Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Papa-mweupe Mkubwa Ashambuliwa

Papa-mweupe Mkubwa Ashambuliwa

Papa-mweupe Mkubwa Ashambuliwa

Samaki mla-nyama aliye mkubwa zaidi ulimwenguni, papa-mweupe mkubwa huenda anahofiwa zaidi na wanadamu kuliko na viumbe wengineo. Hata hivyo, sasa samaki huyo analindwa katika maeneo ya bahari huko Afrika Kusini, Australia, Brazili, Marekani, Namibia na katika Bahari ya Mediterania pia. Nchi na serikali nyingine zinafikiria pia kumlinda papa huyo. Lakini kwa nini wamlinde samaki ajulikanaye kuwa muuaji? Kama tutakavyoona, hilo ni suala gumu. Wala maoni ya umma juu ya papa-mweupe sikuzote hayategemei mambo hakika.

PAPA-MWEUPE mkubwa * pamoja na nyangumi muuaji, na nyangumi anayetoa spemaseti, ndio wanaoongoza utaratibu wa mlishano baharini. Yeye ndiye bingwa katika jamii ya papa, ni hodari kuliko wote. Yeye hula chochote—samaki, pomboo, hata papa wengine. Lakini kadiri anavyozeeka, kunenepa, na kukosa wepesi, anaanza kupendelea kula sili, pengwini, na mizoga—hasa nyangumi waliokufa.

Papa wengi hutafuta chakula kwa kutumia uwezo wao wote, kutia na uwezo bora walio nao wa kuona. Kwa kufaa wao huitwa pua inayoogelea kwa sababu ya uwezo wao mkubwa wa kunusa. Lakini, hata hivyo, wana uwezo mkubwa sana wa kusikia hivi kwamba hata wanaweza kuitwa masikio yanayoogelea.

Masikio ya papa hufanya kazi kwa kutumia chembe zilizo ubavuni mwa mwili wake zinazohisi kanieneo. Mfumo huu hunasa kila sauti, nao umezoea kunasa mtetemo wa vurugu—kwa mfano, samaki akitapatapa kwenye ncha ya mkuki. Hivyo, ni jambo la busara kwa wavuvi wanaotumia mikuki kuondoa samaki anayevuja damu na kutapatapa majini, haraka iwezekanavyo.

Papa wana uwezo wa kutambua pia. Sehemu ya ampullae of Lorenzini—vitundu vidogo vilivyo puani—huweza kutambua maeneo yenye uga-umeme hafifu unaotokana na mpigo wa moyo, kusonga kwa shavu la samaki, au misuli ya windo linaloogelea. Kwa kweli, uwezo wake wa kutambua ni wenye nguvu sana kiasi cha kumwezesha papa ahisi utendeano wa uga-sumaku wa dunia na wa bahari. Tokeo ni kwamba, papa waweza kujua upande wa kaskazini na wa kusini.

Kumtambua Papa-Mweupe

Japo anaitwa papa-mweupe mkubwa, ni sehemu ya chini ya mwili wake tu iliyo nyeupe au iliyo na rangi hafifu. Kwa kawaida mgongo wake ni wa rangi ya kijivu iliyokoza. Rangi hizo mbili hupakana ubavuni mwa samaki huyo na kutokeza mstari uliopindika ulio tofauti katika kila papa. Rangi hizo humwezesha ajifiche, lakini huwasaidia wanasayansi pia kumtambua kila papa.

Papa-weupe hukua kufikia urefu gani? “Papa-weupe wakubwa zaidi wanapopimwa kwa usahihi,” chasema kitabu cha Great White Shark, “huwa na urefu wa kati ya meta 5.8 na 6.4.” Samaki wenye ukubwa huo waweza kuwa na uzito wa zaidi ya kilogramu 2,000. Lakini, majitu haya hunyiririka majini kama makombora, kwa sababu ya mapezi yao yenye umbo la pembetatu yaliyojipinda nyuma na yanayoungana na pingiti lenye umbo kama la topido. Mkia wao wenye ulingano sawa na wenye nguvu, ni adimu sana miongoni mwa papa, kwa kuwa papa wengine huwa na mikia tofauti sana isiyolingana.

