Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Nyama Isiyo ya Kawaida Yauzwa
Licha ya sheria za kimataifa zinazoharamisha uuzaji na ulaji wa nyama ya popo huko Ulaya, nyama hiyo inauzwa kinyume cha sheria kwenye maduka na mikahawa huko Uingereza. “Ni jambo linalohangaisha sana kwamba popo wanaolindwa wanauawa na kuuzwa kwa siri katika nchi nyingine, pia kuna hatari ya kiafya inayokabili umma kwa sababu ya kula nyama isiyokaguliwa,” asema Richard Barnwell, wa shirika la Hazina ya Ulimwengu ya Viumbe Asili. Katika sehemu fulani za Afrika, popo wala-matunda wamekuwa chakula muhimu kwa muda mrefu, na huko Malaysia na Indonesia, idadi ya baadhi ya popo wala-matunda walio adimu sana imepungua ghafula kwa sababu ya uuzaji wa nyama yao. Huko Shelisheli pia, mchuzi wa popo wenye viungo huonwa kuwa tunu. Hata hivyo, gazeti la The Sunday Times la London laripoti kwamba popo “si wanyama pekee walio hatarini wanaoliwa sana Ulaya.” Mikahawa ya Brussels, jiji kuu la Ubelgiji, inauza nyama ya sokwe.
Je, Wewe Hubabaika?
Takriban asilimia 15 ya watu wote wana vitabia vya wasiwasi, lasema gazeti la Globe and Mail la Kanada. Watafiti wanasema kwamba watu fulani hubabaika kwa “kusokota nywele, kugongagonga miguu chini, kutingisha miguu, kuuma-uma kucha na vitabia vingine kama hivyo.” Kwa nini watu hubabaika? Peggy Richter, daktari wa magonjwa ya akili katika Kituo cha Uraibu na Afya ya Akili cha Toronto, aamini kwamba misogeo hiyo ya kawaida hustarehesha. Kwa upande mwingine, mwanasaikolojia Paul Kelly asema kwamba kubabaika husababishwa na wasiwasi na ni itikio la ghafula linalozuka tu bila mtu kufahamu nalo huondoa mkazo. Kulingana na wataalamu, “waweza kujifunza kukatiza na hatimaye kuacha tabia hiyo kwa tiba ya kubadili mawazo—yaani, kukazia fikira kitu kingine unapogundua kwamba unababaika,” lasema gazeti la Globe.
Je, Ni Waraibu wa Kola?
Wamexico hunywa wastani wa lita 160 za vinywaji vya kola kila mtu kwa mwaka, laripoti Mexican Association of Studies for Consumer Defense. Kila mwaka, fedha nyingi zaidi hutumiwa kwa ajili ya vinywaji vya kola, kuliko zinazotumiwa kwa ajili ya vyakula kumi vya msingi zaidi. Baadhi ya watu wanasema kwamba kunywa vinywaji hivi baridi kupita kiasi ni mojawapo ya visababishi vikuu vya utapiamlo huko Mexico. Baadhi ya vitu vilivyomo katika Kola vinaweza kuzuia ufyonzaji wa kalisi na chuma. Matatizo mengine ambayo yanadhaniwa kuwa yanahusiana na unywaji wa kola hutia ndani hatari kubwa ya vijiwe vya figo, vijishimo kwenye meno, kunenepa kupita kiasi, na shinikizo la damu, kukosa usingizi, vidonda vya tumboni, na mahangaiko. ‘Tulikuwa “walaji-mahindi,”’ lasema gazeti la Consumer’s Guide Magazine, ‘lakini sasa waweza kusema sisi ni wanywaji wa “kola.”’
Je, Ni “Vita Adilifu”?
