Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Theolojia ya Ufanisi Niliona habari ya “Theolojia ya Ufanisi” katika makala ya “Kuutazama Ulimwengu” (Juni 22, 1999) kuwa yenye kupotosha sana, nikitumia maneno yasiyo makali. Makanisa yote ya Kipentekoste na ya karama hutia moyo upaji kwa kutegemea kanuni zifaazo za Biblia. Makala hayo yaliandikwa kwa nia ya kuhukumu.

C. B., Marekani

Makala yetu yalinukuu maneno ya mwanatheolojia Mlutheri Wanda Deifelt kwa usahihi na bila upendeleo kama yalivyoandikwa katika kijarida cha “ENI Bulletin,” cha Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Kama ilivyotajwa, makala ya kijarida hicho hayakuhusu makanisa ya Kipentekoste na ya karama kwa ujumla bali yalihusu makanisa hususa katika Amerika ya Latini.—Mhariri.

Vinland Ningependa kuwashukuru kwa ajili ya makala “Nchi ya Kihekaya ya Vinland Iko Wapi? (Julai 8, 1999) Nimependezwa kwa muda mrefu na watu wa Skandinavia na nilitumaini kwamba mngezungumzia habari hiyo. Hatimaye tamaa yangu imetimizwa.

S. S., Japani

Makala yenu ni yenye kuelimisha. Hata hivyo, naona uhitaji wa kurekebisha jambo moja. Wanahistoria wengi hutumia neno linalopendwa la “Waskandinavia” kurejezea tu mabaharia wa Norse ambao walivamia pwani ya Ulaya.

J. S., Marekani

“Amkeni!” liliwahoji wanahistoria kadhaa mashuhuri wa Norway na Greenland kuhusu jambo hilo. Mwafaka ni kwamba ingawa kwaweza kuwako ubishi fulani miongoni mwa wanahistoria kuhusu neno “Skandinavia,” neno “Waskandinavia” na “Norsemen” kwa wazi yana maana sawa kwa watu wanaosema Kiingereza.—Mhariri.

Mwokokaji wa Jela Ningependa kuwashukuru kwa moyo wangu wote kwa ajili ya makala “Mungu Amekuwa Msaidiaji Wetu.” (Juni 22, 1999) Nililia machozi ya shangwe niliposoma jinsi Francisco Coana alivyojifunza kweli na kufanya utumishi wa Yehova kuwa jambo kuu maishani mwake. Kusoma kuhusu majaribu yaliyowapata ndugu zangu Wakristo huko Msumbiji kwa kweli kulitia nguvu imani yangu.

J. H., Marekani

Wazazi Wagonjwa Niliguswa na makala ya “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Mama Ni Mgonjwa Sana?” (Julai 22, 1999) Sikufikiri kwamba kuna vijana wengine wengi ambao wana pendeleo kama langu la kumtunza mpendwa aliye mgonjwa. Nyanya yangu huishi nasi, naye amekuwa kitandani kwa miezi minne. Nilianza kulemewa sana na kuchoshwa kumtunza. Nilipata nguvu niliyohitaji sana niliposoma makala hayo. Yalinihakikishia utegemezo wa Yehova.

J. P., Filipino

Makala hayo yalinifariji sana, na kunipa nguvu za kumtunza mama yangu, aliye na mshuko-moyo. Niliweza kutumia madokezo yaliyotolewa na makala hayo ya kuona hali hiyo kwa njia halisi na kuonyesha hisia-mwenzi zaidi, uelewevu, na busara.

G. L., Italia

Makala hayo yalikuja kwa wakati barabara. Nina kansa, nami naishi na mwanangu. Mwanangu alikuwa akiteseka sana hivi kwamba sikujua tena jinsi ya kumfariji. Makala hayo yalieleza barabara hisia zake. Makala haya si ya vijana pekee. Yanahusu maisha yalivyo.

R. Z., Ujerumani

Makala hayo yalinisaidia ning’amue jinsi ilivyo muhimu kudumisha utendaji wa kiroho. Niligundua kwamba unaweza tu kumsaidia mgonjwa kwa kukazia Ufalme wa Mungu maishani mwako.

P. E., Austria