Sehemu zinazomtofautisha zaidi papa-mweupe na zenye kutisha ni kichwa chake kikubwa chenye umbo la pia, macho yake meusi yenye uhasama, mdomo wake uliojaa meno makali ajabu, yaliyochongoka yenye umbo la pembetatu. “Visu” hivi vikatavyo kuwili vinapovunjika au kung’oka, meno mengine hutoka safu ya nyuma na kuchukua mahali pake.

Damu Moto Huwatia Nguvu

Mfumo wa kuzungusha damu wa papa wa jamii ya Lamnidae, inayotia ndani mako, por-beagle, na papa-mweupe, ni tofauti sana na mfumo wa papa wengine wengi. Halijoto ya damu yao ni karibu nyuzi 3 hadi 5 Selsiasi zaidi ya halijoto ya maji. Damu yao moto huboresha umeng’enyaji na huwapa nguvu na kuwafanya wawe wastahimilivu. Mako, anayekula samaki wa baharini wenye mwendo wa kasi, kama vile jodari, aweza kutimua mbio ghafula kwa mwendo wa kilometa 100 kwa saa!

Papa wanapoogelea, huinuliwa na mapezi mawili ya kidari. Wanapoogelea kwa mwendo wa pole sana, wao hukwama na kuzama kama ndege, licha ya kwamba wanahifadhi mafuta mengi sana katika ini yanayowasaidia kuelea na ambayo huchangia robo ya uzito wote wa papa! Kwa kuongezea, ni lazima papa wa aina nyingi waendelee kuogelea ili waweze kupumua, wanapoogelea maji yenye oksijeni nyingi huingia mdomoni na kwenye mashavu. Hilo hutokeza sura yao isiyo na tabasamu daima!

Je, Yeye Ni Mla-Watu?

Kati ya jamii 368 za papa zinazojulikana, ni aina 20 tu zilizo hatari. Kati ya hizo ni aina nne tu zinazochangia visa vipatavyo 100 vya kushambulia wanadamu vinavyoripotiwa kila mwaka ulimwenguni pote. Mashambulizi 30 kati yake hutokeza vifo. Aina nne hatari ni papa aina ya bull, ambaye huenda amewaua wanadamu wengi zaidi kuliko papa mwingine yeyote, papa aina ya tiger, papa-cheupe, na papa-mweupe.

Ajabu ni kwamba, angalau asilimia 55—na katika sehemu nyingine za ulimwengu, takriban asilimia 80—ya watu walioshambuliwa na papa-mweupe walinusurika. Mbona wengi wamenusurika shambulio la mwindaji huyo anayehofiwa?

Kuuma na Kutema

Inajulikana kwamba papa-mweupe hutema windo lake baada ya kumwuma mara moja kwa nguvu. Kisha husubiri kiumbe huyo afe kabla ya kumla. Wanadamu wanaposhambuliwa, zoea hilo hutokeza fursa ya kuokolewa. Nyakati nyingine, msaada umetolewa na waandamani jasiri ikikazia hekima ya shauri la kutoogelea kamwe ukiwa peke yako.

Hata hivyo, majaribio hayo ya kuokoa yangetokeza kifo kama papa-mweupe hangekuwa na zoea jingine. Harufu ya damu haimtii kichaa cha kula kama papa wengine. Lakini kwa nini papa-mweupe hutumia mbinu ya kuuma na kutema?

Ni kwa sababu ya macho yake, akisia mwanasayansi mmoja. Tofauti na papa wengine, papa-mweupe hana utando mfano wa kope wa kulinda macho yake; badala yake, yeye huyazungusha mashimoni anapokaribia kugongana na kitu. Mara anapogongana, jicho hubaki wazi, labda hupigwa makucha na sili. Kwa hiyo, papa-mweupe huzoea kuuma haraka kwa nguvu zenye kufisha kisha kutema windo lake.

Kumbuka pia kwamba papa-weupe hutenda kama watoto wachanga wa binadamu—wao hutia mdomoni kila kitu ili kukionja! “Kwa kusikitisha, papa-mweupe mkubwa anapouma [kuonja] kila kitu matokeo yanaweza kusababisha msiba,” aeleza John West, mwanabiolojia wa Sydney wa viumbe wa baharini.