“Vita inayokumba Yugoslavia imetokeza migawanyiko halisi katika makanisa, kutokana na fasiri ya hoja ya kawaida ya ‘vita adilifu,’” lasema gazeti la Kifaransa la Le Monde. Wazo la vita adilifu (jus ad bellum) lilianza zamani wakati wa Augustine, aliyeishi katika karne ya tano. Kwa mujibu wa Le Monde, hoja za “kiadili” zinazotetea vita ya aina hiyo zilizotangazwa rasmi na mwana-falsafa Mkatoliki wa baadaye, Thomas Aquinas, zatia ndani hoja zifuatazo: Lazima kuwe na “sababu halali,” vita yapasa kuwa “uamuzi wa mwisho kabisa,” yule anayepigana vita lazima awe na “mamlaka halali,” na “silaha [hazipasi] kutumiwa kuleta madhara na mvurugo zaidi ila kusuluhisha tatizo.” Sharti jingine lililoongezwa katika karne ya 17 ni “uwezekano wa kufanikiwa.” Ingawa makanisa mengi sasa yanapinga wazo la “vita takatifu,” yanaendelea kujadili ile inayoonwa kuwa “vita adilifu.”
Vijana Wabrazili Wenye Kutenda Kingono
Katika Brazili, “asilimia 33 ya wasichana na 64 ya vijana wanaume hufanya ngono mara ya kwanza wakiwa na umri wa kati ya miaka 14 na 19,” laripoti gazeti la O Estado de S. Paulo. Kwa kuongezea, idadi ya wasichana Wabrazili wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 19 wanaoanza utendaji wa ngono kabla ya ndoa imerudufika katika muda wa miaka kumi tu. Kulingana na mtaalamu wa takwimu za kima cha uzazi Elizabeth Ferraz, kumekuwa na “badiliko kubwa katika mtazamo kuelekea ngono.” Kwa mfano, uchunguzi mwingine unaonyesha kwamba asilimia 18 ya wabalehe Wabrazili tayari wamezaa angalau mtoto mmoja au wana mimba sasa.
Hospitali Yenu Ni Salama Kadiri Gani?
“Wagonjwa wana uwezekano unaozidi 1 kwa kila 10 wa kuambukizwa magonjwa katika hospitali moja huko Ireland,” laripoti gazeti la The Irish Times. Maambukizo ya hospitalini (HAI), kama yanavyoitwa, huhitaji tiba zaidi na muda mrefu zaidi wa kulazwa hospitalini. Kwa wastani, kisa kimoja cha HAI chaweza kugharimu dola 2,200 za Marekani kwa kila mgonjwa, na huhitaji siku 11 zaidi za kulazwa hospitalini iwapo ni ambukizo la damu. Yanayohangaisha hasa ni maambukizo ya “vijidudu sugu,” ambavyo “vinazidi kukinza viuavijasumu vingi,” lasema gazeti hilo. Wale walio katika hatari ya kupata HAI ni “wazee-wazee, watoto wachanga, wale wanaolazwa hospitalini kwa muda mrefu, [na] wale walio na matatizo sugu kama vile magonjwa ya moyo au mkamba sugu.”
Kadirio la Idadi ya Chembe za Urithi Laongezwa
Hivi karibuni watafiti wamerekebisha kadirio la idadi ya chembe za urithi katika kila chembe ya mwanadamu hadi 140,000, laripoti gazeti la The New York Times. Makadirio ya awali yalikuwa chembe za urithi 50,000 hadi 100,000. Hili lamaanisha kwamba mwili wa mwanadamu ni tata zaidi ya ilivyofikiriwa awali. Chembe za urithi huagiza chembe za mwili kupanga asidi amino katika utaratibu unaofaa ili kufanyiza protini. Ongezeko hilo kubwa lililorekebishwa “laonyesha kwamba kuna mengi zaidi ya kujifunza kuhusu utaratibu wa chembe za urithi za mwanadamu,” lasema gazeti hilo.
