Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kujiua Tatizo Lililojificha Linaloenea Kasi

Kujiua Tatizo Lililojificha Linaloenea Kasi

Kujiua Tatizo Lililojificha Linaloenea Kasi

JOHN NA MARY * wana umri unaozidi miaka 50 na wanaishi katika nyumba ndogo kwenye eneo la mashambani huko Marekani. John ana ugonjwa unaofisha wa kuvimba mapafu na moyo unaovilia damu na kusita. Mary hawezi kuwazia kuishi bila John, naye hawezi kustahimili uchungu wa kumwona akidhoofika zaidi na zaidi, na kuwa hoi. Mary ana matatizo yake ya afya naye ameugua mshuko-moyo kwa miaka mingi. John amekuwa akihangaika sana karibuni kwa sababu Mary amekuwa akisema juu ya kujiua. Fikira zake zimekanganyika kwa sababu ya mshuko-moyo na dawa anazotumia. Anasema kwamba hawezi kustahimili wazo la kubaki peke yake.

Dawa zimetapakaa kila mahali nyumbani—vidonge vya moyo, dawa zinazopunguza mshuko-moyo, dawa za kutuliza maumivu. Mapema asubuhi moja, Mary aingia jikoni na kuanza kubugia vidonge. Aendelea kumeza tu hadi John anapomkuta na kumpokonya vidonge hivyo. Yeye aita kikosi cha waokoaji huku Mary akiwa amezimia. Yeye asali kwamba isiwe kuchelewa mno.

Yanayofunuliwa na Takwimu

Mengi yameandikwa katika miaka ya karibuni kuhusu kuongezeka kwa visa vya kujiua miongoni mwa vijana—yafaa, kwa kuwa ni msiba gani mkubwa unaoweza kupita kifo cha mapema cha kijana, mchanga mwenye mataraja mema? Lakini, vyombo vya habari havitaji jambo hakika la kwamba visa vya kujiua katika nchi nyingi huongezeka kulingana na umri. Hilo ni kweli iwe jumla ya visa vya kujiua katika nchi fulani iko juu au chini, kama sanduku lililo katika ukurasa uliotangulia lionyeshavyo. Kuchunguza takwimu hizo hufunua pia hali ya tatizo hilo lililojificha linaloenea tufeni pote.

Mnamo mwaka wa 1996 Vituo vya Kudhibiti Magonjwa vya Marekani viliripoti kwamba idadi ya visa vya kujiua miongoni mwa Wamarekani wenye umri wa miaka 65 na zaidi iliongezeka ghafula kwa asilimia 36 tangu mwaka wa 1980. Idadi kubwa ya Wamarekani wazee-wazee walichangia ongezeko hilo—japo si hao tu. Idadi halisi ya watu wenye umri unaozidi miaka 65 waliojiua mwaka wa 1996 iliongezeka pia, kwa asilimia 9, mara ya kwanza kwa muda wa miaka 40. Kuhusu vifo vilivyotokana na majeraha, Wamarekani wengi wazee-wazee walikufa kutokana na kuanguka na aksidenti za magari peke yake. Kwa kweli, huenda hata takwimu hizi zenye kushtua zikawa chini sana. “Yashukiwa kwamba takwimu hizo zinazotegemea hati zinazoeleza kisababishi cha kifo zinataja visa vichache sana vya kujiua,” chasema kitabu A Handbook for the Study of Suicide. Kitabu hicho chaongezea kwamba watu fulani wanakadiria takwimu halisi kuwa maradufu zaidi ya takwimu zilizoripotiwa.

Matokeo ni nini? Marekani sawa na nchi nyinginezo nyingi, inakumbwa na tatizo lililojificha linaloenea kasi tufeni pote la kujiua kwa raia wazee-wazee. Dakt. Herbert Hendin, mtaalamu wa tatizo la kujiua, asema: “Licha ya kwamba visa vya kujiua katika Marekani huongezeka kwa kawaida kulingana na umri, kujiua miongoni mwa watu wazee-wazee hakuzingatiwi sana na umma.” Mbona iwe hivyo? Yeye adokeza kwamba sehemu ya tatizo hilo ni kwa sababu visa vya watu wazee-wazee kujiua vimekuwa vingi sikuzote, “havijazusha hofu ya ghafula kama ongezeko kubwa la vijana kujiua.”

Kujiua Haraka Zaidi

Japo takwimu hizo zinatisha, ni tarakimu tu zisizo na utu. Haziwezi kueleza maisha ya upweke pasipo mwenzi mpenzi, kujitegemea kunakokatisha tamaa, kuvunjika moyo kwa sababu ya maradhi sugu, hisia ya upweke na huzuni iletwayo na mshuko-moyo mkali sana, habari zenye kukatisha tamaa za kuwa na ugonjwa wa kufisha. Ukweli wenye kuhuzunisha ni kwamba ingawa vijana huenda wakajaribu kujiua kwa sababu ya kutenda bila kufikiri kwa sababu ya matatizo ya muda, kwa kawaida wazee-wazee hukabili matatizo yaonekanayo kuwa ya kudumu na yasiyoweza kutatuliwa. Tokeo ni kwamba, mara nyingi wao huazimia kujiua kuliko vijana nao hujiua haraka zaidi.

“Si kwamba tu kujiua kumeenea sana miongoni mwa wazee-wazee, bali tendo la kujiua ladhihirisha tofauti muhimu kati ya vijana na wazee,” asema Dakt. Hendin, katika kitabu chake Suicide in America. “Hasa uwiano wa majaribio halisi ya kujiua hubadilika sana miongoni mwa wazee-wazee. Miongoni mwa watu wote kwa ujumla, uwiano wa majaribio ya kujiua na kujiua halisi umekadiriwa kuwa 10 kwa 1; miongoni mwa vijana (wenye umri wa miaka 15 hadi 24), umekadiriwa kuwa 100 kwa 1; na miongoni mwa wale wenye umri unaozidi miaka 55, umekadiriwa kuwa 1 kwa 1.”

Hizo ni takwimu zinazohitaji kufikiriwa kama nini! Jinsi lilivyo jambo lenye kuvunja moyo kuzeeka, kudhoofika kimwili, na kuteseka kwa maumivu na ugonjwa! Si ajabu kwamba wengi hujiua. Hata hivyo, kuna sababu nzuri ya kuthamini sana uhai—hata chini ya hali ngumu sana. Fikiria kilichompata Mary aliyetajwa mwanzoni.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Majina yamebadilishwa.

[Chati katika ukurasa wa 3]

Visa vya Kujiua Kati ya Kila Watu 100,000, Kulingana na Umri na Jinsia

Wanaume/Wanawake Miaka 15 Hadi 24

8.0/2.5 Argentina

4.0/0.8 Ugiriki

19.2/3.8 Hungaria

10.1/4.4 Japani

7.6/2.0 Mexico

53.7/9.8 Urusi

23.4/3.7 Marekani

Wanaume/Wanawake Miaka 75 na Zaidi

55.4/8.3 Argentina

17.4/1.6 Ugiriki

168.9/60.0 Hungaria

51.8/37.0 Japani

18.8/1.0 Mexico

93.9/34.8 Urusi

50.7/5.6 Marekani