Ingawa papa-mweupe ni mnyama hatari, yeye si kiumbe mharibifu na mkatili anayetamani nyama ya binadamu. Mpiga-mbizi mmoja ambaye hukusanya moluska, alipokaa baharini kwa muda wa saa 6,000 alikutana na papa-weupe wawili tu na hakuna aliyemshambulia. Kwa kweli, mara nyingi papa-mweupe amewatoroka wanadamu.

Mvumbuzi wa bahari Jacques-Yves Cousteau na mwandamani wake walipokuwa wakipiga mbizi baharini karibu na Kisiwa cha Cape Verde, walikutana ghafula na papa-mweupe mkubwa ajabu. “Alitenda kwa njia ambayo hatukutarajia kamwe,” akaandika Cousteau. “Kwa woga mwingi, jitu hilo lilibwaga tuta kubwa la kinyesi na kutoroka kwa kasi sana.” Alimalizia hivi: “Nilipofikiria visa vyetu na papa-mweupe, niliduwazwa sana na tofauti kubwa iliyopo baina ya maoni ya umma juu ya papa-mweupe na tulivyomwona akitenda.”

Papa-Mweupe Awindwa

Maoni ya umma yameathiriwa sana na riwaya ya Jaws iliyoandikwa miaka ya 1970, iliyogeuzwa kuwa sinema inayopendwa. Ghafula papa-mweupe akaanza kuonwa kuwa kiumbe mwovu, na “makundi ya wawindaji wanaotafuta sifa yalishindana ili kuona ni nani angekuwa wa kwanza miongoni mwao kuchoma kichwa au mataya ya huyo mla-watu motoni,” chasema kitabu cha Great White Shark. Punde si punde, jino la papa-mweupe lililowekewa fremu lilikuwa likiuzwa dola zipatazo 1,000 za Marekani (huko Australia); na seti nzima ya mataya, zaidi ya dola 20,000.

Lakini mbali na hayo, papa-weupe wengi kupindukia hufa katika nyavu za wafanya-biashara. Kwa kuongezea, mamilioni ya papa wengine hunaswa kila mwaka ili kuridhisha wanunuzi wanaoongezeka upesi wa bidhaa za papa, hasa mapezi. Katika miaka ya majuzi, kwa sababu ya kupungua sana kwa idadi yao, onyo limekuwa likitolewa ulimwenguni pote kuhusu papa-weupe hasa.

Kupata Kuwaelewa

Papa wana sifa ya kuzunguka-zunguka baharini wakitafuta viumbe wagonjwa, wanaoelekea kufa, wadhaifu, na wafu. Hivyo, bahari yenye papa wengi, huwa safi na salama.

Tume ya Species Survival ya Shirika la Kimataifa la Kuhifadhi Mali-asili, ilipotambua hatari inayokabili papa, ilianzisha Kikundi cha Wataalamu wa Papa ili wachunguze matatizo yote ya papa. Hata hivyo, si rahisi kumchunguza papa-mweupe—hawazai sana, nao hufia uhamishoni. Kwa hiyo ni lazima wachunguzwe wakiwa katika mazingira yao ya asili.

Kadiri ambavyo wanadamu wamepata kuwafahamu zaidi papa, ndivyo maoni yao kuelekea viumbe hawa wenye kuvutia sana yamebadilika. Lakini hilo halimbadili papa-mweupe mkubwa. Ingawa yeye si mkatili, hata hivyo, yeye ni mnyama hatari na apasa kushughulikiwa kwa tahadhari na staha. Staha nyingi sana!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Papa-mweupe mkubwa, au papa-mweupe ana majina kadhaa ya kawaida. Kwa mfano, huko Australia, nyakati nyingine yeye huitwa white pointer; huko Afrika Kusini, blue pointer.

[Picha katika ukurasa wa 11]

Papa hawa wana midomo mikubwa yenye kutisha

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]

▼Photos by Rodney Fox Reflections ▸

South African White Shark Research Institute