye michongoma. Quetzal wanaposhuka kwa kasi ili kuchopoa tunda hilo, nyakati nyingine manyoya ya mkiani hunaswa na kubaki kati ya michongoma. Hata hivyo, hatimaye manyoya hayo ya mkiani hukua tena.

Kwa njia hii ndege huyo huishi kupatana na jina lake. “Quetzal” hutokana na neno la Kiazteki “quetzalli,” linalomaanisha “mwenye thamani” au “maridadi.” Kwa kusikitisha, umaridadi huo umehatarisha kuwapo kwa quetzal. Kwa hakika, quetzal huhesabiwa miongoni mwa viumbe walio hatarini. Wamewindwa kwa ajili ya ngozi yao, ambayo huuzwa ikiwa hedaya. Baadhi ya ndege hao wamenaswa wakiwa hai ili wauzwe wakiwa vipenzi. Hata hivyo, kiongozi wetu atuambia kuwa sasa quetzal analindwa kisheria kutokana na hatari hiyo.

Lakini hatari nyingine inayotisha kuokoka kwao ni uharibifu wa misitu, unaoharibu makao yao. Takriban asilimia 27 ya eneo la Kosta Rika limetengwa likiwa hifadhi ya kulinda ndege huyu anayeng’aa na wanyama-mwitu wengine.

Safari yetu ya kwenda kumwangalia quetzal kwa kweli imekuwa yenye kuthawabisha. Kwa kweli, waweza kuona kilemba cha manyoya ya quetzal alichopewa Hernán Cortés katika Jumba la Makumbusho la Uingereza huko London. Lakini manyoya ya quetzal huvutia zaidi yaonekanapo kwenye ndege aliye hai porini! Angalau kwa sasa, quetzal wa mwituni wanaendelea kufurahia uhuru na usalama wa kadiri katika misitu yenye ukungu ya Amerika ya Kati.