Maoni Yaliyobadilika Kuhusu Helo
Kwa karne nyingi Kanisa Katoliki limefundisha kwamba helo ni mahali ambapo nafsi za watu waovu huteswa milele. Kwa wazi fundisho hilo limebadilika. Helo “si adhabu dhahiri kutoka kwa Mungu,” asema Papa John Paul wa Pili, “bali ni hali itokanayo na mitazamo na matendo ya watu katika maisha ya sasa.” Ndivyo linavyoripoti gazeti la L’Osservatore Romano. “Badala ya kuwa mahali,” papa asema, “helo huonyesha hali ya wale ambao kwa hiari na kwa wazi wanajitenga wenyewe na Mungu, chanzo cha uhai na shangwe kamili.” Yeye aongeza kwamba “adhabu ya milele” si kazi ya Mungu; badala yake, “ni kiumbe mwenyewe anayejitenga na upendo wa [Mungu].”
Kutembea kwa Ajili ya Afya
Pamoja na kukusaidia upunguze uzito na mkazo, matembezi husaidia kupunguza “shinikizo la damu na hatari ya kupatwa na mshtuko wa moyo,” lasema gazeti la The Globe and Mail, la Toronto. Kudumisha afya nzuri kunahitaji jitihada ya kutembea kwa muda ulioratibu. Muda mrefu kadiri gani? “Kwa mujibu wa kichapo Canada’s Physical Activity Guide to Healthy Active Living, iwapo unatembea kwa kasi ya wastani, unahitaji kujitahidi kutembea kwa muda wa dakika 60 kwa siku—kwa vipindi vya angalau dakika 10 kila kimoja.” Kutembea haraka au kuendesha baiskeli kwa dakika 30 hadi 60 kwa siku au kufanya zoezi la viungo la kukimbia kwa dakika 20 hadi 30 kila siku kwaweza pia kukufanya udumishe afya nzuri. Gazeti la Globe lapendekeza kutumia viatu vyepesi vilivyo wazi vyenye soli inayopindika, vinavyotegemeza nyayo vema, vyenye soli ya ndani yenye mto, na visivyobana vidole.
Onyo la Mapema
“Ulimwengu unaweza kutarajia mwongo wa ‘misiba mikubwa sana,’” laripoti World Press Review, likitegemea makala yaliyo katika gazeti la Financial Times la London. Huku likitaja misiba ya asili kama vile tufani na matetemeko ya dunia, Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na Shirika la Mwezi Mwekundu laonya kwamba idadi kubwa ya watu wanakabili hatari ya kukumbwa na misiba mikuu. “Majiji 40 kati ya majiji 50 yanayositawi haraka zaidi ulimwenguni, yako katika maeneo yanayokumbwa na matetemeko, na nusu ya watu ulimwenguni huishi katika maeneo ya pwani, yanayokabili hatari ya kufurika kwa bahari,” lasema gazeti hilo. Ishara nyingine ya kuogofya ni kwamba ingawa misiba inaongezeka, hazina ya serikali ya msaada wa dharura imepungua katika nchi nyingi.
Usiku Mrefu
“Giza tukufu.” Hivyo ndivyo mvumbuzi wa ncha za dunia wa Norway Fridtjof Nansen alivyoeleza “Mörketid,” au wakati jua linapokosa kuchomoza kabisa kaskazini mwa Norway. Kwa miezi miwili, mng’ao hafifu tu wa rangi nyekundu na kijivujivu huonekana kwa saa chache wakati wa mchana. Lakini si kila mtu anayefurahia kipindi hiki cha giza. Kulingana na gazeti la Ibbenbürener Volkszeitung, asilimia 21.2 ya Wanorway wanaoishi mbali na ukanda wa ncha ya dunia hushikwa na mshuko-moyo wa majira ya baridi kali. Huenda unasababishwa na ukosefu wa melatonini, homoni inayotokezwa ubongoni. Dawa pekee ni nuru. Hata hivyo, idadi kubwa ya watalii huvutiwa kuzuru ukanda wa ncha ya dunia na tepe za nuru zenye kumweka, mng’ao wa theluji kwenye mbalamwezi, na nuru yenye kuburudisha ya vijiji vilivyotapakaa.